Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kuelekea siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi Taasisi ya VIJANA THINK TANK(VTT) limetoa hamasa kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi nchini, kusoma masomo hayo kwa vitendo ili kuona Sayansi inavyofanyakazi katika mazingira halisi.
Hayo yamesemwa na msimamizi wa maji na Bwawa la mradi mkubwa wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Mhandisi Dismas Mbote alipokua akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Halisi waliokwenda kutembelea mradi huo Februari 5, 2021 kujionea namna taaluma ya Sayansi inavyotumika katika kutekeleza mradi huo.
Mhandisi Mbote amesema kuwa, wanafunzi wanapojifunza masomo ya Sayansi nje ya darasa inawasaidia zaidi kuona ni namna gani sayansi inafanya kazi katika mazingira halisi na hivyo kuleta hamasa ya kupenda masomo hayo na fursa za kuwa wabunifu zaidi.
“Ni muhimu masomo haya yatolewe katika uhalisia wa vitendo yani “practical”, hii itasaidia wanafunzi kuona uhalisia wa Sayansi, kama ambavyo leo wamejifunza Sayansi ya ujenzi wa Bwawa hili na hatua zote za ujenzi wa handaki maalumu la kuchepusha maji, na hatua nyingine zitakazofuata za ujenzi wa Bwawa, hii yote ni Sayansi,” alisema Mhandisi Mbote.
Ameongeza kuwa, TANESCO ni mdau mkubwa wa masuala ya Sayansi, hivyo inatoa fursa kwa wadau mbalimbali kutembelea mradi wa JNHPP kujifunza Sayansi ya ujenzi wa Bwawa la kihistoria litakaloleta mageuzi katika sekta ya Nishati ya Umeme nchini.
“Kama walivyokuja wanafunzi hawa, wamepata elimu hii hivyo niwakaribishe na wadau wengine wa Sayansi kutembelea kituo hiki na kujifunza zaidi”, aliendelea kusema Mhandisi Mbote.
Naye mwalimu wa sayansi katika shule ya Sekondari halisi, Hassan Mkingie ameishukuru Vijana Think Tank(VTT) kwa kuandaa safari hiyo pamoja na TANESCO kwa kudhamini wanafunzi kutembelea mradi huo na kusema kuwa, imeleta hamasa kubwa kwa wanafunzi hasa wa kike kupenda zaidi masomo ya Uhandisi.
“Wanafunzi wamefurahia ziara hii na wengi wametamani kuwa wahandisi wa Umeme”, amesema Mkingie.