SEOUL, KOREA KUSINI
VIONGOZI wa Korea mbili wamekutana mjini, Korea Kaskazini jana kwa mkutano wao wa kuondoa silaha za nuklia kwenye rasi ya Korea.
Aidha walijadiliana masuala mengine, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa kiini cha mzozo baina yao.
Rais Moon Jae-in wa Korea kusini aliwasili Pyongyang kwa mkutano huo wa tatu kwa mwaka huu na Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong un.
Kabla ya kuanza kwa mkutano wao huo wa kilele Rais wa Korea Kusini, Moon jae in na wa Kaskazini, Kim Jong un walitumia gari la pamoja kukatisha katikati ya mji mkuu, Pyongyang ambako maelfu ya raia walijipanga barabarani wakiwashangalia wakisema ‘Muungano wa taifa’ na kupeperusha bendera za Korea zote mbili, wakiashiria haja ya kuungana tena korea hizo mbili.
Hata hivyo, nchini Korea Kusini mkutano huo umekumbwa na maadamano ya wananchi kupinga ushirikiano wa karibu na Korea Kaskazini.
Moon ambaye aliwasili Pyongyang jana akilakiwa kwa gwaride la kijeshi na heshima huku zulia jekundu limetandikwa mbele ya mwenyeji wake. Kim Jong Un, ambaye uwepo wake uwanja wa ndege umetajwa na vyombo vya habari kuwa jambo la kushangaza.
Viongozi hao waliambatana na wake zao walikumbatiana kwa furaha katika tukio ambalo lilirushwa moja kwa moja katika televisheni nchini Korea Kaskazini na Kusini.
Moon, ambaye alifanya juhudi za kuwa mpatanishi katika mazungumzo kuhusu silaha za nyuklia kati ya Marekani na na Pyongyang alisema kuwa atatafuta suluhu ya kudumu wakati wa mkutano huo wa siku tatu.