MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema viongozi wa madhehebu ya dini na waganga wa tiba asili ni nguzo muhimu katika kutokomeza Kifua Kikuu(TB) nchini.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza Kifua Kikuu (TB) nchini, uliofanyika Dar es Salaam.
Waziri Ummy alisema waganga wa jadi na viongozi wa dini ni wadau muhimu katika mapambano dhidi ya TB.
Alisema utafiti uliofanywa 2018 na Mpango wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma unaonyesha waganga wa jadi wamekuwa waathirika wakubwa wa ugonjwa wa kifua kikuu.
Alisema viongozi wa dini ni kundi jingine muhimu katika mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini kutokana na idadi kubwa ya waumini wanaowaamini katika kufikisha ujumbe.
“Waganga wa jadi ni wadau muhimu katika mapambano ya kifua kikuu, utafiti wa 2018 uliofanywa na mpango wa taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma unaonyesha waganga wa jadi na wenyewe wamekuwa waathirika wa kifua kikuu.
“… na viongozi wa dini tunawahitaji wanaposimama katika makanisa na katika misikiti yetu ili wawe wanawakumbusha waumini juu ya Kifua Kikuu,” alisema Waziri Ummy.
Alisema mwaka 2017 Tanzania iligundua na kuwapatia matibabu takribani wagonjwa 75,000 ikiwa ni asilimia 44 tu ya wagonjwa wanaokadiriwa kuugua TB.
Alisema hiyo ina maana ya kuwa wagojwa 85,000 zaidi ya asimilia 50 hawagunduliwi na hivyo kukosa matibabu kila mwaka nchini.
Pia Waziri Ummy alisema TB huathiri takriban watu milioni 10.4 duniani kila mwaka na asilimia 25 ya wagonjwa wanatoka barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 barani Afrika zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa TB na inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa TB 154,000 kila mwaka.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi, hali iliyoleta mafanikio ikiwamo kuvuka malengo ya mwaka 2018 ambako walifikiwa wagonjwa 75,845 ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammad Kambi, alisema Tanzania ina wastani wa wagonjwa 154,000 ambao wanatakiwa kuibuliwa na kuanzishiwa matibabu.