26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

SHERIA YA MATIBABU INAYOMPA HAKI MGONJWA KUMSHTAKI DAKTARI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

ILI binadamu aweze kutimiza majukumu yake ya kila siku ni lazima awe na afya njema, inapotokea ameugua huhitaji kupata tiba dhidi ya ugonjwa unaomsumbua.
Miaka ya nyuma, huduma za matibabu zilikuwa zikitolewa zaidi katika
vituo vya afya,
zahanati na hospitali zinazomilikiwa na serikali.
Baadae tukashuhudia mashirika ya dini na taasisi mbalimbali nazo
zikipata kibali cha kuanzisha huduma hizo za matibabu na hata watu binafsi.
Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, Maulid Kikondo anasema hali hiyo
imesababisha baadhi ya wamiliki kutoa matibabu kwa lengo la kufanya kibiashara zaidi kuliko kutoa huduma.
“Kwa kawaida mtu anapopatiwa matibabu huwa ni kwa nia njema, lakini kama ilivyo kwa mambo mengine ingawa ni jambo jema, kuna wakati matatizo mbalimbali hujitokeza,” anasema.
Anasema matatizo hayo mara nyingi hujitokeza kati ya mtoa huduma na mpokea huduma.
“Unapokuwa na mfumo wa biashara kwenye matibabu huwezi kuwakwepa
wajanja wajanja, kwa sababu siku zote wafanyabiashara hutaka
kutengeneza faida na hapa ndipo ‘yanapozaliwa’ matatizo.
“Kwa mfano, unakuta mtu amekwenda hospitalini anajikuta anaandikiwa vipimo vingi ambavyo vingine wala havihitaji kupewa dawa nyingi,
kwa sababu mmiliki anahitaji kupata faida,” anabainisha.
Anasema ingawa si wamiliki wote wenye nia hiyo, lakini kati ya wale
walio waamini wanaofanya kazi kwa kuzingatia maadili wapo ambao hufanya kinyume.
“Miaka ya nyuma madaktari wengi walikuwa wakisoma hapa nchini na walikuwa rahisi hata kufahamiana na kujuana, tofauti na leo hii wengine wanasoma nje ya nchi na wanarudi kufanya kazi nyumbani,”
anasema.
Anasema wakati walipokuwa wachache ilikuwa rahisi kujua na kukosoana pale ambapo mwenzao anakuwa amefanya makosa katika kutoa matibabu
tofauti na sasa.
Anasema kutokana na hali hiyo, ni muhimu sasa jamii kuanza kujifunza, kuifahamu na kuielewa vema sheria ya matibabu.
“Kutokana na matatizo ya matibabu yanayoweza kujitokeza kati ya mtoa huduma na mpokea huduma, kilitengenezwa kipengele maalumu cha
sheria kwa lengo la kuyatatua,” anasema.
Wakili huyo anafafanua kuwa wataalamu wa sheria walitengeneza ‘Medical
legal’ ambayo baadae ilitumika kutengeneza kipengele cha ‘medical
Negligence’ ambacho kazi yake ni kushughulika na haki za wagonjwa.
“Yaani inapotokea mgonjwa amepata madhara yoyote wakati akipatiwa matibabu, kipengele hicho kinaeleza nani ambaye anawajibika kwa
madhara hayo,” anabainisha.

Anasema kuwa kipengele hicho cha sheria kilitengenezwa makusudi ili kulinda haki za mgonjwa, kwamba kinaeleza wazi wakati gani daktari anapaswa
kuwajibika pale ambapo inatokea anatoa matibabu kinyume na taratibu zilizowekwa.
Anasema sheria hiyo lengo lake kuu ni kusimamia na kulinda haki
za mgonjwa kuhakikisha anapatiwa matibabu sahihi yanayostahili.

Jinsi inavyofanya kazi
Anasema jambo ambalo kila mtu anapaswa kulijua ni kwamba daktari anapaswa kupata idhini ya mgonjwa kabla ya kumpatia matibabu.
“Ili daktari awe na haki ya kutoa matibabu ni lazima pawe na idhini ya mgonjwa, aridhie mwenyewe na kabla ya kuridhia kutibiwa lazima pawepo majadiliano.
“Daktari anapaswa kumweleza kwa kina mgonjwa kwa mfano juu ya faida na madhara ya matibabu (dawa) au sindano atakayochomwa.
“Lazima daktari amweleze mgonjwa ili aridhie mwenyewe iwapo apatiwe matibabu kwa dawa au sindano aliyoipendekeza.
“Mgonjwa naye anakuwa tayari anaelewa kwamba ingawa hiyo anayopatiwa ni tiba lakini labda inaweza kumsababisha athari nyingine mwilini,
kwa mfano itasababisha figo zake kushindwa kufanya kazi,” anasema na kuongeza:
“Lakini hapa kwenye idhini ya mgonjwa wakati mwingine huwa
kuna utata, wapo watu ambao hudhani kwamba mgonjwa akisema sawa huku
akiwa hajaelezwa faida na madhara ya matibabu anayopewa ni sahihi jambo ambalo si sawa.
“Sheria inataka lazima pawe na ‘informed concept’ mgonjwa lazima aelezwe na aelewe hasa huduma anayokwenda kupatiwa ni ipi ili atoe idhini yake.”
Anasema inapotokea kwa bahati mbaya mgonjwa ndiye aliyesaini fomu ya matibabu na hakukuwa na majadiliano ya kutosha
kuelezwa juu ya kile anachokubaliana, iwapo atapata madhara moja kwa
moja daktari aliyempatia huduma anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa sheria hiyo.
“Madaktari wanaifahamu vema sheria hii na wengi wapo makini katika utendaji wao, ndiyo maana kabla ya kumuhudumia mgonjwa hufanya majadiliano kwa sababu akienda kinyume anaweza kushtakiwa kwa sheria
hii.
“Hata kabla daktari hajakuchoma sindano lazima akueleweshe
kwa kina juu ya matibabu hayo na wewe mwenyewe uamue kama akutibu au la.
Anasema watu wengi wamekuwa wakipatiwa matibabu yasiyo sahihi na kuishia kupata madhara hata hivyo, kwa kuwa hawana uelewa wowote kuhusu
sheria hiyo wamekuwa wakiugulia majumbani mwao.
“Uelewa wa Watanzania kuhusu sheria hii ni mdogo mno, wengi wanapata madhara na hawajui kwamba wanaweza kupata haki yao kwa kushtaki
mahakamani, kesi zinazokuja mahakamani ni chache mno. Mataifa yaliyoendelea wanaitumia sheria hii kudai haki zao,” anabainisha.

Lazima uandaliwe kisaikolojia

Wakili Maulid Kikondo anasema ingawa sheria inatambua kwamba mgonjwa anapochukua uamuzi wa kukaa mbele ya daktari ni hatua ya kuridhia,
kuna matibabu ambayo daktari anapaswa kumuandaa kisaikolojia
mgonjwa kabla ya kumtibu.
“Kwa mfano mgonjwa ni wa jinsi ya kike na daktari ni mwanamume, ikiwa
itabidi avue nguo kwa mfano ili atibiwe, ni lazima daktari amueleze mapema ili ajiandae kisaikolojia,” anasema.
Anasema kwa kuwa mgonjwa ana haki na maisha yake ataamua mwenye iwapo
apatiwe matibabu hayo au la na kwamba daktari hapaswi kumlazimisha.
Matibabu kwa mtoto
Anasema ni makosa daktari kumtibu mtoto aliye chini ya umri wa miaka
18 kabla ya kupata idhini kutoka kwa wazazi au walezi wake.
“Ndiyo maana kabla ya kumfanyia matibabu yoyote mtoto chini ya miaka 18 lazima
wazazi wake waitwe, wao watatoa idhini kwa niaba yake,” anafafanua.

Mgonjwa aliyezidiwa
Wakili huyo anasema taaluma inampatia haki daktari kumsaidia na kumuhudumia mgonjwa aliye katika hali mbaya ambayo inaweza kumsababishia kupoteza maisha bila kusubiri idhini yake.
“Yaani kwa mfano, mtu amepata ajali na kufikishwa haraka hospitalini, daktari ana haki ya kumsaidia bila kusubiri majadiliano na idhini ya
mgonjwa, lakini anachopaswa kufanya  ni kutibu tatizo
lilomfanya mgonjwa kufikishwa hospitalini.
“Kwamba, labda anajeraha linatoka damu nyingi, atatibu jeraha hilo
pekee ikiwa mgonjwa huyo ana tatizo jingine kwa mfano aliwahi kuumia jicho lake huko miaka ya nyuma, daktari hana haki kumtibu kwa wakati
huo kwa sababu mgonjwa hajaridhia,” anasema.

Sheria msumeno
Anasema wakati sheria hiyo ikilinda haki za mgonjwa wakati mwingine pia hulinda haki za daktari anayempatia matibabu.

“Kwa mfano, daktari amepokea majeruhi wa ajali amempatia huduma lakini kwa bahati mbaya majeruhi huyo akafariki dunia na ndugu wakalalamika
kwamba daktari amesababisha kifo cha ndugu yao tutasikiliza maelezo ya pande zote mbili.

“Ikiwa mgonjwa huyo
alifariki wakati daktari akitimiza wajibu wake wa kumsaidia kuokoa maisha kwa kutibu tatizo lililokuwa likihatarisha uhai wake, basi daktari husika anakuwa huru.
“Lakini ikiwa mgonjwa alifariki wakati daktari akitibu tatizo jingine ambalo halihusiani na ajali hiyo, bila idhini ya mgonjwa hapo anakuwa matatani na atahukumiwa kwa mujibu wa sheria,” anafafanua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles