Na GRACE HOKA- DAR ES SALAAM
SOKA ya Wanawale kwa Tanzania ilianza kuchezwa mwaka 2002, japokuwa kwa hapa nchini, ilichelewa tofauti na nchi nyingine.
Mara ya kwanza soka ya wanawake ilipoanzishwa hapa nchini, watu wengi walikuwa na mhemko wakitaka kuona jinsi akina dada watakavyokuwa wakicheza mchezo huo.
Kadri muda ulivyozidi kwenda, wengi walianza kuhamasika na kuwashawishi wasichana katika maeneo mbalimbali kujitosa kwenye mchezo huo unaotajwa kuongoza kwa kupendwa kila pembe ya Dunia.
Hata wazazi, hasa wa Dar es Salaam, walianza kuonekana kuukubali mchezo huo na kuwaruhusu mabinti zao kuucheza.
Baada ya mchezo huo kushamiri katika maeneo mbalimbali, huku timu lukuki zikianzishwa, hatimaye iliundwa timu ya Taifa iliyopachikwa jina la Twiga Stars.
Kuundwa kwa Twiga Stars, yalikuwa ni matokeo ya kuimarika kwa timu za wanawake kama Sayari Queens, Mburahati Queens, JKT Queens, Future Queens na nyinginezo.
Timu ya Taifa, kwa wakati huo ilikuwa ikinolewa na marehemu, Athuman Machuppa ambaye aliwajengea msingi imara wachezaji waliokuwapo katika kikosi hicho na baadaye kuwika vilivyo.
Baada ya soka kupamba moto jijini Dar es Salaam, ilianza kusambaa katika mikoa mbalimbali, kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani.
Matokeo yake, ikapatikana timu imara iliyopata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambako ilifanya maajabu kwa kuzitambia nchi zilizoanza mchezo huo muda mrefu.
Ni kutokana na hali hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa agizo kwa kila mkoa kuwa na timu za soka za wanawake, jambo lililotekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mbali ya mikoa, agizo lilitolewa kwa shule kuanzia za msingi hadi sekondari kuwa na timu za soka za wanawake kama sehemu ya kuuhamasisha mchezo huo.
Kupitia mkakati huo, wasichana wengi wakawa wamejitokeza kuucheza mchezo huo, tena wakionyesha vipaji vya hali ya juu kuliko hata baadhi ya wanaume.
Hatimaye Tanzania ikawa kinara wa soka la wanawake katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na kuzifunika Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na nyinginezo.
Mafanikio hayo yote hayakuja hivi hivi, bali yametokana na jitihada za makusudi zilizofanywa na TFF, tangu ilipokuwa chini ya Rais, Leodegar Tenga hadi Jamal Malinzi anayeelekea kumaliza muda wake.
Tenga na Malinzi, kwa kufahamu umuhimu wa soka la wanawake, walianzisha Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) ambapo mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa ni Madina Mhando.
TWFA imeendelea kushirikiana na TFF kuufanikisha mchezo huo ambapo kwa sasa inaonekana wazi soka la wanawake linaweza kufika mbali kutokana na mikakati ya uongozi wa chama hicho, hasa huu mpya ulioingia madarakani hivi karibuni.
Viongozi wapya wa TWFA waliochaguliwa hivi karibuni, ni Mwenyekiti, Amina Ngaluma ambapo Katibu wake, ni mwanahabari mahiri na mkongwe, Somoe Ng’itu.
Wakizungumza na MTANZANIA mara baada ya kuingia madarakani, viongozi hao wametamba kulipaisha soka la wanawake nchini.
Hata hivyo, Amina na Somoe, wanakabiliwa na changamoto kubwa inayoukabili mchezo huo ambayo kwa kiasi fulani inaonekana kutishia ushiriki wa watoto wa kike katika soka.
Changamoto hiyo si nyingine, bali ni tabia ya wasichana wanaocheza soka kuiga tabia za kiume na hivyo kupoteza uhalisia wao kama wasichana.
Kwa sasa wasichana wanaocheza soka, ni aghalabu kuwakuta wakiwa wamevaa mavazi ya kike, zaidi ya kuvaa suruali, ‘pensi’, fulana, kofia za kiume na nyinginezo.
Mbaya zaidi, uvaaji wao huwa hauna tofauti na wanaume, hasa suruali ambapo hupenda kutumia mtindo maarufu wa ‘kata k’, yaani mlegezo.
Lakini pia, utembeaji wao huwa wa kitemi kama wanaume, ikiwamo uzungumzaji wao kiasi kwamba unaweza usimfahamu kama ni mwanamke unapokutana naye.
Hali hiyo inaonekana kuwashtua wazazi na walezi wengi kama ilivyo kwa jamii inayowazunguka.
Ni vema ikafahamika kuwa mwanamke ni mwanake tu, anatakiwa kuvaa mavazi ya kike, kuzungumza kama mwanamke, lakini pia matendo yake kuwa kama motto wa kike, licha ya kucheza soka.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wanasoka wa kike wa hapa nchini, huko Ulaya na kwingineko, wanasoka wanawake huwa na kila sifa anayostahili kuwa naye mtoto wa kike.
Hivyo basi, wakati viongozi wapya wa TWFA wakiwa wanajipanga kuupeleka mbali mchezo huo, ni vema wakaangalia ni vipi wanaweza kukomesha tabia ya wachezaji wanawake kuwa na tabia za kiume ili mwisho wa siku, waweze kuwashawishi wazazi kuwaruhusu mabinti zao kujikita katika soka.