31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YAONYA VYAMA VYA SIASA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevionya vyama vya siasa kutogeuza kampeni za uchaguzi mdogo na kuwa mikutano ya vyama vya siasa.

Hivi sasa vyama mbalimbali vinaendelea na kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43, ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 26.

Akizungumza jana wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alisema vyama vinatakiwa kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili na taratibu zilizoainishwa kwenye uchaguzi.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, tume inayo mamlaka ya kuruhusu kuwepo kwa kampeni za uchaguzi na siyo mikutano ya vyama vya siasa,” alisema Jaji Kaijage.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, alifafanua kuwa anayeruhusiwa kufanya kampeni ni mgombea husika, chama chake au mtu yeyote ambaye mgombea ataona anafaa.

“Tume haijaruhusu mikutano ya vyama vya siasa bali mikutano ya kampeni kwa lengo la kuwashawishi na kuwahamasisha wapenzi wa vyama wampigie kura yule ambaye wanamtaka.

“Mkutano wa kampeni ni ule wa kumnadi mgombea na haiwezekani ukafanye mkutano katika kata ambayo haifanyi uchaguzi,” alisema Kailima.

Alisema wapigakura 333,309 wanategemewa kupiga kura katika uchaguzi huo ambapo vituo 884 vitatumika kupiga kura.

Katika hatua nyingine, tume hiyo imesema hadi sasa bado haijapokea taarifa yoyote kutoka kwa Spika wa Bunge au Mahakama inayoonyesha kwamba Jimbo la Longido liko wazi.

“Tume inatangaza kile ambacho imekithibitisha, taratibu za Longido na kwenye maeneo mengine zitafuata muda si mrefu, hivyo vuteni subira,” alisema Kailima.

 

VYAMA VYA SIASA

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AFP), Rashidi Rai, alisema taifa limeingia katika hatua ambayo haijazoeleka na kuiomba Serikali iruhusu mikutano ya vyama vya siasa.

“Tutumie uchaguzi huu kufanya kampeni za kiungwana, huku tukiendelea kuomba mamlaka husika ituruhusu kufanya mikutano ya vyama,” alisema Rai.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Johnson Mwangosi, alisema uwanja wa kisiasa nchini si mzuri kwa sababu sheria mbalimbali zinavunjwa.

Katibu Mkuu Baraza la Wazeee Chadema, Rodrick Lutembeka, alisema licha ya kuwapo kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi, lakini bado kuna changamoto kwenye kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles