31.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana wahimizwa kufungua kampuni

Mwandishi wetu -Lindi

MAFUNZO ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana wajasiriamali ambayo yamegharamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, yakiratibiwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, yamepokewa vema na vijana wa Mkoa wa Lindi.

Hadi wakati huu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu imeshawafikia vijana kwenye mikoa ya Dodoma, Geita, Mwanza, Ruvuma, Songea, Mbeya na hivi sasa yanaendelea kufanyika Mkoa wa Lindi.

Mafunzo hayo kwa mara ya kwanza yalizinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama Julai 29 mwaka huu jijini Dodoma na yanatarajiwa kufikia vijana wasiopungua 1,200 katika mikoa minane nchini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo mkoani Lindi, Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Silas Daudi, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya programu ya kitaifa ya ukuzaji ujuzi ambayo inatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau.

Daudi alizitaja baadhi ya programu zinazotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo wa elimu na mafunzo ya kuongeza ujuzi kulingana na mahitaji ya vijana.

“Kupitia programu hizi, Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu imepanga kujenga kitalu nyumba (green house) kimoja kwa halmashauri zote nchini na kuwafundisha vijana 100 kila halmashauri kutumia kitalu nyumba ambavyo vitatumika kama shamba darasa kwa vijana kujifunza teknolojia hii.

“Hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu imejenga kitalu nyumba kimoja na kuwafundisha vijana 100 kwa kila halmashauri katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na zoezi hili linaendelea katika mikoa 14 iliyobaki,” alisema Daudi.

Alisema kuwa kundi la vijana ndiyo sehemu kubwa ya nguvu kazi ya taifa na kwamba kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014, vijana wanafanya asilimia 56 ya nguvu kazi ya taifa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa kundi la vijana katika taifa, programu zote zimeandaliwa maalumu kwa kundi hili kuwawezesha kujiajiri kwa tija na kuongeza wigo wa ajira kwa vijana wengine.

“Tunaamini kupitia mafunzo haya utakuwa mwanzo wa vijana kuanzisha makampuni yao binafsi, kusimamia na kufanya biashara kwa tija na kutengeneza ajira kwa vijana wengine, lakini pia elimu hii itawasaidia kujua ni sifa zipi wanapaswa kuwa nazo pindi wanapozisogelea fursa za mikopo na ruzuku kutoka kwenye mifuko ya uwezeshaji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles