22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE AWAOMBA VIONGOZI WASICHOKE KUKEMEA MAOVU

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye amewaomba viongozi wa dini wasichoke kukemea matendo maovu yanayoweza kulipekeka taifa pabaya.

Akizungumza katika Misa ya kuaga mwili wa Kada wa Chadema Kata ya Hananasif, marehemu Daniel John, Sumaye alisema viongozi wa dini wakihofia kukemea siasa chafu watalipeleka taifa kusikofaa.

Sumaye alisema Mungu ndiye anayehusika na roho za binadamu lakini imefika wakati baadhi ya watu wanaingilia kazi yake jambo alilodai kuwa halikubaliki.

“Tumesononeshwa sana na tukio hili la kinyama lililofanywa na wabaya hawa. Tunamuombea marehemu safari njema, kikubwa sote tutarejea kwa Mungu ili mzigo huu uwe mwepesi kwa kuwa tumeumia mno,” alisema Sumaye.

Paroko wa Kanisa Katoliki la Hananasif, Kinondoni, Alistadius Kibangula ambaye aliongoza ibada ya misa ya kumuaga John, alisema kifo chake ni fursa kwa waliobaki kujitafakari mapito yao na mwisho wa safari.

Alisema Mungu ana mipango ya kila mmoja ambapo katika baadhi ya maandiko anaondoa hofu na kuwainua kiimani binadamu hivyo kufa ni kubadili hali ya maisha.

“Hata Yesu alisema naondoka, naenda kuwaandalia makao. Nyumbani kwa baba yangu kuna makao, nikimaliza nitakuja kuwachukua ili nilipo mimi nanyi muwepo, ni tafakari kwetu hii,” alisema Padre Kibangula.

Alisema ni jambo la kutafakari na kujiuliza ili makao yatakayoandaliwa yasiwe ya uharibifu bali ya milele.

“Nawashauri tuishi kiimani kadri ya imani zetu, tupendane kwani lolote baya mtakalowatendea hawa mtakuwa mmenitendea mimi,” alisema Padre Kibangula.

Alisema adhimisho la misa hiyo ni kujiimarisha kiimani, kujenga matumaini na kuwaombea marehemu.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Thomas Kaijage alishukuru viongozi wa Chadema, dini, marafiki na majirani kwa kuungana nao katika kipindi kigumu.

Kabla ya kupelekwa kanisa kwa ajili ya ibada ya misa, marehemu aliondolewa nyumbani kwake Hananasif ambako mamia ya waombolezaji wakiongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema walifurika kumuuga.

Awali, majira ya saa 11.30 alfajili mwili wa marehemu ulipokelewa nyumbani kwake ukitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Vilio na simanzi vilitawala eneo la kanisa la Hananasif ambako mamia ya waombolezaii walijitokeza kuuga mwili wa marehemu.

Katika baadhi ya maeneo ya Kinondoni, askari polisi walionekana wakifanya doria wakiwa na gari tatu aina ya ‘Defender’ zilizokuwa na askari wenye silaha.

Baada ya kumalizika kwa misa, wanachama na wafuasi wa Chadema pamoja na majirani wa marehemu waliusindikiza mwili hadi kituo daladala cha Manyanya kabla ya kuzuiliwa na askari ambao waliruhusu magari peke yake kupita.

Mwili wa marehemu uliondolewa kanisani majira ya saa 9.15 kupelekwa Kitelewasi, Mafinga Mkoani Iringa kwa gari aina ya ‘Coaster’ lenye namba za usajili T 481 BNM.  ambapo msafara huo utaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana (Bavicha), Patrick Ole Sosopi.

 

Historia ya marehemu

Marehemu alizaliwa Desemba 26, mwaka 1980 na alifariki Februari 11, mwaka huu. Ameacha mjane Paulina na watoto wawili. Wakati wa uhai wake walikuwa akijishughulisha na upigaji picha wa kujitegemea.

Marehemu John  na rafiki yake Regnard Malya walitekwa Februari 11 na watu wasiojulikana, wakiwa eneo la nyumbani kwao Kinondoni kisha kupigwa maeneo mbalimbali ya mwili wao.

Ilidaiwa kuwa walipakizwa kwenye gari aina ya ‘LandRover’ nyeupe na kwenda kutupwa mahali ambapo Malya alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mwili marehemu John uliokotwa katika Ufukwe wa Coco na kupelekwa Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kabla ya kwenda kutambuliwa na mkewe na rafiki zake wa karibu Februari 13, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles