30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Bashe apigilia msumari wa mwisho wakulima pamba kulipwa kwa akaunti

Derick Milton – Simiyu

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe, amesema suala la wakulima wa pamba kupata malipo yao kwa njia ya akaunti katika msimu wa mwaka huu wa zao hilo halina mjadala.

Bashe amesema kinachotakiwa ni wakulima wenyewe kufungua akaunti kwenye benki mbalimbali.

Amesema kuwa tayari Serikali imeziagiza benki kuhakikisha kila mkulima anapata namba ya akaunti, na kuhakikisha wanazingatia makubaliano yote ambayo waliwekeana.

Bashe alisema hayo jana wakati akizindua mpango mkakati wa mapinduzi ya kilimo cha pamba katika Mkoa wa Simiyu kwa miaka mitano, ambao unatekelezwa na taasisi inayoshughulikia masuala la pamba na nguo ya  GATSBY Africa.

Aliwataka wakulima wote ambao wanazalisha pamba nchini, kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi pindi benki mbalimbali zitakapopita kwenye maeneo yao kuwafungulia akaunti.

Alisema kuwa Serikali tayari imekubaliana na benki hizo, hasa NMB na CRDB zenye mtandao mkubwa nchini, kuwa akaunti zote za wakulima wa zao hilo hazitakuwa na makato na watafunguliwa bure.

“Tumekubaliana na benki kuwa akaunti za wakulima wetu hazitakuwa na makato kama yale ya kila mwezi, na mkulima akitoa pesa zake makato yasiwe makubwa, yawe tofauti na wengine, lakini wakulima watafunguliwa bure,” alisema Bashe.

Alizitaka benki hizo kuhakikisha zinazingatia makubaliano hayo na kuhakikisha wakulima wote wa zao hilo wanafunguliwa akaunti bure na kwa haraka kabla ya muda wa uuzaji wa zao hilo haujafika.

Alisema kuwa lengo la Serikali kufikia uamuzi wa wakulima kulipwa kwa njia ya akaunti, ni kutaka kubadilisha sekta ya kilimo kutoka kuwa huduma hadi kuwa biashara.

“Tunataka kumjengea heshima mkulima, leo machinga wanaheshimika, lakini mkulima hapana, machinga anakopesheka na benki, lakini mkulima hawezi kukopesheka, kwa mkakati huu lazima mkulima akopesheke na turejeshe heshima kwake,” alisema Bashe.

Aidha aliagiza Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha viongozi wa vyama hivyo wanapatiwa mafunzo ya jinsi gani ya kuandaa taarifa za fedha.

Awali akiongelea lengo la mkakati huo, Mkurugenzi wa Gastby anayesimamia mazao ya pamba na nguo, Samwel Kilua, alisema kuwa mkakati huo unalenga kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kuwa utafiti unaonyesha kuwa wakulima wengi wamekuwa wakizalisha kilo 100 hadi 200 kwenye hekari moja, tofauti na inavyotakiwa kwani wakilima kwa tija wanaweza kuzalisha kilo 1,000.

Alieleza kuwa mkakati huo umelenga kuboresha kwenye maeneo ya ugani, kuwaelimisha wakulima namna bora ya kunyunyuzia dawa na kuwafikia wakulima wote katika mkoa huo.

Kilua alieleza kuwa katika mkakati huo wanashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, wanunuzi wa pamba, vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, ambapo kwa hatua za awali vimefikiwa vyama vya msingi vya ushirika 26 mkoa mzima.

Alisema kuwa kupitia mkakati huo wakulima watafundishwa zaidi katika kuongeza uzalishaji kwenye zao hilo, kwa kulima kisasa ikiwa pamoja na kufundishwa namna bora ya kunyunyuzia dawa za viuatilifu vya zao hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo, Antony Mtaka alisema kuwa mkakati huo utaweza kusaidia mkoa wa Simiyu kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 160 hadi kufikia milioni 400.

Mtaka alisema kuwa bado changamoto kubwa imebaki kwa wakulima wenyewe jinsi gani ya kuongeza uzalishaji, kwenye zao hilo ambapo mkakati huo utawezesha kuwainua kiuchumi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles