Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umesema Rais Dk. John Magufuli hajawahi kutamka mahali popote kama Serikali ni ya kwake na si ya CCM, kama ilivyodaiwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Pia umoja huo umesema pamoja na Serikali kuongozwa na Rais Magufuli, bado iko chini ya Chama Cha Mapinduzi na kumtaka Mbowe kuacha maneno ya upotoshaji na uchochezi wa kitoto.
Msimamo huo umetolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipozumgumza na waandishi wa habari kufuatia madai ya Mbowe dhidi ya Rais Magufuli na utawala wake.
Alisema tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita, amekuwa akihimiza shime ya kukuza fikra mpya na kudumisha uzalendo ulioporomoka na kuzaa kundi la mafisadi, wezi wa mali za umma bila kujali itikadi za kisiasa, kwa sababu uzalendo hauna alama ya siasa au chama.
“Mbowe ni mwanasiasa mnafiki na profesa wa kuzua. Amesahau alipowakusanya wananchi pale Mwembeyanga Temeke na kutaja orodha ya viongozi wa Serikali aliodai ni mafisadi likiwemo jina la Edward Lowassa aliyehamia Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais,” alisema Shaka.
Alisema ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ni miliki ya CCM na Rais Magufuli hana ilani binafsi ya uchaguzi, hivyo akamtaka Mbowe aache kumlisha maneno kiongozi huyo wa nchi kwa kusaka kwake umaarufu wa kisiasa.
Akizungumzia madai kuwa utawala wa Rais Magufuli umekuwa ni wa kimabavu, ubaguzi na kujali ukanda na ukabila, Shaka alisema huo ni uzushi mpya kwani sera ya ukanda, ukabila na udini ni ya Chadema kutokana na ushahidi mwingi.
“Mbowe aache kufuatilia mambo ya CCM kwa sababu hayatamsaidia yeye au chama chake. Hana sifa ya kuwa kiongozi mkweli mbele ya Watanzania, kwa sababu ni wakala wa mafisadi na chama chake kimekuwa maficho ya viongozi wasiotamanika katika jamii,” alisema.
Aidha alisema Serikali ya awamu ya tano haijawahi kukataa kupokea ushauri au maoni ndiyo maana Rais Magufuli amekubali hata kupokea ilani ya uchaguzi ya CCM kama mwongozo wake na hakuna mwenye uwezo wa kumpangia namna ya uteuzi wa wasaidizi wake.
Shaka alisema CCM itaendelea kuamini na kufuata Itikadi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ujamaa si utitiri wa vibanda vya nyasi na kadhia ya umasikini bali ni imani na utekelezaji.