NA SHOMARI BINDA,
UONGOZI wa Wilaya ya Tarime umefyeka mashamba 37 ya bangi yenye ukubwa wa ekari 56 wilayani humo katika oparesheni ya siku mbili, imeelezwa.
Oparesheni hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Andrew Satta na vikosi vya mbalimbali ulinzi na usalama.
Vilevile, walikamata magunia 20 ya bangi kavu yenye uzito wa tani moja ambayo yalikuwa yamekwisha kuandaliwa na kutunzwa kwa ajili ya kupelekwa sokoni.
Kamanda Satta, alisema katika oparesheni hiyo walikamatwa watuhumiwa 14 ambao wanajishughulisha na kilimo cha bangi.
Alisema watu hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani.
DC Luoga akizungumzia katika Kijiji cha Nyarwana na Matongo Kata ya Kibasuka, alisema katika oparesheni zote ambazo zimekuwa zikifanyika hiyo imefanikiwa zaidi.
Alisema kuharibiwa mashamba na kukamatwa magunia hayo ya bangi kumetokana pia na ushirikiano kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo.
Luoga alisema mikakati kabambe inaendelea kuandaliwa kukomesha kilimo cha bangi ikiwamo kuanzisha kilimo cha miwa katika mabonde.
"Tulianza mapema kupambana na zao haramu la bangi na maagizo kutoka ngazi ya taifa itaendelea kutusukuma katika mapambano haya na naamini tutafanikiwa na hizi oparesheni tunazoendelea nazo zinatusidia.
"Kuna watu ambao wanakuwa kama wanakwamisha jitihada hiuzi sasa hatuwezi kukubaliana nao na tutawashughulikia," alisema Luoga.
Alisema muda umefika kwa wale wanaojihusisha na kilimo cha bangi kujisalimisha na kuachana na zao hilo haramu .