29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vita yaathiri huduma za afya Ukraine

Residents collect water at a pumping station in SlavianskVita imesababisha vifo na ulemavu kwa maelfu ya watu mashariki mwa Ukraine.Na Joseph Hiza na Mashirika ya Habari

PANDE mbili zinazopingana katika mgogoro wa mashariki mwa Ukraine zilifikia makubaliano wiki iliyopita, hatua ambayo imeleta utulivu kufuatia kusimama kwa mapigano katika sehemu kubwa ya eneo hilo.
Kusitishwa kwa mapigano kunatarajia kuleta ahueni ya kukabiliana na changamoto kubwa ya kiafya eneo hilo ambalo lilikuwa halifikiki kwa wafanyakazi wa misaada.
Hata hivyo, katika mji wa Debaltseve uliozingirwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi matukio machache ya mapigano yameendeelea kushuhudiwa kutokana na waasi wa eneo hilo kudai kutotambua makubaliano hayo yaliyofikiwa mjini Minsk, Belarus.
Makubaliano hayo yalifikiwa kati ya waasi na Urusi kwa upande mmoja na Serikali ya Ukraine na Umoja wa Ulaya (EU) kwa upande mwingine.
Ukiachana na hilo, watu waliotengwa katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kupata huduma za msingi za afya.
Hali hiyo ilihatarisha kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo mkubwa wa kibinadamu, kitu kinachoweza kutokea iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa au iwapo mapigano yatarudia upya.
Mzozo huo umewaathiri watu zaidi ya milioni tano, huku milioni 1.4 wakielezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwa wanakabiliwa na kitisho kikubwa.
Hiyo ni kwa sababu ya kulazimika kuyakimbia makazi yao, ukosefu wa kipato na kusambaratika kwa huduma muhimu, zikiwamo za afya.
Mapigano pamoja na hatua zilizochukuliwa na pande husika katika mzozo huo zimesababisha mahitaji ya dawa kutatizwa kwa kiwango kikubwa au kukatika kabisa.
Hospitali zimeharibiwa au kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maji, umeme na uhaba wa wafanyakazi katika vituo vya afya huku maafisa wa afya wakiyakimbia mapigano.
Kukosekana kabisa chanjo kunatishia kutokea milipuko ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kupooza na surua.
Kuna wasiwasi miongoni mwa watu wanaoishi na ugonjwa hatari wa Ukimwi na Kifua Kikuu, huku usafirishaji wa dawa muhimu ukiwa umekwama kabisa na juhudi za kufuatilia magonjwa zikiwa karibu haziwezekani.
Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa (UN) idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na mgogoro wa mashariki mwa Ukraine ni 700,000, ambao sasa wamegeuka kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao.
Idadi hiyo inasemekana ilikuwa inaongezeka kwa 100,000 kila wiki huku mamia kwa maelfu wakiishi katika hali ngumu za kukatisha tamaa na mazingira machafu yasiyo salama kuishi, hivyo kusababisha kitisho cha afya.
Hali hiyo pia inatoa mwanya wa kusambaa kwa kasi kwa magonjwa ya kuambukiza kama Kifua Kikuu.
Huku kukiwa na kitisho kwa utoaji wa huduma za afya mashariki mwa Ukraine kutokana na kusambaratika kwa raslimali, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na vikwazo vya ziada vya kufikia huduma za afya.
Ukraine ina mlipuko mbaya kabisa duniani wa ugonjwa wa Ukimwi na kuenea kwa ugonjwa huo kumechochewa kwa kiwango kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya kwa kutumia sindano.
Hata hivyo, tofauti na mataifa mengine ya Mashariki mwa Ulaya, nchi hiyo imekuwa ikiendesha kwa muda wa zaidi ya muongo mmoja programu kadhaa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, ambazo zimepongezwa kimataifa kwa kudhibiti kuenea kwa Ukimwi.
Programu hizi zimekuwa zikitolewa kote nchini Ukraine na ni muhimu mno katika eneo la mashariki kwa sababu idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia sindano wanatokea maeneo ya Luhansk na Donetsk yaliyopo mashariki mwa nchi hiyo.
Lakini mashirika ya kitaifa na kimataifa yanayofanya kazi za kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya yanasema upatikanaji wa huduma za kuyaokoa maisha katika maeneo hayo umekabiliwa na shinikizo tangu ulipoanza mzozo huo.
Kwamba huenda ukakatizwa kabisa katika wiki chache zijazo, huku usafirishaji wa dawa zinazotumiwa katika matibabu, methadone na buprenorphine, zikiwa zimeisha na kukwama kupelekwa eneo hilo la uwanja wa vita.
Kundi lingine la watu wanaotengwa na wanaopata shida kupata huduma za afya ni jamii ya Waroma.
Kihistoria inakadiriwa kuwapo jamii ya Waroma ya takriban watu 400,000 nchini Ukraine.
Kama ilivyo kwa Waroma wengine katika nchi za Ulaya Mashariki, inakabiliwa na ubaguzi mkubwa katika jamii, ikiwamo katika masuala ya ajira na elimu.
Inaelezwa kuna Waroma milioni 12 Ulaya na kulifanya kuwa kundi kubwa kabisa la walio wachache barani humo.
Kihistoria Waroma wanatokea India, ambako walihama miaka zaidi ya 1,500 iliyopita na kutapakaa mataifa mbalimbali ya Ulaya na Marekani.
Waroma kwa miaka mingi wamekuwa wakinyanyaswa, wakitengwa, wakifukuzwa katika nchi na hata kuwahi kulengwa na mauaji ya halaiki Ulaya.
Kwa sababu hiyo, nchini Ukraine Waroma wamekuwa hawapati huduma za matibabu kwa sababu wengi hawana vitambulisho rasmi.
Hali hiyo inaifanya jamii hiyo kushindwa kupata huduma za afya, huku ikiishi katika umaskini uliokithiri, unaomaanisha huduma na dawa zinazohitaji kulipiwa haziwezi kuwafikia.
Dk. Dorit Nitzan, Mkuu wa WHO nchini Ukraine ameliambia Shirika la Habari la IPS kuwa hata kabla ya mzozo kuanza, Waroma nchini Ukraine walikuwa wakizifikia huduma chache za matibabu ya afya na za kujikinga na magonjwa.
Matokeo yake watoto wengi wa Waroma hawajapata chanjo.
Pamoja na hayo kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza iko juu miongoni mwa Waroma, ikilinganishwa na umma kwa ujumla wake nchini Ukraine.
Zola Kondur wa shirika la haki za binadamu la Waroma lijulikanalo kama Chiricli ameliambia IPS kuwa Waroma ni miongoni mwa watu wanaokabiliwa na hatari nchini Ukraine na wanafanyiwa ubaya kwa sababu tu ya kabila lao hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles