Na GABRIEL MUSHI
“NIMEKUWA mmoja wa vijana waliokumbana na athari za ukeketaji kwa dada zetu baada ya kushindwa kuendelea na uhusiano wa kimapenzi na msichana mmoja ambaye alikuwa amekeketwa. Sababu mojawapo iliyosababisha tuachane ni kutofurahia tendo la ndoa.” Hayo ni baadhi ya maneno ya kijana Kelvin Josephat (29) Mkazi wa Kiomboi Kitunda.
Kelvin ni mmoja wa vijana waliozungumza na MTANZANIA kuhusu athari walizoziona ndani ya jamii inayowazunguka kuhusu ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji.
Anasema imekuwa ni aibu kwa binti wa kabila ambalo hupendelea mila na desturi kukeketa kutofanyiwa kitendo hicho na hata hufikia hatua ya kutengwa pale anapofikia hatua ya kuolewa endapo atagundulika kuwa hakupitia mila hiyo.
“Baadhi yao hawapendi kukeketwa, ila wanalazimika kufanyiwa hivyo kutokana na uamuzi wa wazazi katika kutekeleza mila na desturi zao.
“Lengo kubwa la kuwakeketa ni kuwafanya wanawake wasiwe wahuni au kujihusisha na uhusiano na wanaume wengi, ndio maana huwaondoa sehemu ile ambayo inaaminika kuwa huwa inawaletea hamu ya kufanya mapenzi,” anabainisha Kelvin.
Ukeketaji ni nini?
Ofisa Mwezeshaji wasichana kutoka Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Lennyster Byalugaba anatafsiri neon ukeketaji kuwa ni upasuaji wa sehemu za nje za viungo vya uzazi ambavyo vinakatwa kusudi wasifurahie tendo la ndoa, hivyo wawe waaminifu zaidi kwa waume wao.
“Ukeketaji umeenea hasa kati ya mataifa na makabila wenye asili ya bonde la Mto Nile na majirani zao. Unasababisha wasichana wengi kufa na wengine kupatwa na maumivu makali wakati wa hedhi, tendo la ndoa na kujifungua,” anasema.
Anasema ukeketaji ni aina mojawapo ya ukatili wa kijinsia ambao hapa Tanzania ni tatizo kubwa ambalo linawanyima uhuru wanaume, wanawake na watoto kufurahia haki zao za msingi ambazo pia ni haki za binadamu.
“Tatizo hili lipo duniani kote kwani tafiti zinaonesha kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu katika maisha yake amewahi kufanyiwa ukatili wa kijinsia ama kimwili, kingono na kisaikolojia. Tafiti pia zaonesha kuwa duniani kote, asilimia 16-52 ya wanawake wanafanyiwa ukatili wa kimwili na waume au wapenzi wao walau mara moja katika maisha yao. Hali duni ya kiuchumi na kutofahamu sheria kunawafanya wahanga wengi wa ukatili wa kijinsia kushindwa kupata msaada pindi wanapofanyiwa ukatili huo,” anasema.
Ushiriki wa vijana kupinga ukeketaji
Piramidi ya idadi ya watu nchini inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu Tanzania ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 na vijana. Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2012 asilimia 77 ya Watanzania wana umri ulio chini ya miaka 35 na asilimia 19 wanaumri kati ya miaka 15 – 24.
Kwa kuwa vijana ndio nguvu au chachu ya mabadiliko katika jamii, CDF imeamua kuwatumia vijana ili kurahisisha utoaji wa elimu katika kata ya Kitunda ambayo katika utafiti wa awali uliofanywa na jukwaa hilo, umeonesha Manispaa ya Ilala inaongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji ambao umekithiri katika kata ya Kitunda inayoishi watu wenye mila na desturi za makabila yanayohusudu vitendo hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Lennyster anasema licha ya kwamba mradi huo ambao umefadhiliwa na ubalozi wa Uholanzi, umelenga kuhamasisha jamii katika kupinga ndoa za utotoni na ukeketaji, wameamua kuhusisha wanaume hasa vijana ili kuangalia wana jukumu gani katika kupinga vitendo hivyo.
“Vijana wapo tayari kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka kwa sababu wavulana au wanaume ndio changamoto kubwa katika jamii zetu, ndio wanaowapa mimba watoto wa kike lakini pia wanaotoa uamuzi katika familia.
“Kwa mfano, mtoto akeketwe ama lah! mama ana uamuzi lakini baba ndio kichwa cha familia. Kwa hiyo, tumeona ni vizuri kuwahusisha hawa ili wakatoe elimu kwa familia zao na wanaume wenzao juu ya masuala haya,” anasema.
Gerad Mkanza (28) ni mmoja wa vijana wanaoishi katika kata hiyo, anasema baadhi ya mabinti katika jamii inayowazunguka wamekeketwa kutokana na kulazimishwa na wazazi wao ili tu kutekeleza mila na desturi za makabila yao.
“Kuna binti namfahamu aliketetwa, nikaumia baada ya kunieleza wazi kuwa amefanyiwa hivyo kwa nguvu.
“Nilienda kuonana na baba yake, nikamnunulia pombe ili aniweke wazi kwanini amechukua uamuzi huo, ndipo akanieleza wazi kuwa hiyo ni mila na desturi yao, ila baada ya kumweleza madhara ya kitendo hicho alionekana kujutia kumlazimisha binti yake akeketwe.
“Tunaona kuwa watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 15 wanajielewa ila hawana uamuzi dhidi ya wazazi wao, hivyo ni vyema sisi wanaume hususani vijana kuzungumza na wazazi wetu ili kuibadilisha jamii.
Mikakati iliyowekwa
Ofisa Mtendaji Kata Kitunda, Festo Mlimila anasema katika kata hiyo yenye wakazi 32,188, moja ya mikakati waliyoweka ni kuwashirikisha wanaume katika utoaji elimu kuhusu madhara ya ukeketaji.
“Dhana ya ukeketaji iliyopo kwenye kata yangu inatokana na makabila ambayo kiujumla hutekeleza tamaduni zao kule Mara. Kwa hiyo, hiki ni kitendo cha kimila ndio maana kinapotokea huko mikoani kwao na huku lazima wafanye kwa mujibu wa taratibu zao. Kwenye kata yetu haifanyiki moja kwa moja uwazi lakini katika kata ya Kivule nako matukio hayo yameshamiri na kuna mangariba.
“Tunashirikiana na CDF kutoa elimu ndio maana sasa haya mambo huwezi kuyakuta wazi, yanafanyika kwa vificho na yanapotokea polisi wanachukua hatua,” anasema.