31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nchi 15 zaruhusiwa kuleta waangalizi wa uchaguzi

 MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

NCHI 15 kupitia balozi zao nchini, zimeruhusiwa kuleta waangalizi wa kimataifa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilisema uamuzi huo umefikiwa baada ya balozi za nchi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu.

Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfred Fanti.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza umekuwa tofauti na miaka iliyopita kwa kuwa unafanyika kwa kugharamiwa na fedha za ndani badala ya wahisani jambo ambalo baadhi ya watu walianza kuhofia kutokuwepo kwa waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi.

“Huu ni Uchaguzi Mkuu ambao kwa mara ya kwanza kwa asilimia 100 tunaugharamia sisi wenyewe kama Serikali ya Tanzania.

“Utaratibu wa uchaguzi chini ya sheria ya uchaguzi na chini ya utaratibu wa kimataifa huwa tunakuwa na waangalizi wa uchaguzi, mwaka huu nchi hizo 15 kupitia balozi zao zimepata kibali mara baada ya kufuata taratibu za kuomba kuleta waangalizi wa Uchaguzi Mkuu,” alisema Profesa Kabudi.

 Mbali na Balozi wa Umoja wa Ulaya, pia Profesa Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni na baadae Balozi wa Poland nchini, Krzysztof Buzalski.

Profesa Kabudi aliwakabidhi vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu namna uchaguzi unavyoendeshwa nchini, hasusani baada ya uwepo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani kuhusu kuenguliwa kwa wagombea wao. 

Kwa upande wake, Balozi Fanti alisema nchi za Umoja wa Ulaya zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mchakato wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zinavyoendelea nchini ambapo hadi sasa wanaridhishwa na kampeni zinavyofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na zoezi la uangalizi wa uchaguzi huo. 

Balozi wa Italia, Mengoni, alisema amevutiwa na namna vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote kwa uhuru na bila ya ubaguzi na kupongeza namna Watanzania wanavyojitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea mbali na tishio la corona na kwamba ana imani kuwa kiongozi atakayechaguliwa atakuwa ametokana na utashi wa wananchi.

 Mbali na masuala ya Uchaguzi Mkuu, Profesa Kabudi na mabalozi hao wamejadili pia masuala ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, maendeleo ya kiuchumi, biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles