30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Serikali, ubalozi watoa neno katazo la Marekani

Nora Damian -Dar es Salaam

SERIKALI imesema haijapata taarifa rasmi kutoka kwa Serikali ya Marekani juu ya kumzuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuingia nchini humo na kuzuia Watanzania kushiriki bahati nasibu ya kupata kibali (visa) cha kuingia nchini humo.

Juzi Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ilitangaza kumzuia Makonda kuingia nchini humo kwa madai ya ukandamizaji wa haki za binadamu.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela, alisema mpaka sasa hawajapata taarifa rasmi.

“There is no document’ hivyo, Serikali haiwezi kutoa kauli kwa mambo yanayozungumza kwenye mitandao,” alisema Buhoela.

Gazeti hili pia lilifanya juhudi za kuwatafuta viongozi mbalimbali wa Serikali kuzungumzia suala hilo bila mafanikio ambapo simu ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na Naibu wake Dk Damas Ndumbaro, zilikuwa zikita bila kupokelewa.

MTANZANIA Jumapili lilipojaribu kuwasiliana na Ubalozi wa Marekani Tanzania kujua iwapo ulipeleka taarifa rasmi serikalini, ulisema hawana cha kuongezea na kwamba taarifa hiyo inabaki kama ilivyo.

“Taarifa hiyo imetoka Washington, kama ubalozi hatuwezi kusema kitu chochote… inabaki kama ilivyo,” alisema ofisa mmoja alipozungumza na gazeti hili.

TUHUMA ZA MAKONDA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo, alitangaza marufuku hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter. Marufuku hiyo pia inamhusisha mke wa Makonda, Mary Massenge.

Marekani ilidai kuwa Makonda ameshiriki katika ukandamizaji wa haki za binadamu, kuwanyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wao.

“Leo tumetangaza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, kuwa hataruhusiwa kuingia Marekani kwa kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya kuporomoka kwa heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania,” alisema Pompeo.

Pia taarifa ya wizara hiyo ilidai kumekuwa na matendo ya viongozi yanayokandamiza uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika kwa amani, kukandamiza makundi yasiyo na sauti na upinzani wa kisiasa na kutishia maisha.

“Tunaitaka Serikali ya Tanzania kuheshimu haki za binadamu na za msingi kama uhuru wa kujieleza na mikusanyiko ya amani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

KATAZO LA VIZA

Katazo la visa linazihusu nchi za Tanzania, Nigeria, Myanmar, Eritrea, Sudan na Kyrgyzstan.

Kulingana na katazo hilo, marais wa Nigeria na Eritrea wamepigwa marufuku kabisa kuomba visa za kuhamia Marekani. Hivyo raia wa nchi hizo ambao watataka kuingia Marekani kwa kutalii ama biashara wataruhusiwa.

Marekani ilidai uamuzi huo unatokana na nchi hizo kutotaka au kushindwa kuheshimu aina fulani ya usimamizi wa utambulisho wa kimsingi, kubadilishana taarifa na vigezo vya uchunguzi wa usalama wa taifa na usalama wa raia ambavyo vilianzishwa na wizara hiyo mwaka wa 2017.

Bahati nasibu hiyo hutoa visa kwa watu takribani 50,000 kutoka nchi zenye kasi ndogo ya maendeleo kila mwaka kuingia na kufanya kazi Marekani.

Taifa la Belarus ambalo lilitajwa katika rasimu ya awali ndilo ambalo halijaorodheshwa katika taarifa za juzi.

Ofisa wa ngazi ya juu wa Marekani alisema nchi hizo sita zimeshindwa kufikia ‘kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa’.

“Nchi hizi, kwa sehemu kubwa, zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbalimbali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka,” Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Chad Wolf, aliwaambia waandishi wa habari.

Wolf alisema maofisa wa Marekani watakuwa tayari kushirikiana na nchi hizo sita ili kuimarisha matakwa ya ulinzi waweze kutoka kwenye vikwazo hivyo.

Nchi hizo mpya zinaungana na nchi nyingine saba ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani tangu mwaka 2017.

Nchi hizo nyingi zikiwa na raia wengi Waislamu ni Libya, Iran, Somalia, Syria, Yemen.

Kwenye orodha hiyo pia zimo Korea Kaskazini na Venezuela.

MARUFUKU ZILIANZA 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump alianzisha marufuku kwa baadhi ya raia wa mataifa ya kigeni kuingia Marekani mwaka 2017 ambapo alisaini katazo la kwanza la aina hiyo kwa nchi za Iran, Iraq, Syria, Yemen, Libya, Somalia, Chad, Venezuela na Korea Kaskazini.

Katazo hilo lilipingwa vikali hususani kwa kuzilenga zaidi nchi zenye Waislamu wengi. Awali katazo hilo lilipingwa kwa amri ya mahakama kabla ya Mahakama ya Upeo ya Marekani kukubaliana na hoja za upande wa Trump mwaka 2018.

Kwa upande wa Venezuela marufuku hiyo inawalenga viongozi wa Serikali ya Rais Nicolas Maduro ambayo Marekani haiitambui.

Hata hivyo nchi za Iraq na Chad kwa sasa zimeondolewa kwenye zuio hilo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles