27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

LEMA AHOJIWA KWA SAA TATU KUWAITA MA-DC WAPUMBAVU

Na JANETH MUSHI-ARUSHA


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amehojiwa na Jeshi la Polisi kwa saa tatu kwa tuhuma za kuwaita Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga kuwa ni wapumbavu na wajinga.

Lema alihojiwa jana katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa kuanzia saa saba mchana hadi saa 10 jioni kabla ya kuachiwa  baada ya katibu wake, Innocent Kisanyage, kumdhamini.

Lema anadaiwa kutoa maneno hayo katika mikutano yake ya hadhara iliyofanyika hivi karibuni jijini hapa, huku akidai kuwa walichokifanya wakuu hao wa wilaya ni kinyume na ubinadamu na wanamvunjia heshima Rais Dk. John Magufuli aliyewateua.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa, Lema alisema polisi wamemweleza kuwa katika baadhi ya mikutano yake alitoa kauli zinazowalenga wakuu hao.

Hivi karibuni, Byanakwa aliagiza kukamatwa na kuwekwa ndani mmoja wa walimu wilayani humo kwa kushindwa kutaja majina yake, huku akimwamuru kupiga push-up.

Naye Odunga alidaiwa kumchapa mzazi baada ya mtoto wake kurusha jiwe katika gari lake.

Lema alidai kuwa vitendo hivyo haviendani na hadhi ya vyeo vya ukuu wa wilaya walivyonavyo.

“Nilisema kweli kwa sababu matendo waliyofanya ni ya kipumbavu na kijinga

na nilimshauri Rais Magufuli awafute kazi mara moja kwa matendo ya kijinga na kipumbavu waliyofanya, kwani vitendo hivyo vinafanya utendaji wake uwe na kasoro na kufifisha juhudi zake katika mambo ya msingi ya nchi,” alisema Lema na kuongeza:

“Matendo hayo ni ya kinyama, udhalilishaji, hayana lugha nyingine ya kukemea zaidi ya kuyaita ya kipumbavu na ya kijinga, wamenipa dhamana leo (jana) na nimetakiwa kuripoti polisi Septemba 19, mwaka huu.”

Lema alisema kuwa taifa liendako, Magufuli atakuja kubaini baadhi ya watendaji wake hawamsaidii katika kutekeleza majukumu yao na badala yake wanazidi kumharibia kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, hakupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokewa.

Lakini mmoja wa askari ambaye hakutaka kutaja jina lake, alithibitisha Lema kuhojiwa na polisi wanaendelea kuchunguza kauli hizo

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles