Na MWANDISHI WETU
-KAGERA
VIONGOZI wa dini mkoani hapa wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kwa kufanya maamuzi na kuchukua hatua zinazolenga kumwinua mwananchi mnyonge na kumfanya afaidike na rasilimali za nchi yake.
Katika mkutano wa pamoja na uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kagera juzi mjini Bukoba, viongozi hao wameeleza kuridhishwa kwao na juhudi zinazofanywa na Serikali na hasa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na yenye manufaa kwa umma.
Wametoa mifano ya ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema wanatambua na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kupambana na changamoto za kupunguza umaskini kwa watu wanyonge.
“Tunatumia kikao hiki kuipongeza Serikali kwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano baina ya Watanzania na kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo zinalenga masilahi mapana ya wananchi,” alisema Askofu Kilaini.
Katika kikao hicho, viongozi hao wa dini waliahidi kushirikiana na Serikali ya mkoa katika kudumisha amani na utulivu mkoani ili kudumisha mshikamano baina ya Watanzania.
Kama ilivyo desturi, mwaka 2019 umepewa jina la “Biluga Omumpiita”, ujumbe huo ukiwa na maana ya kwamba ‘maisha mazuri na kufanya kazi kwa bidii’.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, aliwaambia viongozi hao wa dini kwamba wao ni nguzo kuu ya amani katika mkoa na pia hutegemewa katika kudumisha maadili na kuwaunganisha wananchi na Serikali yao.
“Sisi serikalini tutaendelea kushirikiana na nyinyi kama ilivyo desturi ya mkoa wetu wa Kagera na tunawategemea sana katika kuhakikisha mkoa wetu unaendelea kudumisha amani na utulivu.
“Kila mara mnapokutana na waumini wenu mkahubiri amani na utulivu sisi kwetu kazi inakuwa nyepesi. Pia mnapowahimiza wananchi wafanye kazi, kwetu sisi inakuwa rahisi kwa sababu mnakuwa mmetangulia kuweka msukumo kwa wananchi,” alisema RC Gaguti.
Kikao hicho kilijumuisha viongozi wa dini wakiwamo Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta, Askofu Dk. Abedinergo Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kasikazini Magharibi.