33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

STARS INABADILIKA, GONJWA LILE LILE

Na MARTIN  MAZUGWA-DAR ES SALAAM


TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeondolewa katika hatua ya awali ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN) kwa bao la ugenini.

Mashindano ya CHAN safari hii yanatarajia kufanyika nchini Kenya mapema mwakani, huku Tanzania tukiendelea kuwa watazamaji kwa mara nyingine.

Stars ambao walilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani kabla ya juzi, kulazimishwa tena sare ya bila kufungana nchini Rwanda na kuaga kwa mara ya pili mfululizo hatua ya awali.

Licha ya makocha kubadiLishwa na wachezaji wapya kuingia katika kikosi, lakini bado Tanzania imekuwa ikifanya makosa yaleyale miaka nenda rudi.

Hatua ya awali imekuwa saizi yetu

Hii ni mara ya pili kwa Stars kuondolewa katika hatua ya awali, kwani mwaka 2015 pia  iliondolewa kwa mabao 4-1 kutoka kwa Uganda ‘The Cranes’ wakianza kwa kupoteza mabao 3-0 katika uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, kabla ya kwenda kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Mandela uliopo Namboole.

Mara ya mwisho kikosi cha Tanzania  kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji ndani CHAN, ilikuwa mwaka 2008 wakati huo kikosi kikiwa chini ya kocha Mbrazili , Marcio Maximo katika mashindano hayo       yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Ivory Coast, ambapo hata hivyo stazi iliishia hatua ya    makundi.

Uchaguzi wa kikosi kwa mazoea

Miaka ya karibuni kikosi cha timu ya Taifa, Tanzania, kimekuwa kikiitwa kwa mazoea jambo linalofanya tushindwe kutibu gonjwa letu la nenda rudi, huku wale tuliokuwa tumewaacha wakitupita kila kukicha.

Kitendo cha kuachwa kwa wachezaji wa kikosi bora cha msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Salum Kimenya pamoja na mfungaji bora Abdulrahman Mussa, ambao waliachwa bila sababu inaonyesha ni jinsi gani ambavyo hatupo makini katika kutafuta kitu bora.

Hakukuwa na ulazima wa kulazimisha nyota waliokaa nje nusu msimu na kuwaacha nyota bora, ambao walikuwa fiti msimu mzima siwezi kuingilia majukumu ya kocha lakini kwa hili alichemka.

Makosa yanayojirudia katika safu ya ulinzi

Moja kati ya idara zenye mapungufu makubwa ni sehemu ya ulinzi ambayo ipo chini ya himaya ya Salim Mbonde na Nurdin Chona, Gadiel Michael pamoja na Shomari Kapombe wamekuwa wakikosa mawasiliano mazuri, hasa timu inapokuwa inashambuliwa wanashindwa kupeana majukumu.

Tatizo lilianza kuonekana katika mashindano ya COSAFA mchezo wa nusu fainali dhidi ya Zambia, ambao Stars ilipoteza kwa mabao 4-2 huku mabao mawili yakipatikana kwa njia ya  mipira mirefu ambayo ilishindwa kuzuiliwa mapema na mwisho ikazaa bao.

Tatizo hilo  ambalo halikufanyiwa kazi mapema limejitokeza pia katika mchezo wa awali wa kuwania kufuzu  CHAN, ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1, huku Wanyarwanda wakitumia udhaifu ule ule kujipatia bao kwa mpira mrefu ambao walinzi wa Stazi walishindwa kuuzuia kabla ya kumfikia mchezaji aliyetoa pasi ya mwisho.

Ubutu wa safu ya ushambuliaji

Bado Tanzania inakabiliwa na ubutu wa safu ya ushambuliaji hii inatokana na timu zetu kufanya usajili mkubwa kwa washambuliaji kutoka nje ya nchi jambo linalosababisha washambuliaji wetu kukosa nafasi ya kucheza hivyo kuongeza matatizo kwa timu yetu ya Taifa.

Tanzania hivi sasa ina washambuliaji kama vile Mbwana Samata, Elius Maguri, John Bocco, Abdulrahman Musa, John Bocco, Mbaraka Yusuph ambapo hadi sasa nyota pekee ambaye anaweza kuvaa viatu vya wakongwe ni Sammata anayekipiga  nchini Ubelgiji ambaye katika michezo 39 amepachika mabao 14.

Hatuna mshambuliaji wa uhakika, ambaye anaweza kuvaa viatu vya wakongwe kama vile Peter Tino pamoja na Zamoyoni Mogela ‘Golden boy’ jina alilopachikwa na kocha Rudi Gutendorf ambaye alimwita jina hilo kutokana na kasi yake ya upachikaji mabao.

Hadi sasa ni Mrisho Ngassa, ambaye ndiye kinara wa upachikaji mabao katika timu ya taifa kwani katika michezo 99 aliyoshuka dimbani amezifumania nyavu mara 24.

Kutotumia vyema uwanja wa nyumbani

Moja ya makosa ambayo yamekuwa yakitugharimu miaka ya karibuni ni kushindwa kuutumia uwanja wa nyumbani ambao umekuwa ukituhukumu kila mwaka.

Mara nyingi timu mbalimbali zimekuwa zikitumia uwanja wa nyumbani kama silaha kutokana na sapoti ya mashabiki lakini kwa Tanzania jambo hilo ni nadra sana kuliona.

Angalia sare dhidi ya Algeria ya bao 2-2 mchezo wa kufuzu mataifa ya Afrika nchini Gabon, lakini pia dhidi ya Lesotho ya bao 1-1 ya kufuzu fainali ya mataifa ya Afrika ni kati ya mifano ambayo tunaweza kujifunza kupitia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles