*Mzee Wasira ampigia hodi kwa Shaka…
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Waziri wa zamani, Mzee Stephen Wasira amekutana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya (CCM) Lumumba jijini Dar es Salaam.
Mzee Wasira na Shaka wamezungumza kwa undani masuala kadhaa muhimu yanayohusu idara ya Itikadi na Uenezi. Pia Mwanasiasa huyo ameitaja idara ya itikadi na uenezi akisema ingekuwa ni vitani, idara yake ndicho kikosi kinachotakiwa kwenda mstari wa mbele katika uwanja wa vita kukabili mapambano ya kisiasa.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumanne Mei 25, 2021, Mzee Wasira amemueleza Shaka kuwa, kuna baadhi ya vyama na wanasiasa wanaamini idara hiyo inamhitaji Mwanasiasa mzumgumzaji anayepepeta maneno na kusahau kuwa huo ndiyo mdomo, moyo na sikio la chama ndani ya umma .
Mzee Wasira amesema mantiki ya idara hiyo si kuwa msemaji peke yake wa chama bali pia ni idara nyeti inayomhitaji mwanasiasa anayetosha kuizumgumzia, kuielezea na kuifafanua siasa, sera na itikadi ya chama.
Amesema ameupongeza uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake makini wa kumteua Katibu Mkuu mpya kijana anayetokana na CCM, Daniel Chongolo na kumteua Shaka kuwa Katibu wa Idara muhimu ya itikadi na uenezi.
Pia, amesema kuwa wajumbe wengine wa Sekreterieti wanatosha kwani miongoni mwao wapo wazoefu, viongozi mahiri na wengine mashuhuri mno waliowahi kuhimili purukushani na mikiki ya kisiasa.
“Umefanya kazi nzuri sana ukiwa Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar na baadae Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa. Ulichapakazi ya kijasiri ukijibu mapigo ya upinzani kwa wakati na kwa nguvu ya hoja. Umekuwa ukipangua hoja kwa mirejesho ya kisiasa, kihistoria aidha ya TANU au ya ASP,” amesema Mzee Wasira.
Aidha, amemtaka Shaka aendelee kuchapakazi na kuvipitia vitabu, matoleo na machapisho ya chama yalioandikwa na wanasiasa na wana historia mbalimbali kwani ndiyo yatakayomzidishia ufahamu wake na ukomavu wa kisiasa pamoja na utendaji mzuri na kwamba ataacha kumbukumbu isiyosahaulika.
Kwa upande wake Shaka amemhakikishia Mzee Wasira kupokea ushauri wake wa busara na kumpa moyo katika juhudi za kutimiza wajibu wake akiwa katika idara ya itikadi na uenezi akisimamia uhai wa Chama na kupigania maslahi mapana ya CCM.
Shaka amelisema yote ambayo amekuwa akiyajibu, kuyasema na kutetea chama huwa si maneno yanayotoka moja kwa moja mdomoni mwake bali huwa tayari ameyadurusu kitambo toka kwenye vitabu vya kumbukumbu muhimu za kisiasa, sera, dira na kujua chama kilipotoka, kilipo na kinakotaka kuelekea.
Hata hivyo Katibu huyo wa itikadi na uenezi alimueleza Mzee Wasira akisema wanasiasa mahiri na mashuhuri sana duniani wamejifunza, kuelekezwa hatimaye wakafahanu na kuwe weledi toka kwa wanasiasa waliowatangulia kwani hata walimu nao wana wakufunzi wao.