Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
VIONGOZI wanne kati ya saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliotakiwa kuripoti polisi wameitikia wito huo baada ya kwenda katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Waliofika polisi jana ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Viongozi hao waliwasili kituoni hapo jana saa 6:06 mchana wakiwa wamevalia sare za chama chao huku wakisindikizwa na Mwanasheria wa chama hicho, Peter Kibatala na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya.
Viongozi hao wa Chadema walifikia hatua hiyo siku moja baada ya kutakiwa kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Polisi Dar es Salaam.
Viongozi wengine waliotakiwa kwenda polisi ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Vicent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) Salum Mwalimu ambaye pia alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni katika uchaguzi mdogo uliofanyika Febreuari 16 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitoa sababu za viongozi hao kutokufika kuwa walikuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli nyingine.
“Wakati tunaupata wito wa polisi, Salum Mwalimu alikuwa ameshatangulia kwenda Iringa kwa ajili ya maziko ya Katibu wa Kata ya Hananasif, Daniel John.
“Kuhusu Dk. Mashinji yeye aliondoka jana (juzi) saa 10 jioni kwenda Marekani kikazi, safari ambayo tulikwishaipanga kwa muda mrefu.
“Kwa upande wa Mwenyekiti Mbowe yeye alikuwa safarini nje ya Dar es Salaam,”alisema Mrema.
Hata hivyo licha ya viongozi hao wanne kutii wito huo wa polisi hawakufanyiwa mahojiano badala yake walitakiwa kurudi polisi Jumanne ijayo Februari 27 mwaka huu.
Baada ya uamuzi huo viongozi hao wote wanne waliachiwa kwa dhamana.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuachiwa, Mnyika alidai kuwa ingawa hawakufanyiwa mahojiano, lakini amebaini kuwapo kusudio la kutaka kuwabambikizia mashtaka mawili likiwamo la kufanya maandano bila ya kibali.
“Kusudio jingine ambalo nimeliona ni kutaka kuwabambikizia kesi viongozi hao kuhusisha na risasi ambayo ilisababisha kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Akwilina Akwilin.
“Sasa hili ni jambo ambalo halina msingi wowote kwa sababu wote waliokuwa eneo la tukio wanajua kwamba risasi hiyo ilipigwa nyuma ya basi, basi ambalo lilikuwa linatoka Magomeni kwenda Morocco.
“Sisi waandamanaji tulikuwa tunaelekea Magomeni kwa hiyo kwa vyovyote risasi isingeweza kutoka upande wa waandamanaji na kupiga nyuma ya basi… kwa hiyo hizi jitihada zitashindwa kwa hiyo tumekuja tuwasikilize wito wao,” alisema Mnyika.
Mwanasheria wa Chadema, Kibatala aliliambia MTANZANIA kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho hawakuweza kufika kutokana na sababu mbalimbali.
“Kwa mfano Katibu Mkuu yuko Marekani, hao wengine hawakupatikana kwa hiyo ngoja tuone hadi hiyo Jumanne ambayo wametakiwa kurudi kama watapatikana tutaambatana nao, lakini kama hawatakuwapo tutawajulisha polisi,” alisema Kibatala.
Kuhusu sababu za kutokuhojiwa kwa viongozi waliokwenda polisi, Kibatala alisema wameambiwa kuwa kuna taratibu hazijakamilika kwa hiyo bado wanaendelea na upelelezi.