27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukatili wanaopitia kina mama, watoto Mufindi

Kanky Mwaigomole.

MAMA anaporudi nyumbani akitokea kwenye mihangaiko yake ya kutafuta kipato, anategemea akifika huko acute amani, watoto wake wakiwa salama. Siku zote hilo ndio tabasamu kubwa hasa la mama.

Ila ripoti iliyowahi kutolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa na Uhalifu, (UNODC), inasema nyumbani ni mahali hatari zaidi hasa kwa wanawake wengi duniani, hii ni kutokana na baadhi ya wanawake kupoteza maisha mikononi mwa wenzi wao au familia.

Ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni tatizo linaloleta fedheha kubwa katika jamii nyingi iliyopo Halmashauri ya Mufindi, mkoani Iringa.

Serikali kwa kushirikiana na taasis zisizo za kiserikali za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake (UN WOMEN), pamoja na Uniliver Tanzania, wameanzisha kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia, wakiwa na kauli mbiu insemayo: ‘Ulinzi wa mama na mtoto ni msingi wa maendeleo.’

Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Sechelela Dagaa, anasema kuwa kampeni hiyo imeanza Agosti mwaka huu, na itaisha Septemba mwaka huu, ikiwa na lengo la kuwaelimisha wanawake pamoja na wanaume wilayanï Mufindi kuhusu vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia.

Kwa mujibu wa Sechelela, takwimu wilayani Mufindi zinaonyesha kuwa wanawake ndio wahanga wa ukatili wa kijinsia kutokana na wanawake hao kutoa taarifa kwa wakati wanapofanyiwa ukatili, tofauti na wananaume.

Sechelela anakiri kuwapo kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume, japo wengi wao hawatoi taarifa kwa kuhofia kunyanyapaliwa na jamii, kutokana na mila na desturi zinazo mwangalia mwanamume.

Kampeni hii inafanyika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, katika mashamba ya chai na kata zinazo zunguka mashamba hayo. Hii ni kutokana na wafanyakazi wengi hawapati fursa ya kupata elimu ya ukatili wa kijinsia.

Anasema mwamko umekuwa mkubwa kwani wananchi wengi wemejitokeza kuuliza mswali na kutaka kufahamu ni wapi wanaweza kupata msaada wa kisheria, endapo wanapitia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi na ndani ya familia.

Anaongeza kuwa miongoni mwa changamoto walizozipitia tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo, ni pamoja na muda mdogo uliopo wa kuelimisha jamii, hii ni kwa sababu watu wengi huwa mashambani wakifanya kazi.

Sechelela anatoa rai kwa wanaume kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya kikatili dhidi yao, ili nao waweze kupata msaada wa kisheria.

Anasema ukatili wa kijinsia ni kitendo anachofanyiwa mtu yeyote awe mwanamke au mwanamume, kwa lengo la kumdhuru au kumuumiza kisaikolojia, kimwili, kiafya, kingono na kiuchumi.

Lengo la kampeni hii ni kupaza sauti pamoja na kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii ya Halmashauri ya Mufindi.

Aidha, wakati wa kampeni hiyo wananchi wamepata fursa ya kuuliza na kujibiwa maswali yanayohitaji ufafanuzi wa kisheria ambapo Hakimu Mkazi Mfawadhi wa Wilaya ya Mufundi, Maua Hamduni, anasema kampeni hiyo itasaidia kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Miongoni mwa sheria ambazo Maua alizitolea ufafanuzi kwa undani zaidi ni pamoja na sheria ya mirathi, ambapo wanawake wengi huathirika kutokana na kutokujua sheria hiyo.

Amina Saleh (55) ni mjane aliempoteza mume wake miaka saba iliyopita, anasimulia namna alivyopokonywa mashamba ya marehemu mume wake mara baada ya msiba kuisha.

“Mimi na marehemu mume wangu tulikua tunalima zao la mahindi, ambalo lilikuwa linatuingiza kipato na kusaidia kuendesha maisha yetu ya kila siku, lakini hali ilibadilka baada ya mume wangu kufariki, kaka wa marehumu mume wangu waligawana mashamba yote bila hata kuniachia shamba hata mmoja la kulima ili niweze kuwahudumia watoto,” anabainisha mjane huyo.

Miradi mingi ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto imeanzishwa sehemu mbalimbali ulimwenguni, lakini bado wanawake wanakabiliwa na visa vya unyanyasaji wa kingono na kiuchumu,  ambavyo kwa kiasi kikubwa haviripotiwi. Lakini pia wanawake na watoto hususani katika kaya masikini, huozeshwa na wanaume wenye umri mkubwa badala ya kupewa fursa ya kumaliza masomo yao.

Kulingana na tafiti iliyofanywa na UNICEF, takribani wasichana watatu kati ya 10 na mvulana mmoja kati ya saba wameripoti kutendewa walau tukio moja la ukatili wa kijinsia kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 wakati asilimia sita ya wasichana wamelazimishwa kujamiiana kabla hawajatimiza miaka 18.

Imebainika kuwa watu waliotenda ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana walikuwa wana umri mkubwa kuliko waathirika.

Matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wasichana na watoto yalitokea mara nyingi zaidi majumbani, shuleni au njiani kwenda au kutoka shuleni.

Meneja Mradi wa Kupinga Ukatili wa Kijinisia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake (UN WOMEN), Lucy Tesha, anasema ukatili wa kijinsia unaweza kukomeshwa endapo elimu itawafikia walengwa.

“Unaweza ukakuta binti mwenye umri chini ya miaka 18 ameingiliwa kinguvu lakini hajui ni wapi anaweza kwenda kupata msaada wa kisheria, au hana uelewa kwamba anatakiwa kutoa taarifa ya tukio lilomkuta baada ya muda gani ili ushahidi usipotee,” anasema.

Tesha anaongeza kuwa baadhi ya watu hawafahamu kuwa serikali inatoa huduma bure, katika dawati la jinsia kwenye vituo vingi vya polisi na kwamba Jeshi la Polisi liko mstari wa mbele kutokomeza vitendo vya ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Lucy anaongeza kuwa wanawake wengi pia hukumbwa na unyanyasaji wa maneno na kiuchumu, ila bado hawatambui kuwa vitendo hivyo ni miongoni mwa unyanyasaji wa kijinsia.

Veronica Mlelwa, ni mwanamke wa miaka 28, ambaye alinga’twa nyama ya mdomo wake wote wa juu, wakati wa mabishano kati yake na mumewe, baada ya kupika chakula ambacho hakikukolewa chumvi vizuri.

“Tabia ya kung’ata na kunyofoa sehemu ya mdomo imekuwa ndio desturi hapa Mufindi. Mume wangu alinipiga kupita kiasi na baada ya hapo akaona haitoshi akanig’ata na kukinyofoa kipande cha mdomo wangu. Tulipelekena kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye alishindwa kuamua ugomvi kwa sababu wana undugu, kwahiyo tukarudi nyumbani nami nikaendelea kuuguza kidonda change,” anasimulia.

Veronica anasema kuwa wanawake wengi wanapigwa, ila wananyamazishwa kwa kuambiwa kuwa vitendo hivyo sio unyanyasaji bali ni mume anaamua kumuadabisha mkewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles