23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO WATANO WATUMBULIWA NHC

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SIKU chache baada ya Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kusimamishwa kazi, wakurugenzi wengine watano wa shirika hilo, nao wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi.

Mbali na hao, pia wafanyakazi wote wa ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC na wahudumu nao wamesimamishwa.

Wakati hayo yanafanyika, Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, imemteua Felix Maagi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa NHC.

Taarifa za ndani ambazo MTANZANIA imezipata, zilieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa jana katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wake Blandina Nyoni.

Waliosimamishwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Ubunifu, Issack Peter na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, James Rhombo.

Wengine ni Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara, David Shambwe, Mkurugenzi wa Utawala na Huduma za Mikoa, Raymond Mdolwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Milki, Hamad Abdallah.

MTANZANIA lilipomtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika, alisema wenye mamlaka ya nidhamu ya NHC ni bodi ya shirika hilo, hivyo atafutwe mwenyekiti wake.

“Wenye mamlaka ya nidhamu ya NHC ni bodi, hivyo mtafute mwenyekiti wake,” alisema Mwanyika.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Bodi, Blandina, simu yake iliita bila kupokewa na baada ya kupigiwa tena haikupatikana hewani na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu pia haukujibiwa.

Hata hivyo, alipotafutwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi naye simu yake haikupatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu hadi gazeti linakwenda mitamboni.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Lukuvi, alimsimamisha Mchechu ili kupisha uchunguzi.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, ilieleza kuwa Lukuvi alichukua uamuzi huo kutokana na mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.

Ingawa taarifa hiyo haikuzitaja tuhuma zinazomkabili Mchechu, lakini katikati ya wiki iliyopita wakati Rais Dk. John Magufuli akizindua nyumba mpya 150 za makazi zilizojengwa na NHC eneo la Iyumbu nje kidogo ya mji wa Dodoma, alimshushia tuhuma nzito Mchechu na shirika analoliongoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles