25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

VIJANA 113 WAJITOKEZA KUMRITHI SADIFA UVCCM  

Na AGATHA CHARLES – dar es salaam


VIJANA 113 wamechukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ili kumrithi mwenyekiti anayemaliza muda wake, Sadifa Juma Khamis.

Hayo yameelezwa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.

Pia alisema vijana wengine 237 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo wa ndani ya chama kitaifa.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM inayoshikiliwa na Mboni Mhita, Shaka alisema wamejitokeza vijana 24.

“Katika nafasi tano za wajumbe wa Halmashauri Kuu wamejitokeza 103 kuchukua fomu, nafasi tano za wajumbe wa Baraza Kuu Taifa wamejitokeza waombaji 81, nafasi moja ya wawakilishi (Umoja wa Wanawake) UWT wameomba watu 14 na nafasi moja ya uwakilishi wazazi wameomba 15,” alisema.

Shaka alisema maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wilaya hadi Taifa yanaendelea vyema na uchaguzi wote wa ndani ya UVCCM unatarajiwa kukamilika Novemba.

Alisema mchakato wa uchaguzi huo ulianza tangu Aprili, mwaka huu ndani ya jumuiya za chama na kwamba kutokana na mabadiliko ya kanuni ya UVCCM yaliyofanyika Machi, mwaka huu uchaguzi ulianzia ngazi za matawi.

Shaka alisema hadi jana jumla ya matawi 23,529 sawa na asilimia 99.4 kati ya matawi 23,670 sawa na 0.59 yalikamilisha uchaguzi.

Katika ngazi ya kata, alisema matawi 3,913 sawa na asilimia 96.59 kati ya kata 4,051 sawa na asilimia 3.4 pia yalikamilisha uchaguzi.

“Kwa upande wa Zanzibar, majimbo 54 sawa na asilimia 100, wamekamilisha uchaguzi,” alisema.

Shaka alisema katika ngazi ya wilaya na mkoa, mchakato wa uchujaji majina kwa walioomba nafasi ulianza na kwamba jumla ya vijana 7,606 walijitokeza kuchuka fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika umoja huo.

Alisema licha ya wasifu wa kila mgombea kuandikwa katika kitabu maalumu watakachopatiwa wajumbe wa mkutano mkuu siku ya uchaguzi husika, lakini pia watapata nafasi ya kujieleza baada ya taratibu za vikao vya uteuzi kukamilika.

Pia alionya kuwa ni mwiko kwa mgombea kuanza kampeni kabla ya muda au wapambe wake kufanya ushabiki wa kisiasa kumnadi, kumpigia debe au kujipitisha kuelezea nafasi anayogombea.

“Tunaendelea kuwasisitiza kuwa ni marufuku na hairuhusiwi kabisa walioomba nafasi mbalimbali kuanza kufanya kampeni za kihuni, kutumia lugha chafu, siasa za maji taka kuchafuana, matusi, dharau kinyume na ubinadamu,” alisema.

Shaka alisema mambo hayo yakiachwa yanaweza kuzaa utoaji wa rushwa na aliomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia nyendo za wagombea.

“Tunaendelea kuviomba vyombo vinavyohusika katika ngazi zote, hasa Takukuru kuendelea kufuatilia kwa karibu nyendo za wagombea na wapigakura ili kubaini, kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Mgombea au mpigakura yeyote atakayethibitika kutoa au kupokea rushwa, hatua za kimaadili na kisheria tunaelekeza zichukuliwe ili kulinda heshima ya taasisi yetu,” alisema.

Pia alisema uchaguzi wa UVCCM katika ngazi zilizobakia utafanyika kwa misingi ile ile ya uhuru na uwazi, huku kila mgombea akipitishwa na vikao vya kikanuni na kikatiba baada ya kukidhi masharti ya uchaguzi kwa mujibu kanuni na katiba.

Shaka alisema hivi karibuni kumekuwa na malumbano yenye kupandikiza chuki na mifarakano na kuchafuana kupitia mitandao ya kijamii kinyume na misingi na maadili ya CCM.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles