JANETH MUSHI-ARUSHA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, inawashikilia watu tisa, wakiwemo viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM kwa tuhuma mbalimbali za rushwa.
Miongoni mwa wanaoshikiliwa, ni pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), watumishi na wafanyabiashara mbalimbali.
Waliokamatwa ni Mjumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Arusha, Sifael Pallangyo, Katibu wa Malezi Wilaya ya Longido na Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Arusha, Upendo Ndoros, Katibu wa Wazazi Wilaya ya Longido na Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Arusha, Laraposho Laizer.
Wengine ni Katibu wa wazazi Kata ya Kikatiti, Meru, Godwait Mungure, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Tukusi wilayani Monduli, Mboiyo Mollel, Mwenyekiti wa Kamati ya pembejeo Kijiji cha Loita Kata ya Nkoanrua, Kanankira Nnyary, wafanyabiashara wa Kata ya Olturmet, Gervas Mollel na Joseph Mollel.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge, alisema tukio la kwanza lilitokea Juni 26, mwaka huu.
Alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema, kuwa Lilian Ntiro ambaye anatarajia kugombea ubunge wa viti maalumu (Wazazi) Mkoa wa Arusha alikuwa akifanya siasa ambazo hazikuwa sahihi.
Alisema mtuhumiwa anadaiwa kumpatia Pallangyo fedha kwa ajili ya kwenda kuwahonga wajumbe wa Baraza la Wazazi Wilaya ya Longido kama kishawishi cha kumpigia kura katika kura za maoni zinazotarajia kufanyika hivi karibuni.
Alisema baada ya taarifa hiyo, taasisi hiyo kwa kushirikiana na ofisi yake Wilaya ya Longido, waliandaa mtego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kila mmoja akiwa na kiasi tofauti cha fedha zilizokuwa zimeandaliwa kugawiwa kwa wajumbe wa baraza hilo.
“Pallangyo alikutwa na shilingi milioni 14, Upendo shilingi 552,000 pamoja na simu aina ya Irtel smart ambapo kulikuwa na mawasilianao na watuhumiwa wenzake, Laraposho alikuwa na shilingi 117,000, simu aina ya Samsung Galaxy ambapo kulikuwa na mawasiliano na watuhumiwa wenzake.
“Mungure alikuwa na simu ndogo ikiwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Pallangyo,” alisema
Alisema uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea ambapo watuhumiwa wote wako mahabusu tangu Juni 26, mwaka huu, huku wakitarajiwa kupewa dhamana jana.
Alisema taasisi yake inaendelea kumshikilia mtia nia (Lilian) kwa mahojiano.
WAJIPATIA MILIONI 15/-
Pia taasisi hiyo, inawashikilia Gervas Mollel na Joseph Mollel ambao ni wafanyabiashara wa Olturmet kwa kujipatia Sh milioni 15 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mfanyabiashara mwenzao, Advera Kyarunzi mkazi wa Mto wa Mbu wilayani Monduli.
Alisema awali ilielezwa wafanyabiashara hao, wote walikuwa wakishirikiana kusafirisha mbegu za vitunguu kutoka Tanzania kwenda Uganda, ambapo Septemba 2018 baada ya kupakia mzigo ukiwemo wa Advera uliokuwa wa Sh milioni 15, walikubaliana Advera, Gervas Andrea na Haruna Kitundu, watangulie kwa basi kwenda mpaka Murongo ambako wangekutana na Mollel ambaye alikuwa dereva wa gari aina ya Fuso yenye namba T 449 ATT.
“Gervas alisema anaumwa tumbo, atampatia Advera kijana mwingine wa kuvuka naye mpakani, Advera alipojaribu kuwasiliana na Christopher ikawa hapatikani kwenye simu na hakuweza kumuona tena wala kupata mzigo, aliendelea kufuatilia fedha zake bila mafanikio, watuhumiwa tunaendelea kuwahoji,” alisema
PEMBEJEO ZA RUZUKU
Katika tukio la tatu,alisema taasisi hiyo imewakamata Mboiyo Mollel, Mikidadi Mollel na Kanankira kwa kosa la kughushi vocha za pembejeo za kilimo za ruzuku ambazo walitakiwa kuzigawa Kijiji cha Tukusi wilayani Monduli, mwaka 2016.
Alisema watuhumiwa walipaswa kugawa mbegu za mahindi, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia kwa wakulima,wao waligawa mbegu tu na baadaye katika vocha wakaonyesha wamegawa vitu vyote wakati siyo kweli, ambapo uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
KIZIMBANI RUSHWA
Wakati huo huo, taasisi hiyo imemfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olmotony, Daniel Luka kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh 70,000 kutoka kwa Nai Mollel mkazi wa kitongoji hicho ili asimchukulie hatua, baada ya kubaini alikuwa amejiuanganisha maji ya kijiji kinyume na taratibu.
Alisema mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani Juni 26, mwaka huu ambapo awali Juni 21,mwaka huu, Nai alifika ofisi hiyo ya mwenyekiti kutaka kujua utaratibu wa kuunganishwa maji ambapo alimtaka kuandika barua na kuambatanisha na ‘Chai’, kwa maana ya fedha.
“Baadaye mwenyekiti alimweleza iwapo anataka jambo hilo liishe aandike barua ya maombi na fedha Sh 100,000 na kumpelekea. Taarifa ilipelekea kuandaliwa mtego wa rushwa ya Sh 70,000 na kufanikiwa kumkamata Juni 25, mwaka huu,” alisema
Alisema taasisi hiyo inaonyesha wale wote watakaoanza kuwarubuni wapiga kura kwa rushwa na kufanya kampeni kabla ya muda kwamba vitendo hivyo wanavyofanya ni kinyume na sheria na wakibainika watachukuliwa hatua kali.
“Takukuru inahamaisha wananchi kuendela kutoa taarifa hasa kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu na kutoa taarifa za wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye taasisi za Serikali na maeneo mengine,” alisema.
Katika hatua nyingine, taasisi hiyo Mkoa wa Singida inatarajia kuwafikisha mahakamani Hakimu wa Mahakama ya Mwanza, Kilimatinde Bahati manongi na mzazi mwenzake Haji Bwegege ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.
Manongi anadaiwa kuomba rushwa y ash 350,000 ili atoe upendeleo kwa mtoa taarifa kwenye shauri la madai namba 03/2020.
Juni 28, mwaka huu, taasisi hiyo ilimkamata bwegewe maeneo ya stendi akipokea sh 170,000 ya kiasi alichoomba.