26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Vitambi hupunguza uwezo kushiriki tendo la ndoa – Daktari

AVELINE KITOMARY

KITAMBI au kiribatumbo ni hali ya tumbo kuwa kubwa, ambapo huchomoza mbele na wakati mwingine kunig’inia. 

Kitambi kinasababishwa na ongezeko la mafuta mwilini ambayo huwa yanakuja kutunzwa katika eneo la tumbo hasa kwa wanaume.

Utunzanji wa mafuta kwa wanawake ni tofauti kidogo kwa sababu wao hutunzwa kwenye matiti, makalio na wakati mwingine kwenye tumbo.

Wataalamu wa afya wanasema hali ya mafuta mengi mwilini inatokana na aina ya ulaji, huku vyakula hivyo vikiwa havina kazi na kuwekwa sehemu za kuhifadhia.

Uwapo wa mafuta ya ziada mwilini hasa  kwa wanaume hufanya tumbo kuwa stoo (ghala) la kuhifadhi mafuta.

Mara nyingi katika jamii watu walio na kitambi wamekuwa wakionekana katika picha nzuri kuwa wana afya njema na uwezo kiuchumi.

Na wakati mwingine watu hao wamekuwa wakijivunia kuwa katika hali hiyo huku wakiona ufahari kwao, hii ni kwa upande wa wanaume tu.

Lakini sio wanaume wote hupenda kuwa na kitambi, wengine wanajitahidi kufanya mazoezi ili waweze kupunguza au kuondoa kabisa.

Kwa wanawake mambo ni tofauti, wengi huchukia kuwa na vitambi hii ni baada ya kuwaharibia mwonekano wao wanaoupenda.

Hakuna utafiti unaoonesha kuwa kitambi  kinarithiwa kwa wanaume, hutokea baada ya kupunguza ufanyaji wa  kazi tofauti na mwanzo hasa pale umri unaposonga.

HUATHIRI UPUMUAJI

Katika makala haya, tutazungumzia madhara ya kitambi kwa wanaume na hatua mbazo zinapaswa kuchukuliwa ili kuweza kupunguza kitambi.

Mkuu wa Idara ya Utengamao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Abdalah Makala, anasema kitambi huweza kusababisha matatizo katika mfumo wa upumuaji.

“Mafuta yanafaida mwilini lakini pale yanapozidi yanakuwa na madhara katika afya na madhara makubwa ya mtu mwenye tumbo kubwa ni msuli  wa upumuaji unaoitwa diaphragm kukosa  nafasi nzuri  ya kushuka na kupanda.

“Kwahiyo, unapokosa nafasi yake na kutokuwa huru inapunguza uwezo wa kupumua vizuri ndo maana mtu akiwa na kitambi akitembea kwa haraka anachoka na kuanza kupumua kwa shida,” anaeleza.

Anasema kuwa madhara mengine ya mafuta hayo ni kusababisha mishipa ya damu kuziba hivyo kuleta athari mwilini kwa kusababisha magonjwa mengine.

“Athari nyingine inayoweza kutokea ni presha ya juu na kisukari, ambapo haya ni magonjwa yaliyofanyiwa utafiti.

Lakini pia, utafiti mmoja unaonesha hata vifo vya mapema vinatokana na kuongezeka uzito uliokithiri,” anaeleza Dk. Makala.

HUATHIRI NGUVU ZA KIUME

Kwa mujibu wa Dk. Makala mafuta yanapoongezeka mwilini yanaweza kuathiri uwezo wa misuli kufanya kazi hivyo, kusababisha kupungua kwa uwezo wa tendo la ndoa.

“Mafuta yanapoongezeka mwilini yanaathari nyingi ambayo ni kupunguza uwezo wa misuli kuvumilia kwenda umbali mrefu hivyo, kufanya mtu kuchoka haraka na kwenye kuchoka inaweza kusababisha athari katika nguvu za kiume.

 “Hali hii inaweza kusababisha mwanamume kuwa na uwezo mdogo katika ufanyaji wa tendo la ndoa,” anasema.

MATUMIZI YA MIKANDA KATIKA KUPUNGUZA TUMBO

Baada ya kitambi kuonekana kero, wapo wanaume ambao wanatumia njia mbalimbali ili waweze kuvipunguza.

Wengine hufanya mazoezi, lakini pia wapo wanaume wanaotumia mikanda/belt  kuhakikisha wanafanikiwa kupunguza tumbo.

Dk. Makala anasema upunguzaji wa kitambi kwa kutumia mikanda huenda isiwe njia sahihi kutegemeana na mhusika.

“Kuna aina mbalimbali za mkanda, ipo inayotumika kwaajili ya mgongo ambayo husaidia kushikilia misuli hasa mhusika anapokuwa na maumivu ya mgongo.

 “Lakini pia kuna mikanda inayosaidia   mtu kulingana na udhaifu wa misuli alionao hivyo, wapo watu wanaosema ukivaa mikanda unaweza kuwa na faida kwenye misuli ya tumbo lakini hili si kwa wote.

 “Sio sahihi wanaume kuvaa mikanda/belt  ya tumbo, kwani tafiti zinaonesha kuwa kadiri misuli inaposaidiwa ndivyo inavyozidi kuwa dhaifu – yaani  unavyoshikilia unauondolea uwezo wa kutanuka,” anasema Dk. Makala.

JINSI YA KUPUNGUZA KITAMBI

Dk. Makala anashauri njia bora ya kupunguza kitambi kuwa ni kubadilisha  aina ya ulaji na kufanya mazoezi kwa kiasi.

Pia anashauri ni vema kuwaona wataalamu wa afya ili kuweza kuelekeza namna bora ya aina ya vyakula na aina ya mazoezi yanayotakiwa kufanyika kulingana na jinsi mtu alivyo.

“Yapo mazoezi ya aina nyingi ambayo yanapunguza tumbo kabisa, ni vyema kuwaona wataalamu husika watakulekeza namna bora ya kufanya mazoezi yatakayosaidia kupunguza mafuta mwilini  na udhaifu wa misuli.

“Siku hizi tunaona watu wanakimbia kama njia ya kufanya mazoezi, lakini wengine wanakimbia siku ya Jumamosi tu baada ya hapo hakimbii tena anaenda baa na kunywa pombe, sasa utafikiria ile sukari inayoingia mwilini inakazi gani wakati haitumiki?” anahoji.

Anashauri watu kubadilisha mlo hasa  wa jioni badala ya kula vyakula vizito wale vyakula  vilaini kutokana na kutotumika mwilini kwa wakati huo.

 “Utakuta usiku mtu anakula chakula kingi na akishakula hakifanyiwi kazi, baadaye kinabadilishwa kuwa mafuta na yanatunzwa.

“Kitu kingine mtu anapokuwa amekula usiku anatakiwa ajipe saa mbili kabla ya kwenda kulala hivyo, muda bora wa kula ni saa moja ili chakula kisagwe na tunatakiwa tule kidogo tu.

 “Vyakula vya wanga kama ugali, wali, mihogo usiku sio vizuri, ni vema kula hivi kwa nyakati za asubuhi kwani wakati huo unaenda kufanya kazi na kitatumika ipasavyo,” anaeleza Dk. Makala.

Anashauri watu kubadilisha mfumo wa maisha kwa kutembea katika sehemu za karibu badala ya kuchukua usafiri au kupanda ngazi badala ya lifti.

“Mtu anatakiwa kukimbia dakika 90 kwa wiki nikimaanisha dakika 30 kwa siku tatu kama unakazi na kama unatembea haraka basi angalau dakika 150 kwa wiki maana yake ni dakika 30 kwa muda wa siku tano.

“Mazoezi ni pale unapopanga kuwa unaenda kufanya kwa sababu ubongo una kazi ya kukariri hata mazoezi usipobadilisha unakuta unazoea, kama ulizoea kuzunguka uwanja mara mbili siku inayofata unaongeza hadi mara tatu.

“Tafiti zinaonesha kwamba kama utatembea hatua 1,500 kwa siku, inasaidi kupunguza uzito lakini hivi vitu vinaendana na aina ya vyakula,” anasema Dk. Makala.

MAZOEZI HUONGEZA NGUVU ZA KIUME

Dk. Abdallah Makala anashauri kuwa ufanyaji wa mazoezi una nafasi kubwa na njia bora zaidi katika kuongeza nguvu za kiume.

Anataja mazoezi yanayoweza kuongeza uwezo wa tendo la ndoa kuwa ni kukimbia, kucheza mpira, kuogelea na mazoezi mchanganyiko.

Hivyo, anapinga matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume huku akibainisha kuwa utumiaji wa supu ya pweza hauongezi nguvu za kiume.

“Katika kuhakikisha afya inakuwa njema kila siku kwa wanaume, tafiti zinaonesha kuwa hawahitaji kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.

“Utafiti uliofanyika unaonesha kuwa pamoja na mazoezi kusaidia kupunguza madhara kama kisukari, magonjwa ya moyo lakini pia yanachangia uwezo katika ufanyaji wa tendo la ndoa.

“Utafiti uliofanyika ambao watu walipewa mazoezi kwa miezi tisa, ulionesha hawa watu waliongeza uwezo wa kufanya tendo la ndoa, uwezo wa kuridhika katika kufanya tendo la ndoa na uhusiano ukaboreka zaidi,” anabainisha Dk. Makala.

Anaeleza kwamba kwa wanaume, homoni za kiume za testestrone zinasukumwa na  mazoezi wanayofanya.

“Mazoezi kama  kukimbia, kucheza mpira, kuogelea pamoja na mchanganyiko wa mazoezi kama kuruka kamba, kunyanyua kitu na mengineyo, utafiti unaonesha wanaume hao wakifanya mapenzi walionekana kuwa vizuri zaidi lakini walikuwa wamefanya mazoezi siku sita kabla. 

“Kwa vijana, wakifanya mapenzi wanatumia kiasi cha mafuta (carol) moja ni sawa na mtu aliyetembea mwendo wa kiasi, pia kuna utafiti ulifanyika mtu ambaye amefanya mazoezi ya kukimbia katika mashine kwa dakika 30 alitumia nguvu mara tatu zaidi ya mtu aliyefanya tendo la ndoa, mtu huyo alichoma carol (kiasi cha mafuta) tatu 3,” anafafanua Dk. Makala.

Anasema kwa upande wa wanawake pia utafiti ulionesha mazoezi yalionesha faida nzuri ikiwamo mwili kuchangamka kufanya tendo la ndoa na wakawa wanaridhika mapema.

“Ilionekana kwamba wanawake ambao wanaendesha baiskeli kwa muda wa dakika 20 hawa mzunguko wa damu uliongezeka.

“Kwa upande wa wanawake kucheza mpira, kuogelea, kuendesha baiskeli na mengine yanasaidia lakini wakifanya mapenzi kabla ya kuingia kwenye mazoezi hupata udhaifu kwenye mwili ni bora kufanya kwanza mazoezi kabla kufanya tendo hilo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles