25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa vijiji wanaouza ardhi siku zao zahesabika

Amina Omari -Kilindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameonya viongozi wa vijiji wanaouza ardhi na kusababisha migogoro, huku akiwataka viongozi wa Serikali kukaa ofisini siku mbili, nyingine waende kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yao.

Majaliwa alitoa onyo hilo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara eneo la Bokwa, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Alisema Serikali haitasita kumchukulia hatua kiongozi wa kijiji atakayehusuka na kuuza ardhi kinyume cha utaratibu na kusababisha migogoro.

“Ole wenu wenyeviti wa vijiji mnaofanya biashara ya ardhi, taratibu za umiliki wa ardhi mnazijua, lakini nyie mnapindisha, badala ya kuwashirikisha wananchi, mnawafanyia maamuzi kwa niaba,” alisema Majaliwa.

Aidha kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuumaliza.

“Nashangaa mnagombania mipaka, Tanzania ni nchi huru, kila mtu anastahili kulima na kuishi popote, bora tu afuate taratibu, haya mambo ya mipaka tuachieni Serikali,” alisema Majaliwa.

CHANGAMOTO YA KILINDI

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, alisema changamoto ya Wilaya ya Kilindi ni kutokuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

“Tunatarajia kuanza kuweka mpango wa matumizi ya ardhi katika vijiji vitano vitakavyopitiwa na mradi wa bomba la mafuta, ni matumaini yangu kwa hapo tutakuwa tumeweza kumaliza migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa,” alisema Mabula.

Mbunge wa Kilindi, Omari Kigua, aliiomba Serikali kumtatulia changamoto ya barabara ili kusaidia kuinua uchumi wa wilaya hiyo.

WATENDAJI KUKAA OFISINI

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema watendaji wa Serikali kutotenga muda wa kusikiliza na kutatua kero, ndio kumesababisha wananchi kuvamia misafara ya viongozi.

Akihutubia wananchi wa Kibirashi wilayani Kilindi, Majaliwa alisema alichogundua ni watendaji kutowajibika ipasavyo katika kushughulikia kero za wananchi kwani badala ya kuwafuata ili kusikiliza kero zinazowakabili, wao wanasubiri wafuatwe ofisini.

“Mtumishi wa umma siku zako za kukaa ofisini ni mbili tu, siku nyingine zote nenda kwa wananchi kasikilize wana kero gani, zitafutie ufumbuzi, sio mpaka wasubiri misafara ya viongozi na kuivamia,” alisema Majaliwa.

MIMBA KWA WANAFUNZI

Aidha katika hatua nyingine, Majaliwa alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua wanaume wanaohusika na kuwapa mimba mabinti na kukatiza masomo yao.

Alisema Serikali inatengeneza mfumo madhubuti kwa mtoto wa kike kupata elimu, lakini wapo wanaume wenye nia ovu wanachangia kuharibu malengo hayo.

“Serikali inajitahidi kuweka mazingira mazuri kwa watoto wa kike wasome, halafu kuna wengine wanawaharibia ndoto zao.

“Niwaagize mahakimu, utakapokutana na kesi ya binti amepewa mimba na ushahidi unao, wewe mfunge tu miaka 30 ili akitoka awe ameshazeeka,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles