29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo Wizara ya Mambo ya Ndani wapishana Takukuru

Ramadhan Hassan -Dodoma

SIKU nane tangu Rais Dk. John Magufuli awatumbue vigogo wa Wizara ya Mambo ya Ndani, zimeonekana kuwa ngumu zaidi kwa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola baada ya jana tena kuhojiwa kwa saa tano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini Dodoma.

Mbali na Lugola wengine waliohojiwa kwa kupishana muda ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Thobias Andengenye.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ramadhan Kailima licha ya kwamba hawajatumbuliwa lakini taarifa zinaeleza kuwa nao watahojiwa leo kuanzia saa tatu asubuhi.

Tofauti na vigogo hao wengine waliotumbuliwa pamoja na Lugola, mbunge huyo wa Mwibara kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiye anayeonekana hadi sasa kukaliwa kooni zaidi si tu na serikali bali pia Bunge na chama chake cha CCM ambacho kimemtaka ajieleze namna alivyodhalilisha nafasi aliyopewa na Rais Magufuli.

Lugola na wenzake wanahojiwa kwa agizo la Rais Magufuli mwenyewe  kutokana na kashfa ya watendaji wa wizara hiyo kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408 (sawa na Sh trilioni moja) kutoka kampuni moja nje ya nchi bila kufuata sheria.

ATINGA NA ILANI YA CCM TAKUKURU

Lugola alifika Makao Makuu ya Takukuru Jijini Dodoma jana mapema saa 1.24 asubuhi huku akiwa meshika begi dogo lililoashiria kuwa na nyaraka kadhaa pamoja ilani ya CCM ambapo aliingia kupitia geti kuu akitembea kwa miguu.

Baada ya kufika mlangoni aliwasalimia baadhi ya waandishi walioweka kambi katika ofisi hizo kwa bashasha akisema; “hamjambo, hamjambo, hamjambo wote,”

Lugola alikaribishwa na wafanyakazi wa Takukuru na kisha kuingia moja kwa moja ndani.

MTANZANIA Jumamosi ambalo liliweka kambi katika Ofisi ya Takukuru zilizopo jirani na Uwanja wa Jamhuri lilishuhudia Lugola akitoka ndani ya ofisi hizo saa 12.38 mchana.

Mara baada ya kutoka maofisa wa Takukuru walimvua kitambulisho alichokuwa amekivaa na kisha kumuelekezwa sehemu lilikuwepo gari lake lenye namba T 657 DFL Land Cruiser GX  V8.

Tofauti na wakati akiingia ambapo alishushwa nje ya geti na kisha akatembea kwa miguu, safari hii gari hilo lilimfuata hadi mlangoni mwa ofisi hizo.

Wakati akielekea kwenye gari aliwasalimia Waandishi wa Habari  ambao walikuwa wakimfuata.

Lugola; Habari zenu

Waandishi: Salama, Salama mkuu

Lugola: mpo?

Waandishi:tupo

Lugola: eeh.

Pamoja na kwamba waandishi walimtaka Lugola kusema chochote (ingawa kanuni haziruhusu kuripoti) hata hivyo hakuzungumza zaidi ya kuingia katika gari lake na kisha kuwauliza iwapo picha walizokuwa wakimpiga zinatosha.

“Picha zinatosha?haya kwaherini,”alisema Lugola na kisha kuondoka.

KINGU

Kwa upande wake, Kingu aliingia katika viwanja vya Takukuru saa 4.44 asubuhi akiwa katika gari lenye namba za usajili STL 2763 Land Cruiser V8  huku amevaa shati la kitenge.

Baada ya kushuka kwenye gari alipokelewa na watumishi wa Takukuru na kisha kupelekwa ndani kwa ajili ya mahojiano.

Tofauti na Lugola mahojino ya Kingu na Takukuru yalidumu kwa saa nne kwani alitoka saa  8.33 mchana.

ANDENGENYE

Aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Thobias Andengenye yeye aliingia Makao Makuu ya Takukuru saa 1.47 mchana.

Kama ilivyo  kwa wengine waliotangulia naye alipokewa na mtumishi wa Takukuru akiwa ameshika begi la mkononi na kisha  kuingia moja kwa moja Ofsini kwa ajili ya mahojiano.

Mahojiano kati ya Andengenye na maofisa wa Takukuru yalidumu kwa takribani saa tano ambapo alitoka katika ofisi hizo saa…

Januari 23 mwaka huu, wakati Rais Dk. John Magufuli akizindua nyumba za makazi ya askari Magereza, Ukonga, Dar es Salaam, alitengua uteuzi wa Lugola na Andengenye huku Kingu ambaye aliomba kujiuzulu akimteua kuwa balozi.

Rais Magufuli pamoja na kuwaondoa viongozi hao kwa kashfa ya kusaini mkataba huo tata alifichua jinsi wizara ya mambo ya ndani inavyomtesa.

“ Kama kuna wizara inanitesa ni Wizara ya Mambo ya Ndani, nataka muelewe inanitesa sana.

“Tangu tumeingia madarakani, kuna tume nyingi zimeundwa kuchunguza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa miradi ya ovyo iliyokuwa ikifanyika, na mimi nilitegemea watu watakuwa wanajifunza.

“Kulikuwa na mkataba wa ovyo unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408.

“Umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wa Tanzania walipokuwa wanakwenda kwenye majadiliano wanalipwa ‘seating allowance’ (posho ya vikao) ya Dola 800 (Sh 1,832,170) na hata tiketi za ndege walilipiwa.

“Yanayokwenda kununuliwa kule kwenye mkataba ni ya ovyo, ni ya ajabu, ukitaka kuuvunja, yale ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema maofisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wajitafakari.

Maofisa hao wanadaiwa kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Andelardus Kilangi alipofiwa na mkewe.

LUGOLA ALIVYOKALIWA KOONI

Siku moja kabla ya kuitwa Takukuru kuhojiwa baadhi ya wabunge wameonekana kumkalia kooni Lugola kutokana na kauli zake alizotoa bungeni wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipokuwa akijibu hoja za Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mkataba tata wa ununuzi wa sare za polisi.

Wakati huo, alidai kwamba atavua nguo iwapo itaonekana kwamba hakuna sare za Jeshi la Polisi zilizonunuliwa kama ambavyo ripoti ya CAG iliainisha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Nagwenjwa Kaboyoka akihitimisha kwa kujibu hoja mbalimbali za wabunge mara baada ya asubuhi kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa mwaka 2019, ndipo alipoibua suala la Lugola.  

 “Tunataka kumtoa Mheshimiwa Rais asionekane ana ‘Double Standard’. Mimi nilikuwa nimesafiri, nilikuwa South Africa, nikapata taarifa kwamba wenzangu wameteuliwa Mambo ya Nje pamoja na Ulinzi na Usalama na wachache wa kamati yangu kwenda kuangalia zile sare za polisi (zilizoainishwa kwenye ripoti ya CAG).

“Wakati huo Mheshimiwa Zungu (Musa) ndio alikuwa Mwenyekiti wa Kamati hii (Ulinzi na Usalama), nikamwambia Zungu naenda kama nani na nikamwambia mimi kama naenda kukagua na kamati yangu ina maana tumekaa na CAG tumepitia zile nyaraka zote zilizotakiwa.

“Maana suala la CAG halikuwa tukazione ‘uniform’ (sare) kwa macho, ilikuwa tunaangalia namna ‘uniform’ zile zilivyonunuliwa. Je, huyo aliyepewa tenda alipatikanaje? ‘Uniform’ zililetwa kutoka wapi? Kiasi cha fedha ni ngapi? Baada ya hapo ndio CAG aende stoo akaangalie kuna nini.

“Kutokana na zile ripoti, aone ‘uniform’ ziliagizwa 100 je, zimekuja 100, viatu viliagizwa 10 je, vimekuja 10, kinyume cha hapo CAG hawezi kutoka akaangalie kitu ambacho hajui anaangalia nini.

“Kwa hiyo kulikuwa na ‘disconcertion’ ambayo mheshimiwa Kangi Lugola ‘ali-mislead’ Bunge kusema atavua nguo kama ‘uniform’ hazipo, ina maana hasomi hata taratibu,” alisema Kaboyoka.

Wakati Kaboyoka akiendelea kuzungumza, Naibu Spika Tulia Ackson aliyekuwa akiongoza kikao hicho, alimkatiza kwa kile alichodai kuwa anakwenda nje ya utaratibu.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alitumia fursa hiyo kuomba utaratibu akilitaka Bunge liunde kamati teule ya kushughulikia ufisadi katika sare za Polisi.

Mdee alisema; “katika taarifa ya PAC imeonyesha ni namna gani kuna mgawanyiko kwenye hoja zinazohusiana na masuala ya kifisadi, mfano Jeshi la Polisi pale ambapo kamati inatoa taarifa uchunguzi ufanyike Serikali wamekuwa ni wazito kufanya uchunguzi.

“Hili limethibitishwa wakati Mwenyekiti wa PAC anaelezea mkataba wa E-Passport (paspoti za kielektroniki) na mradi wa ‘uniform’ za polisi, usanii uliofanywa na wizara, lakini ameonekana anazuiwa kuendelea wakati hoja ilizungumzwa kwa upana na Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa).

“Sasa kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kuunda kamati teule pale kunapokuwa na utata na kwa kuwa Kamati ya Bunge imeonyesha kuna shida, ninaomba nitoe taarifa hii ili nifanye ombi la kuomba niandike ombi hili kimaandishi ili Bunge liunde kamati teule kisha tufukunyue huu ufisadi unaofichwa, Mheshimiwa Naibu Spika nadhani umenielewa.”

Akijimjibu Mdee, Naibu Spika alisema hawezi kuruhusu kuundwa kamati teule kwa sababu ni lazima jambo hilo liwe limefika kwa utaratibu unaotakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles