27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Vita ya uchumi mtihani

Na EVANS MAGEGE

UAMUZI ambao serikali ya Rais Dk. John Magufuli imeufanya katika maeneo mbalimbali yanayogusa uchumi wa nchi, umeendelea kupata mjadala.

Mwelekeo wa mjadala huo ambao MTANZANIA Jumapili inaweza kuufananisha na kitanzi ambacho kutoka kwake kunategemea maamuzi ya serikali  ili kupata matunda au madhara.

Wanazuoni wameelezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ikiwamo ile ya sasa ya kununua korosho yote ya msimu huu kwa bei ya Sh. 3,300, kama ni hatua nzuri lakini inayohitaji kuchukuliwa kwa kuzingatia misingi ya uchumi.

Kabla ya hapo, serikali ilikwishafanya maamuzi katika  maeneo mengine kama ujenzi wa ukuta wa Mirerani, ununuzi wa ndege, miradi mikubwa inayoendelea ya ujenzi wa reli ya kisasa, mradi mkubwa wa umeme wa Stiegel’s  Gorge na mingine.

Akizungumzia uamuzi wa sasa wa Rais Magufuli kulitumia jeshi katika usimamizi wa kununua zao la korosho, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam(UDSM), Dk. Benson  Bana mbali na kuusifu na kufafanisha na njia alizopita muasisi wa Taifa la China Mao Zedong lakini alisema bado hajaelewa  mageuzi anayoyafanya Rais Dk. Magufuli yanasimama katika msingi wa falsafa ipi ya kiuchumi.

“Kama ilivyokuwa kwa Mao Zedong nasi tunaweza kusema tunayaona mabadiliko makubwa ambayo hatujui kama yanaongozwa na itikadi fulani au fikra sahihi za Rais,” alisema Dk. Bana

Alisema, daima nchi zote panapotokea suala la mvutano wa bei kama ilivyokuwa katika sakata la korosho,  Serikali huingilia kati kwa sababu sekta binafsi inayoongozwa na wachache haiwezi kuachiwa iendeshe uchumi.

Mtazamo huo wa Dk. Bana haukutofautiana sana na ule uliotolewa na mchumi kutoka chuo hicho, Profesa Amon Mbelle ambaye alisema  uamuzi wa Rais Dk. Magufuli  kununua korosho yote ni kiashiria kwamba anatambua umuhimu wa kilimo pia kumkwamua mkulima.

Alisema mapinduzi ya kiuchumi huzingatia pia ulinzi wa uhakika kwenye sekta ya kilimo kwa lengo kumfaidisha mkulima.

Profesa Mbelle alikwenda mbali zaidi kwa kusema suala la Serikali kulinda wakulima hufanywa na mataifa yote  ikiwamo Marekani ambapo ruzuku kubwa hutolewa kwa wakulima ili kuendeleza sekta hiyo.

“ Hapo zamani Tanzania  kulikuwa na mfumo mzuri sana wa kutoa ruzuku kubwa kwa wakulima pamoja na kulinda bei ya mazao, lakini hapo katikati mfumo wa kulinda bei ya mazao haukusimamiwa ipasavyo,” alisema Profesa Mbelle.

Aliongeza  kwa kusema bodi za mazao zina tatizo la kukosa mitazamo ya masafa marefu ya kuangalia soko la mazao pamoja na kumhakikishia mkulima bei  nzuri hata kama soko litashuka.

Kwa kujazilizia hoja hiyo alisema udhaifu mkubwa wa bodi za mazao ni kuwa na malengo ya leo na kesho na sio ya miaka mitano ijayo.

“ Mataifa mengine bodi za mazao  huwa na malengo ya miaka mitano kwa kutathimini bei iliyopo sasa na ijayo. Na katika mikakati hiyo huwa wamejipanga vilivyo kulinda bei  ya mazao pia kuwa na ziada ya kumfidia mkulima kama bei itakuwa imeshuka kwenye soko la dunia,” alisema Profesa Mbelle.

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Azaveli Lwaitama alisema uamuzi wa Rais Dk.  Magufuli wa kuingilia kati sakata la bei ya korosho ni mzuri ingawa hautoshi kufananishwa na kiashiria cha mapinduzi ya kiuchumi kama yale aliyofanya Mao.

Pia Dk. Lwaitama alionyesha wasiwasi wake juu ya uamuzi huo wa Serikali kununua korosho yote, kwamba itakuwaje kwa mazao mengine kama ikitokea wakulima watagomea bei elekezi za kuuza mazao yao.

“ Ikitokea wakulima wa mahindi, pamba, kahawa, ufuta, mbaazi nao hawataki kuuza bei ya kulaliwa na mabwanyenye, je Serikali itatumia utaratibu huu huu  wa kununua korosho, kununua na mazao mengine ili kumsaidia mkulima?.

“ Rais kafanya kazi nzuri lakini tatizo chama chake kinamabwanyeye wengi ambao wamesababisha hata bodi za mazao kuoza. Najua anajaribu kujiweka kando ya mabwanyeye kwa kutumia dola kwa maana ya jeshi, sasa tujiulize kwa mazao mengine  jeshi litapewa jukumu hili kama la kwenye korosho,” alihoji Dk. Lwaitama.

Aliongeza kuwa tatizo nchi ipo kwenye mtanziko mkubwa wa mabwanyeye waliovaa vazi la “ubepari wa manunuzi ya soko”.

Kwamba Rais anatakiwa kurekebisha mfumo huo na kuweka mfumo mpya angalau wapatikane mabwanyenye wazalendo watakaofanya biashara yenye kuwapa unafuu wakulima.

“Katika mtanzuko huu, wakulima waligomea bei iliyotolewa na bodi, wafanyabiashara nao wakagomea bei aliyoagiza Rais, najua uamuzi wake wa kutumia jeshi ni mzuri kusimamia usafirishaji wa korosho na malipo kwa wakulima lakini kama angetumia bodi kulipa wakulima si ajabu wangetokea matajiri wachache wakazikwapua na kujilimbikizia,” alisema Dk. Lwaitama.

HISTORIA/UGUMU WA KOROSHO

Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanasema historia inaonyesha kuwa bei ya zao la korosho imekuwa ni suala gumu si tu kwa serikali kusimamia bali hata haki ya kumnufaisha mkulima.

Wafuatiliaji wa mambo wanadai kuwa tangu utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, bei ya korosho imekuwa  katika misingi ya kumnyonya mkulima kwa sababu zao hilo halikupewa kipaumbele cha mazao makubwa ya kibiashara kwa uchumi wa nchi.

Inaelezwa kwamba mwenendo huo si tu ulikuwapo ndani ya utawala wa kwanza bali mazingira ya zao hilo kutopewa kipaumbele katika uchumi yalikuwapo tangu enzi ya ukoloni.

Kwamba mazao yaliyopewa kipaumbele wakati huo ni mkonge, kahawa, pareto, karafuu na karanga.

Kwa msingi huo wadadisi wa mambo wanaona kuwa biashara ya zao korosho kwa sasa imeshika nafasi ya kahawa angali zao hilo kama yalivyo mazao mengine kwa sasa nchini ambapo biashara zake zimejikuta zinaathiriwa na mambo matatu ambayo ni siasa, utawala na uchumi.

SIASA

Kwa upande wa siasa inaelezwa kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa vibaraka wa wafanyabiashara  katika kuhujumu bei ya zao la korosho pamoja na mazao mengine kwa nia ya kumnyonya mkulima.

Mtazamo huo unabebwa kwa hoja ya kwamba baadhi ya wanasiasa wameingia kwenye biashara ya mazao au wanatumiwa kama vipaza sauti za kuuaminisha umma juu ya kuporomoka kwa soko la zao kimataifa ajenda ambayo moja kwa moja hutumiwa na wanunuzi wa mazao kununua mazao kwa bei ya chini na yenye kumkandamiza mkulima.

UTAWALA

Upo mtazamo mwingine kuwa utawala umekuwa ni sehemu inayochangia kwa kiasi kikubwa kukandamizwa kwa nguvu ya mkulima katika bei ya mazao.

Wadadisi wa mambo wanaijenga hoja hiyo kwa kuangalia nafasi ya utawala katika uteuzi wa bodi za mazao mbalimbali nchini.

Kwamba tofauti na bodi za mazao zilizokuwapo enzi ya mkoloni au wakati wa utawala wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambazo ufanisi ulikuwa bora na kuvifanya vyama vya ushirika kuwa imara.

Inaelezwa kuwa bodi za mazao zinazoteuliwa kwa sasa si tu kwamba zimejengwa katika misingi ya kisiasa kwa maana ya wajumbe au Mwenyekiti kuwa na vinasaba vya siasa za chama tawala bali hata wajumbe wa bodi hizo wengi wanatazamwa kama wadau wa wanasiasa, washirika wa wafanyabiashara au ni wafanyabiashara wa mazao.

Matokeo ya mtindo huo yamekuwa ni uchochoro wa bodi kutumiwa na watu wenye masilahi binafsi au kuweka maazimio yenye mitazamo dhaifu ya kitaalamu hivyo kujikuta zinatoa bei elekezi ya kuuza mazao kwa nia ya kumnufaisha mfanyabiashara.

Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanapendekeza kuwa aidha wajumbe wa bodi za mazao wawe wanaomba kazi  na kufanyiwa usahili kama ilivyo kwa kazi nyingine kwamba utawala uteue mwenyeiti tu au nafasi ya mwenyekiti wa bodi iwe inaombwa kama kazi nyingine.

UCHUMI

Kwa upande wa baadhi ya wadadisi wanatazama kwamba, hadaa za wafanyabiashara wa mazao kwa wakulima ndizo zimekuwa zikisababisha aidha serikali kupoteza fedha au wakulima kuuza mazao kwa bei kandamizi.

Inaelezwa kuwa hadaa hizo zimegawanyika katika nyanja mbalimbali ikiwamo mizani ya kupimia mazao kuchezewa, kujaza magunia kupita kiasi pamoja ajenda za kuyumbisha soko la mazao ili wanunue kwa bei ya chini.

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles