New York, Marekani
MAREKANI imesema itazipiga marufuku kampuni 28 za China kununua bidhaa nchini humo kwa madai kuwa zinakiuka haki za binadamu na kuwanyanyasa watu wa kabila la Uighur na Waislamu wa jamii nyingine za wachache Jimbo la Xinjiang.
Hata hivyo, Marekani imekanusha kuwa hatua hiyo inahusiana na mazungumzo ya biashara yaliyopangwa kuanza tena wiki ijayo.
Si mara ya kwanza Marekani kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya mashirika ya China.
Mei mwaka huu utawala wa Rais Donald Trump uliiweka kampuni kubwa ya teknolojia ya Huawei katika orodha hiyo kutokana na hofu ya kiusalama kuhusu bidhaa zake.
Katika vikwazo vipya, Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross, ameitangaza hatua hiyo akisema nchi yake haiwezi kuvumilia ukandamizaji na vitendo vya kikatili dhidi ya jamii ya walio wachache nchini China.
Ross alisema marufuku hiyo itazizuia kampuni hizo kununua bidhaa za Marekani hadi kupata kibali maalumu kutoka Washington.
Miongoni mwa mashirika 28 yaliyoorodheshwa ni pamoja na ofisi 18 za usalama zilizoko Xinjiang, chuo kimoja cha polisi na kampuni nane za kibiashara, ikiwemo ya bidhaa za kiteknolojia ya Hikvision na kampuni zinazoshughulika na vifaa vya ujasusi na kutambua sura ya mtu za Megvii na Sense Time.
Marufuku hiyo imetangazwa huku kukiwa na mvutano kati ya Marekani na China, hasa kuhusu sera ya biashara na vitendo vinavyofanywa na China katika Jimbo la Xinjiang.
Nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa duniani, ziko katika vita ya kibiashara, huku zikiwekeana ushuru wa mabilioni ya dola katika bidhaa zao.
Jana, Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa mazungumzo kati ya nchi hizo yamepangwa kuanza tena Alhamisi, huku mjumbe wa ngazi ya juu wa China katika masuala ya biashara, Liu He akitarajiwa kukutana na mwakilishi wa kibiashara wa Marekani, Robert Lighthizer na Waziri wa Fedha, Steven Mnuchin.
Wakati huo huo, Marekani imechukua hatua zaidi dhidi ya China kutokana na sera zake kuelekea Jimbo la Xinjiang.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema China inawashikilia karibu Waighur milioni moja na Waislamu wengine katika kambi za ndani, ambako wanafundishwa propaganda za kikomunisti na kulazimishwa kuukana utamaduni na dini yao, kitendo ambacho Marekani inasema ni sawa na enzi za utawala wa wanazi nchini Ujerumani.
Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja mwezi uliopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliandaa mkutano kuelezea madhila wanayopitia Waighur, huku Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Sullivan akilaani kampeni ya ukandamizaji ya China ambayo ni ya kutisha.
Sullivan alisema Serikali ya China inawazuia Waislamu kusali na kusoma Quran na imeivunja au kuiharibu misikiti kadhaa.
Alisema huo ni mfumo unaotumiwa na chama cha kikomunisti cha China kuwazuia raia wake kutekeleza haki yao ya uhuru wa kidini.
Hata hivyo, hadi hivi karibuni China imeyakanusha madai ya kuwepo kwa kambi hizo, lakini sasa imesema kuna shule za mafunzo ya ufundi, ambazo ni muhimu katika kudhibiti ugaidi, huku ikilalamikia kitendo cha kuingiliwa kwa masuala yake ya ndani.
Uighurs ni kina nani?
Watu wa kabila la Uighurs ni Waislamu Waturuki. Ni asilimia 45 ya watu wanaoishi Xinjiang, asilimia 40 ni watu wa kabila la Han Chinese.
China ilichukua udhibiti wa eneo hilo mwaka 1949 baada ya kuliangamiza jimbo la mashariki mwa Turkestan.
Tangu wakati huo, kumekuwa na uhamiaji mkubwa wa watu wa kabila la Han Chinese na Uighurs wanahofia mmomonyoko wa utamaduni wao.
Xinjiang ni jimbo huru ndani ya China, kama Tibet lililopo kusini mwake.