28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Vita Uingereza kujitoa EU  

cameroonNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

MATOKEO ya kura ya maoni iliyopigwa juzi nchini Uingereza ambayo yameonyesha kuwa Waingereza wengi wameamua kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (EU), yameleta mshtuko mkubwa duniani.

Uamuzi huo ambao umetajwa kuwa ni wa kihistoria, tayari umeibua vita ya maneno kati ya vijana na wazee, huku Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, akishindwa kujizuia kushuhudia matokeo ambayo hakuyatarajia na hivyo kutangaza kujiuzulu nafasi yake saa chache baada ya matokeo ya kura hiyo kutangazwa jana.

Wanataaluma mbalimbali duniani hususani wale wa biashara na uchumi wengi wao wameonekana kukumbwa na mshtuko kutokana na uamuzi huo ambao wanasema kama utaridhiwa na Bunge la nchi hiyo utaathiri hali ya uchumi katika nchi mbalimbali duniani ambako EU ilikuwa ikiendesha au kufadhili miradi yake.

Nchi nyingi ikiwemo Tanzania imetajwa itaathirika na uamuzi huo wa Uingereza kujitoa EU kwa namna mbalimbali ikiwemo kudorora kwa masoko ya fedha na mitaji.

MTANZANIA Jumamosi limezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa, ambaye amesema uamuzi huo wa Uingereza utaathiri masoko ya fedha na mitaji.

Alizitaja athari za muda mfupi kuwa ni kupungua kwa shughuli za kiuwekezaji katika masoko kutoka kwa wawekezaji wa Uingereza.

“Lakini baadaye hali inaweza kubadilika baada ya haya mabadiliko kuzoeleka na wawekezaji kutafuta mbinu mbadala za uwekezaji,” alisema Marwa.

Naye Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alisema uamuzi huo wa Uingereza unaweza kukwamisha baadhi ya miradi ambayo ilikuwa inafadhiliwa na EU kutokana na kukosa fedha ambazo zilikuwa zinachangiwa na nchi hiyo.

“Hapa katika kipindi hiki cha mabadiliko, EU inaweza kushindwa kutoa fedha za miradi iliyokuwa inafadhili kwasababu kujitoa kwa Uingereza kunapoteza pauni milioni 3 zilizokuwa zinachangiwa kwa wiki na nchi hiyo,” alisema Silinde.

Alisema hali itarudi pale Uingereza itakapoanzisha misaada yake yenyewe nje ya EU.

Waingereza wapatao 17,410,742 sawa na asilimia 51.89 ya waliopiga kura ya maoni wametaka Uingereza ijitoe EU huku  16,141,241 sawa na asilimia 48.11 wametaka ibaki.

Katika hotuba yake ya kutangaza kujiuzulu jana, Cameron alisema Waingereza wamechagua njia mpya na kwamba kutokana na uamuzi huo nchi hiyo inahitaji uongozi mpya wa kuongoza katika mwelekeo huo.

“Nimepigana sana katika kampeni kwa kuweka wazi  kile nilichoamini kutoka moyoni mwangu…nilisema kabisa imani yangu ni kwamba Uingereza ipo imara na salama ndani ya EU,” alisema na kuongeza:

“Watu wa Uingereza wamefanya uamuzi wa kuchagua njia mbadala ambayo nafikiri nchi inahitaji uongozi mpya wa kuongoza katika mwelekeo huo.”

Kutokana na hali hiyo, Cameron alisema atajitahidi kuongoza kwa miezi kadhaa na kwamba angependa kumwachia Waziri Mkuu mpya ifikapo Oktoba mwaka huu.

“Nitafanya kila linalowezekana kama waziri mkuu kuendelea kuongoza kwa wiki na miezi kadhaa lakini sidhani kama itakuwa sawa kwangu kuendelea kuongoza nchi.”

Cameron alisema amefanya uamuzi mgumu kwa masilahi ya Taifa ili liweze kuwa na muda wa kujiimarisha na kuwa na viongozi wapya wanaohitajika.

 

SOKO LA HISA LAPOROMOKA

Taarifa zilieleza kwamba dakika 10 baada ya matokeo ya kura ya maoni mauzo katika soko la hisa la FTSE 100 ambalo ni kampuni tanzu ya Soko la Hisa la London, yaliporomoka kwa alama mia tano sawa na asilimia 9 na kuweka rekodi mpya kwa miaka 30.

Mchumi Alan Clarke wa Scotiabank alinukuliwa katika mtandao wa Mirror wa Uingereza  akisema hali hiyo itaathiri zaidi mifuko ya pensheni ambayo imewekeza sana katika hisa na ambayo wafanyakazi wengi wanaitegemea.

Alisema hali hiyo pia itaathiri wawekezaji wadogo ambao wanamiliki hisa na kwamba inaweza kuwa na athari katika masoko mengine ya hisa duniani.

GAVANA WA UINGEREZA

Gavana wa Benki ya Uingereza, Mark Carney, alisema kunaweza kutokea mtikisiko wa soko na uchumi na kuongeza kwamba benki tayari imejiandaa.

“Itachukua muda kwa Uingereza kuanzisha uhusiano mpya na Ulaya na sehemu nyingine za dunia hivyo hali ya mtikisiko kwenye masoko na uchumi inaweza kujitokeza lakini tumejipanga kwa hili,” alisema Carney.

Gavana wa benki kuu ya Kenya ameungana na gavana wa benki kuu ya Uingereza na mataifa mengine kujiandaa kwa mdororo wa sarafu za mataifa yao kutokana na uamuzi wa Uingereza.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, nchini Afrika Kusini, soko la hisa la Johannesburg limeporomoka kwa asilimia 4%, huku kukiwa na shauku kutoka kwa wadadisi kuwa huo ndio mwanzo tu wa msukosuko katika uchumi wa ulimwengu kuhusiana na kura hiyo ya kujiondoa ya Uingereza.

UINGEREZA KUGAWANYIKA

Matokeo hayo pia yameonekana kuwa na athari nchini Uingereza ambapo tayari umeonekana mgawanyiko mkubwa kati ya wale wanaounga mkono na wasiounga mkono kujiondoa EU.

Wakati Uskotishi, London na Ireland Kaskazini wakionekana kupinga kujiondoa, wenzao wa England na Wales wameonekana kuunga mkono kujitoa.

Mgawanyiko huo umechagizwa na kauli za viongozi wa sehemu zinazounda Uingereza.

Waziri wa kwanza wa Uskotishi na kiongozi wa chama cha Scottish National Party (SNP), Nicola Sturgeon, alisema kama Uingereza itajitoa EU basi ataongoza awamu ya pili ya kura ya maoni ya Uskotishi kujitenga.

Nayo Serikali ya Ireland ilitangaza kukutana na baadaye kutoa tamko juu ya uamuzi huo wa Uingereza na kusema kwamba utakuwa na athari kwao na kwa Ulaya nzima.

Pamoja na mgawanyiko huo wa ukanda upo pia mgawanyiko wa makundi ya umri ambapo wakati vijana wengi wakipiga kura ya kukataa kujitenga, wazee wengi walipiga kura za kujitenga kitendo ambacho kimewafanya vijana wengi nchini humo kulalamikia kuamuliwa maisha yao ya baadaye na wazee ambao hawatakuwepo.

TRUMP AKUNWA

Mgombea anayewania urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump, amefurahishwa na uamuzi wa Waingereza na kusema kuwa wameirudisha nchi yao.

Trump amekuwa kwenye uhusiano mbaya na Cameron tangu alipoanza harakati za kuwania nafasi ya kugombea urais nchini Marekani na wakati fulani alikaririwa akisema hatakuwa na uhusiano mzuri na Cameron ikiwa atakuwa rais wa Marekani.

Mwezi Desemba mwaka jana, Cameron alimtaja Trump kama mbaguzi, mjinga na mwenye makosa kutokana na kauli yake kwamba ataweka marufuku ya muda ya Waislamu kuingia Marekani.

BLAIR ASIKITISHWA

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza kupitia chama cha Conservative, Tony Blair, alisikitishwa na uamuzi wa kujiondoa EU na kusema kuwa umefanywa kipinzani badala ya kuchagua.

Aidha, aliweka wazi kuwa uamuzi wa kujitoa EU si suluhu ya malalamiko yaliyotolewa dhidi ya umoja huo na watu waliounga mkono kujiondoa kwani ni mambo ambayo yapo duniani kote.

BORIS KUCHUKUA NAFASI YA CAMERON?

Mwandishi wa habari ambaye kwa sasa amezamia kwenye siasa na mfuasi wa chama cha Conservative, Boris Johnson, anatajwa kuwa huenda akachukua nafasi ya Cameron kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono Uingereza kujiondoa EU.

Boris na wenzake, Michael Gove na Gisela Stuart  kwa pamoja waliitisha mkutano na waandishi wa habari muda mfupi baada ya Cameron kujiuzulu na kusema kuwa wamefurahia ushindi huo ingawa hakuna aliyeweka wazi kama anataka kurithi mikoba ya Cameron.

CHAMA CHA LABOUR

Kwa upande wa chama cha Labour hali inaonekana si nzuri baada ya viongozi wakubwa wa chama kuripotiwa kujiandaa kupiga kura ya kutokuwa na imani na kiongozi wao, Jeremy Corbyn ambaye analalamikiwa kutotoa mchango wa kutosha kwenye zoezi la upigaji kura ya maoni.

Hoja hiyo ya kumwondoa Corbyn inatarajiwa kupigiwa kura mapema Jumanne na kwamba utakuwa mtihani wa kwanza katika uongozi wake.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC, Laura Kuenssberg, hoja hiyo tayari imewasilishwa kwa Mwenyekiti wa Bunge wa chama cha Labour.

Baraza kivuli lilifanya mazungumzo kuhusu suala hilo ambapo Mbunge wa Labour, Angela Smith, alikuwa wa kwanza kusema kuwa Corbyn anatakiwa kuondolewa.

Pamoja na kura hiyo ya maoni kuonyesha kuwa watu wengi wanataka kujitoa lakini bado Bunge la nchini humo linaweza kukwamisha suala hilo japo duru za siasa zinasema huo utakuwa ni ukatili wa kisiasa kwa sababu litakuwa linapinga maoni ya wananchi.

Kwa mujibu wa sheria za EU mwanachama anayetaka kujitoa itamchukua miaka miwili kufanya mazungumzo tangu siku atoe taarifa rasmi ya kujiondoa.

Uingereza ni miongoni mwa nchi 10 zinazochangia kiasi kikubwa katika Umoja wa Ulaya. Kwa mujibu wa taarifa ya fedha ya EU ya mwaka 2014/15 Uingereza ilichangia Euro bilioni 8.8 ikiwa ni karibia ya mara mbili ya kiasi ilichochangia mwaka 2009/10.

Suala hilo pamoja na mambo mengine ikiwemo watu wengi wa Ulaya kuhamia Uingereza na kuchukua ajira ndiyo imesababisha walio wengi kupiga kura ya kujitoa.

TAMKO LA EU

Kutokana na uamuzi huo wa Uingereza, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, amesema mataifa 27 yaliyobakia yanaweza kuendeleza umoja.

Tusk alinukuliwa jana na shirika la habari la Reuters akisema EU imekuwa ikijiandaa kwa tukio hilo.

“Kitu ambacho hakiwezi kukuua huwa kinakufanya uwe imara,” Tusk alisema na kuongeza: “Nataka kumwakikishia kila mmoja kuwa tumejiandaa kwa hali hii.”

Viongozi wa EU akiwemo Cameron watakutana Jumanne huko Brussels. Tusk amesema viongozi 27 wa nchi zilizobaki watakutana kwa dharura kujadili namna ya kushughulika na uamuzi wa Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles