27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

KINGWANGALLA, NYALANDU WATIFUANA

ESTHER MBUSSI-DODOMA


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemlipua aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akidai alitumia madaraka yake vibaya akiwa waziri wa wizara hiyo.

Alisema alisababisha serikali ikose mapato ya Sh bilioni 32 kwa kukataa kusaini tozo ya hoteli za utalii iliyopendekezwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Dk. Kigwangalla alidai pia kuwa Nyalandu alikuwa akifanyia kazi katika chumba maalumu kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Kauli hiyo aliitoa bungeni  Dodoma jana alipokuwa akitoa maelezo ya wizara yake  mwishoni mwa mjadala wa  wabunge kuhusu mpango wa maendeleo wa serikali uliowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Philip Mpango.

Wakati akisema hayo,  Nyalandu naye amejibu mapigo na kumtaka Waziri  Kigwangalla athibitishe madai yake kwamba alikuwa akifanyia kazi katika chumba maalumu kwenye hoteli ya Serena.

Nyalandu alimtaka waziri aeleze namba ya chumba  na uthibitisho kutoka kwa wahusika wa hoteli hiyo.

Alisema kwa kipindi chote alichofanya kazi katika   Wizara ya Maliasili na Utalii, alitambua kwamba naye alikuwa mteule wa Rais ambaye ana vyombo vya kumsaidia kusimamia nyendo za mawaziri.

Akirusha makombora yake bungeni jana, Dk. Kigwangalla alisema jambo ambalo limejitokeza kwa kiasi kikubwa na alitaka kulitolea ufafanuzi ni   kwamba akiwa Waziri mpya wa Maliasili na Utalii ameanza kazi kwa kufukua makaburi.

“Naomba niseme tu mimi si mashuhuri   kwa ufukuaji wa makaburi.

“Lakini ukiwa waziri na ukawekwa katika wizara ambayo wiki ya kwanza tu hata hujaanza kazi kila mtu anasema umekalia kuti kavu, ni lazima kabla hujaanza kazi uliyopewa usafishe kwanza,  usafishe nyumba yako.

“Na   kwa msingi huo tumeanza kazi na tayari mpaka pale mtandao wote wa watu wote waliopo kwenye wizara hii  wanashiriki kwenye ujangili, hujuma na wamekuwa wakitajwatajwa kwenye kashfa mbalimbali za rushwa, tutashughulika nao kwanza.

“Tukimaliza kuing’oa hiii mitandao sasa tutaanza kazi kubwa tatu na za maana zaidi katika nchi yetu ya kuongeza idadi ya watalii na idadi ya vivutio.

“Tutafanya hivyo kwa kuwekeza kwenye kanda nyingine kama kusini ili kuifungua korido ya kusini na serikali imepata takriban Sh milioni 300 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kuifungua kanda ya kusini kwa utalii,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kabla hawajafikia kuanza kutekeleza mipango yote hiyo ni lazima  aanze kusafisha na kwamba hakusudii kufukua makaburi ya mawaziri wazuri waliopita katika wizara hiyo wakapata ajali mbalimbali za siasa kama kina Ezekiel Maige, Balozi Khamis Kagasheki na Profesa Jumanne Maghembe.

“Labda nianze kwa kumzungumzia waziri mmoja ambaye wenzetu hawa wa upinzani walimsema sana alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na huyu si mwingine bali ni ndugu Lazaro Nyalandu.

“Nataka niseme tu kwamba rafiki yangu Joshua Nassari alizungumza kwa mbwembwe nyingi sana hapa bungeni kwamba kama Dk. Slaa….”

Lakini kabla haamaliza alikatisha na sauti za wabunge wakipiga kelele  wakimtaka kutomzungumzia Nyalandu.

Mwenyekiti wa Bunge,  Mussa Zungu alilazimika kuwanyamazisha na kuwataka kuwa wavumilivu.

“Jamani tulieni, ebu tulieni, wewe, mimi ndiye ninayecontrol kiti, wewe Haonga, Haonga kaa kimya, kaa kimya, huwezi kubishana na kiti.

“Kama kuna kasoro kwa mtoa hoja mimi ndiye nitarekebisha siyo wewe, kaa kimya, tulia, itapendeza ukitulia,” alisema Zungu na kumruhusu  Dk. Kigwangalla kuendelea kutoa maelezo.

Dk. Kigwangallah baada ya kuruhusiwa alisema: “Mwenyekiti unajua ukiwa unaishi kwenye nyumba ya vioo usianzishe vita ya mawe, kuna wengine kwa wale mliokuja wapya mnatakiwa mjifunze mazingira ya humu ndani, kuna watu  wanaguswa na kuna wengine hawaguswi.

“… mimi ni katika watu wasioguswa na huwa sipendi upuuzi hata siku moja, kwa hiyo mtu anasema nimeanza kazi kwa kufukua makaburi, sitaki kuwakumbusha yaliyotokea huko nyuma lakini naomba niwape uhakika tu mimi huwa sichezewi chezewi.

“Kwa kuwa wanasema nimeanza kazi hiyo kwa kufukua makaburi basi leo (jana)  nafukua moja na  naanza kufukua hilo moja kwa maelezo yaliyotolewa na upinzani kwenye bunge lililopita ambako walisema Nyalandu kazi yake ni kustarehe kwenye hoteli za utalii, kutembea nchi za mbali ikiwamo Marekani na warembo.

“Sasa mwenyekiti leo (jana) naelewa kwamba kwa nini Nassari  alikuwa sahihi, kwa sababu wakati Waziri Nyalandu akistarehe kwenye Hoteli ya Serena pale Dar es Salaam akitumia helikopta ya mwekezaji wa Tanzania Game Tarackers Safaris (TGTS), mezani kwake…

“Wakati Nyalandu akivinjari Serena ambako alikuwa akifanyia kazi zake za Maliasili na Utalii katika hoteli ile na akapewa chumba akawa anaishi pale, mezani kwake kulikuwa na tamko la serikali kuhusiana na tozo za ada za hoteli  za utalii kwa mahoteli ambayo yapo ndani ya mbuga ya Serengeti.

“Lakini waziri yule hakusaini hiyo hadi anaondoka madarakani maana yake Nyalandu aliikosesha serikali mapato ya takribani Sh bilioni 32,” alisema.

Alisema jambo la pili  ni kuhusu uhusiano wa kutatanisha aliokuwa nao Nyalandu na wawekezaji wa taasisi maarufu ijulikanayo kama Freedking Foundation ambayo inamilikiwa na bilionea kutoka Marekani na pia   ina makampuni yanayofanya kazi za utalii   nchini hadi sasa.

“Moja inaitwa Mwiba Holding nyingine Tanzania Game Trackers  Safaris (TGTS), kampuni iliyopewa zaidi ya vitalu vitano, maana yake hapo kuna mambo hayako sawa , na bado kampuni hii ipo inafanya kazi kwenye sekta hii, ukisema nisifukue makaburi utakuwa unanionea.

“Ni lazima nijue kwa nini walipewa vitalu zaidi ya vitano, kwa nini wanaendelea kuwinda?” alisema.

Nyalandu  

Akijibu tuhuma hizo kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Nyalandu, alisema Dk. Kingwangalla ametumia muda wake ndani ya Bunge kumchafua kwa kusema uzushi na uongo dhidi yake.

Alisema kuchafuliwa kwake kunatokana na uamuzi wake wa kukihama CCM kutokana na mkakati wa kuhakikisha  hakuna kiongozi yeyote atakayethubutu ama kudiriki tena kukihama chama hicho tawala katika Serikali ya Awamu ya Tano.

“Waziri Kigwangalla anayasema hayo huku moyoni mwake akiwa anajua fika kuwa ametumwa kusema uongo dhidi ya Waziri Nyalandu kwa lengo la kuandaa mazingira ya kumkamata na kubwa zaidi, kudhalilisha azma ya Watanzania ambao wako tayari kwa mabadiliko ya uongozi wa nchi kupitia upinzani.

“Amekejeli kuwa Waziri Nyalandu alitumia fedha za Serikali kusafiri USA (Marekani) na mwanadada Aunt Ezekiel. Habari hii ilikuwa ya kuzusha na ilichunguzwa na vyombo vya dola mwaka 2014 na kuthibitika ilitungwa na ilikuwa ya uongo.

‘Katika mkutano huo wa Washington, DC, Waziri Nyalandu alialikwa na Balozi wa Tanzania, Marekani na alipewa ruhusa ya maandishi na Serikali kuhutubia mkutano huo kwa siku moja.

“Wasanii wote walioalikwa  akiwepo mwanadada Aunt Ezekiel, hawakuwa na mwaliko wa wizara ama Serikali, bali waandaji wa kongamano hilo,” alisema Nyalandu.

Alisema Waziri Kingwangalla angetakuwa kuwa na busara na angepaswa kujiridhisha na taarifa kabla ya kuisoma bungeni, ama waliomtuma walimwambia aisome tu hivyo hivyo.

“Na hata nilipoomba kuteuliwa kuwania urais nilitumia usafiri wa magari na ndege za kawaida kwa kulipa nauli, hadi mchakato ulipoisha,” alisema Nyalandu.

Alisema hata alipokuwa waziri aliweza kuipatia Serikali helkopta mpya na ndege kwa ajili ya matumizi ya kupambana na ujangili kwa kuishawishi Benki ya Dunia,   Ujerumani na Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles