*Wasema wasilenge dini kama ngazi yakufanikisha malengo yao
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Viongozi wa Dini ya Kiislamu wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam wamekerwa na kauli zilizotolewa na Mbunge wazamani wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Godbless Lema wakati wa mkutano wa chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Buriaga, Temeke Julai 23, mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jumatano Julai 26, 2023 jijini Dar es Salaam, Sheikh wa Wilaya ya Temeke ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani wilayani humo, Zailai Hassan, amesema kauli ya lema ya kushambulia viongozi wa dini katika jukwaa la mikutano ya kisiasa siyo yakuungwa mkono.
Amesema haiwezekani viongozi wa dini wakadhalilishwa majukwaani nan kwamba jambo hilo halikubaliki na wanalipinga vikali.
“Jambo hili limetukera na kutuhuzunisha sana, haiwezekani viongozi wa dini wakadhalilishwa katika majukwaa ya siasa, alipaswa kuzungumza siasa lakini siyo kuchanganya dini na siasa, jambo hili limetukwaza sana. Lema anapaswa kujikita kwenye siasa na siyo kutuhusisha sisi,” amesema Sheikh Hassan.
Katika hatua nyingine Sheikh Hassan amemsifu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa anmna ambavyo ameendeleza kudumisha amani na utulivu na kwamba anapaswa kuendelea kusimama imara pamoja na kauli zisizo na staha ambazo zimekuwa zikitolewa na badhi ya wanasiasa.
“Tunaendelea kumuombea mama yetu Rais Samia azidi kuwa na huruma kwa sisi watoto wake, kwani sisi tunaweza kusungumza maneno ya kumkwaza lakini atusamehe sisi ili nchi yetu iendelee kuwa na amani,” amesema Sheikh Hassan.
Upande wake Mwenyekiti wa Shamsu L Maarifa Kheri, Khalifa Athumani Bahari amekemea tabia ya wanasiasa kuchanganya dini na siasa na kwamba wasitumie dini kuwa ni ngazi ya kufika malengo waliyopanga kufika.
“Kule kutuhumu Masheikh, Maaskofu na viongozi wa dini ni kiki ambayo mtu anatumia kwamba yeye aende sehemu anayohitaji kwa kutumia wao jamboa mbalo alipaswi kuungwa mkono hata kidogo.
“Hivyo haya yaliyotokea huko Temeke huenda ni baada ya kupeleka mwaliko kwa Masheikh wahudhurie mkutano huo kwa kuamini kwamba mkutano huo ungeenda vema na baada ya kuona hawajafika akaona malengo yake yanakwamba, hivyo masheikh wasitumike kwenye majukwaa ya siasa mbali na kutoa dua,” amesema Kahari.
Katika hatua nyingine Kahari amesema amesema Rais Samia anafanya kazi nzuri ambayo inapaswa kuungwa mkono na Watanzania kwani amekuwa akiwaunganisha bila kujali tofauti zao za dini.
Naye, Sharif Kisogwe ambaye ni Katibu wa Vijana Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam amesema wanalaani kauli ziliotolewa na Lema huku akisisitiza kwamba wanasiasa kwa nafasi zao hawapaswi kuchanganya dini na harakati za siasa.
“Leo hii katika siasa zinazoendelea wanasiasa wanasahau kujikita katika jukumu lao la msingi ambalo ni siasa badala yake wanawachanganya viongozi wa dini katika majukwaa yao, jambo hili siyo jema na tunalaani vikali kwani siyo utaratibu kwa nchi yetu ya Tanzania,” amesema Kisongwe.
Lema alisema nini?
Itakumbukwa juzi Jumapili Julai 23, 2023 katika mkutano huo wa Chadema uliokuwa na kaulimbiu ya Okoa bandari ambao ulifanyika katika viwanja vya buaga Temeke, akiwa katika mkutano huo Lema alisema kuwa: “Wachungaji na Masheikh wameogopa kuja eti wataonekana ni chadema, mbinguni kutakuwa na wacheza disko wengi kuliko hao masheikh, mbinguni kutakuweko na masela wengi kuliko Wachungaji na Masheikh feki, si mje mpiganie haki mfe tuwakute mbinguni,” alisema Lema.
Msajili anasemaje
Akizungumzia hilo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungia ambaye pia ni mlezi wa vyama vya siasa nchini amesema kuwa kwa mujibu wa sheria vyama vya siasa havipaswi kuchanganya dini na siasa.
“Kwa mujibu wa sehria vyama vya siasa havipaswi kuchanganya masuala ya dini na siasa badala yake vinapaswa kujikita kwenye siasa bila kuhusisha viongozi wa dini,” amesema Jaji Mtungi.