Na Zuena Msuya Dar es Salaam
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ametaka Meneja wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Kinyerezi I, Ubungo I pamoja na Mhandisi Mkuu wa Kinyerezi II, Kinyerezi I, na Ubungo I, wasimamishwe kazi na wachunguzwe kwa uzembe.
Dk. Kalemani ametoa maagizo hayo, wakati wa ziara yake ya kukagua vituo hivyo na baadaye kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Februari 06, jijini Dar es Salaam.
Aidha alitoa siku kumi na nne (14) kwa Bodi hiyo kuwafanyia uchunguzi mameneja na wahandisi wakuu hao na kumpatia majibu stahiki Waziri wa Nishati.
Dk. Kalemani alisema kuwa, alifanya maamuzi hayo baada ya kubaini uzembe uliofanyika katika vituo hivyo, ikiwemo kutokuwepo kazini kwa watendaji hao na kutowajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
“Haiwezekani Meneja na Mhandisi Mkuu wote wasiwepo katika vituo vyenu vya kazi bila sababu za msingi, mitambo yote inafanyiwa ukarabati kwa wakati mmoja! Hapana, hii haiwezekani ni uzembe wa hali ya juu lazima wachunguze na waondoe katika nafasi zao za kazi hawa watu wasije kutuletea matatizo,”alisema Dk. Kalemani.
Aidha aliiagiza Bodi ya TANESCO, kuhakikisha kuwa, mtaalamu wa kuunga kifaa cha kubusti umeme kilichopata hitilafu katika Kituo cha Kupoza umeme cha Kinyerenzi I, anapatikana na kufunga kifaa hicho ndani ya siku tatu (3) kuanzia leo na kituo hicho kizalishe umeme kama ilivyokuwa hapo awali.
Sambamba na hilo, aliwataka wataalamu wanaofanya ukarabati katika vituo hivyo kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kukamilisha matengenezo hayo haraka, ili kuruhusu vituo hivyo kuzalisha umeme wote unaotakiwa katika kituo husika.
Vilevile aliitaka Bodi hiyo kufanya ukaguzi katika vituo vya kupoza na kusambaza umeme ili kuona hali halisi ya uzalishaji wa umeme katika mitambo yote, na ndani ya kipindi cha miezi miwili (2) mitambo yote tisa (9) iwe inafanya kazi kwa ufanisi.
“Bodi muanze kufanya uchunguzi kwa wataalamu wanaosimamia mitambo ya umeme, na endapo mtabaini asiyemuaminifu na anayekwenda kinyume na maadili yake ya kazi, lazima achukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu mapema hata kabla ya wizara kuingilia kati,” alisisitiza Dk. Kalemani.
Katika hatua nyingine, aliwataka Mameneja TANESCO katika maeneo ya Chanika, Gongolamboto,Pugu na ukanda mzima wa maeneo hayo waeleze sababu ya kukatika kwa umeme katika maeneo hao mara kwa mara hali ya kuwa hakuna mgao na umeme upo mwingi wakutosha na ziada.
Alieleza wazi kuwa, endapo mameneja hao wameshindwa kutatua tatizo hilo ni dhahiri wameshindwa kufanya kazi, hivyo waondolewe katika nafasi hizo na wawekwe wale wenye uwezo wa kuwahudumia wananchi.
Akizungumzia suala la upatikanaji wa umeme nchini, Dk. Kalemani alisema kuwa, hataki kusikia malalamiko ya wananchi kukosa umeme kwa sababu ya mitambo kuharibika, pia kuwaunganishia huduma ya umeme wale wote ambao wamekwisha lipia huduma hiyo kwa kuwa vifaa vipo vya kutosha, umeme upo mwingi na wakutosha.