Ferdnanda Mbamila -Dar es Salaam
SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika lale la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), imesaini mkataba wenye thamani ya dola za Marekani milioni 10 na Benki ya Amana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Naibu Mkurugenzi wa USAID Idara ya Afrika, Dk. Diana Putman, alisema lengo la DCA ni kuimarisha uwezo wa benki kutoa fedha katika shughuli zinazohusu kilimo na biashara ndogondogo za kati zinazomilikiwa na wanawake na vijana nchini.
Dk. Diana alisema mkataba huu umekusudia kuimarisha uwezo wa Benki ya Amana kutoa fedha kwa wakulima, tunatarajia utachangia katika ukuaji endelevu wa biashara zinazohusiana na kilimo.
Alisema mbali na kufadhili upatikanaji wa mikopo, mkataba huo umeongeza upatikanaji wa wateja kwa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar.
“Wakati USAID inashirikiana na benki za Kiislamu katika maeneo mengine duniani, mkataba na Benki ya Amana ni wa kwanza kwa benki ya Kiislamu Kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema.
Aidha Dk. Diana alisema Serikali ya Marekani inaunga mkono maendeleo ya biashara na mchango wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na uwezo wa kufikia hadhi ya kujitegemea.