33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi watakiwa kutoingilia taratibu za leseni za madini

Na Derick Milton, Simiyu

Ofisi ya Madini Mkoa wa Simiyu imewataka Viongozi wenye Mamlaka kuacha kutumia mamlaka yao kuingilia taratibu za utolewaji wa leseni za uchimbaji wa madini ambazo hufanywa na tume ya madini kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Rai hiyo imetolewa leo Februari 16, na Kaimu Ofisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Joseph Kumbulu, wakati wa kikao cha wadau wa madini mkoani humo na kushirikisha kamati za ulinzi na usalama wilaya zote tano, Wakurugenzi pamoja na wakuu wa Wilaya.

Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Joseph Kumbulu, akizungumza wakati wa mkuatano na wadau wa Madini mkoani humo.

Mhandisi Kulumbu amesema kuwa kumekuwa na viongozi ambao wamekuwa wakiingilia taratibu za utolewaji wa leseni kwenye migodi ya uchimbaji madini, ikiwemo kufuta, kusimamisha uchimbaji au kuzuia leseni zilizotolewa na tume.

Kulumbu amesema kitendo hicho ambacho kimekuwa kikifanywa na viongozi wenye mamlaka ni kosa kisheria kwani hawana mamlaka ya kuchukua hatua hizo lakini pia kimekuwa kikiingizia serikali hasara.

“Kwenye maeneo mengine viongozi ambao wameingilia utolewaji wa leseni kwa kutumia mamlaka yao, serikali imeshtakiwa na wenye leseni kwani hatua zilizochukuliwa hazijafuata sheria na kanuni,” amesema Mhandisi Kulumbu.

Mtendaji huyo amesema kuwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Ofisa Madini Mkoa au tume ya madini kwani ndiyo wamepewa mamlaka ya kufanya hivyo kisheria na siyo kiongozi mwingine yeyote.

“Kwa sasa kiongozi yeyote akifanya hivyo na mwenye leseni akitaka kuishtaki serikali, tunamwambia mshitaki mtu mwenyewe na siyo serikali, tunawaomba viongozi tuwatumie maafisa madini ndiyo wenye mamlaka,” amesema Mhandisi Kulumbu.

Akiongelea suala hilo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga, amesema kuwa hatua za viongozi kuingilia taratibu hizo inatokana na njia zinazofanywa na watendaji wa tume ya madini kutoa leseni kuwa na udanganyifu mwingi.

Kiswaga amesema leseni nyingi zinazotolewa zimekuwa hazifuati taratibu na sheria, hali ambayo imesababisha migogoro mingi huku leseni hizo zikiwajali watu wenye pesa na kuwaacha wanyonge hasa wamiliki wa mashamba wakiangaika.

“ Bariadi tuna uchimbaji wa madini ya dhahabu, lakini tume mmetoa leseni bila ya kufuata sheria ndiyo maana tumeingilia kwa kusimamisha au kuzuia, haziwajali wanyonge hasa wenye mashamba, mnatoa leseni zinazosababisha migogoro,” amesema Kiswaga….

“Leseni nyingine zinatolewa baada ya wananchi kugundua na tena zinatolewa haraka haraka bila ya kuwashirikisha wahusika hasa wenye mashamba au viongozi wa eneo husika, mimi kama Mkuu wa Wilaya siwezi kuruhusu wananchi wangu wanyonywe na hao wenye pesa zao,” amesema Kiswaga.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kama kiongozi wa Wilaya hiyo hataruhusu uwekezaji wowote wa madini usifuata sheria na taratibu za upatikanaji wa leseni ya uendeshaji wa shughuli za madini ndani ya wilaya yake ambao unakwenda kukandamiza maslahi ya wamiliki wa maeneo ya uchimbaji.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, akizungumza wakati wa mkuatano huo.

Kiswaga amesema ataendelea kuingilia taratibu hizo ikiwa atabaini leseni ambazo zinatolewa hazijafuata sheria na wala hataogopa kushitakiwa kama yeye kwa kuchukua uhamuzi ambao unalenga kuwagusa wanyonge.

Akifungua mkutano huo Katibu Tawala wa Mkoa, Miriam Mmbaga amewataka wachimbaji wenye leseni kutowakandamiza wamiliki wa mashamba pamoja na kutowanunua kwa manufaa yao binafsi na badala yake waangalie faida yao wenyewe na sio vinginevyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles