Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi amewataka viongozi wa chama hicho kufanyakazi kwa karibu na watendaji wa Serikali bila kiburi kwa sababu ni wajibu wa kikatiba na Ilani ya chama.
Dk.Nchimbi ameyasema hayo leo Januari 20,2021 jijini Dar es S wakati akipokelewa rasmi na viongozi mbalimbali wa chama na wanachama.
Amesema chama hakipaswi kukwepa wajibu wake wa kuisimamia Serikali lakini kinatakiwa kusimamia kwa kufuata misingi na kufanya kazi kwa weledi.
“Chama chetu kitaendelea kutimiza ahadi zake na kuisimamia Serikali, naahidi kushirikiana na viongozi wenzangu kukiimarisha chama lakini pia kuhakikisha hatumuangushi Rais wetu,”amesema Dk.Nchimbi.
Akizungumzia maandamano amesema wananchi na wanaCCM wanapaswa kuyapuuza maandamano hayo kwani hayana tija kwa Taifa.
Amesema kukimbilia kwenye maandamano ni dalili ya uoga kwani uongozi thabiti unapimwa kwa hoja.
“Kukimbilia kwenye maandano ni dalili ya uoga na kushindwa niwasihi wana CCM na wananchi kwa ujumla wanapoona maandamano yao wajue wameshindwa kufikiri kupitia ubongo wao sasa wanafikiri kupitia miguu yao,” amesema.
Aidha ametoa rai kwa vyama vya siasa kuendelea kushirikiana na CCM ipo tayari kushirikiana na chama chochote cha siasa na milango ya ofisi yake ipo wazi.
Amesema viongozi hao wa siasa na wana CCM wanapaswa kuyaeleza mazuri yaliyofanywa na serikali bila aibu.
“Hakuna sababu ya chama kutopata ushindi katika uchaguzi wa serikali ya mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025 ni kuongeza kasi ya ushindi,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtevu amesema chama kinatarajia kushinda kwa kishindo mitaa yote 574 ya mkoa wa huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila amesema wanatekeleza kwa vitendo ilani ya chama hiko hivyo viongozi wanapoanza kampeni hawatapata tabu kujieleza kwa wananchi badala yake kazi zinajieleza zenyewe
“Tunatekeleza Ilani vizuri ili chama kisipate tabu na hata mvua zilizonyesha leo tunawaahidi wananchi kesho miundombinu yote iliyoleta shida, kesho itakuwa sawa,”amesema Chalamila.