Chadema yatoa ratiba wataka urais, ubunge, udiwani

0
554

 MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba ya uchukuaji fomu za kugombea urais, ubunge na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akitangaza ratiba hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi alisema zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ya urais litafanyika kuanzia Julai 4 hadi Julai 19 mwaka huu. 

Munisi alisema wenye nia ya kugombea nafasi hiyo, wanapaswa kufika katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, kwa ajili ya kuchukua fomu, kisha kutafuta wadhamini 100 kwa kila kanda kumi za chama hicho. 

“Mchakato wa mgombea urais utakuwa wazi kuchukua fomu kuanzia Julai 4 mwaka huu, wenye nia ya kugombea ama wao au mawakala wao watafika makao makuu na kuchukua fomu kutoka ofisi ya katibu mkuu. 

“Julai 19 mwaka huu saa 10:00 jioni wagombea wawe wamekamilisha ujazaji fomu na udhamini walete kwa katibu mkuu,” alisema. 

Alisema wagombea wanatakiwa kutafuta wadhamini katika kanda zote za Chadema, ambazo ziko 10 lakini wadhamini hao wasiwe wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho. 

“Baada ya kuchukua fomu, watakuwa na muda wa kujaza na kuomba mdhamini, mgombea urais au wakala wake, baada ya kuchukua fomu, ataenda kutafuta wadhamini kwenye kanda zetu zote kumi. Kila mgombea kwenye kila kanda apate wadhamini wasiopungua 100,”alisema Munisi. 

Alisema baada ya zoezi la uchukuaji na ujazaji fomu kukamilika, Julai 22 mwaka huu Katibu Mkuu wa Chadema, atawasilisha taarifa za watia nia mbele ya Kamati Kuu ili lipendekeze wanaofaa kuingia katika hatua inayofuata. 

Makada waliotangaza nia ya kugombea urais Chadema ni pamoja na Isaya Mwita, Tundu Lissu, Dk. Majinge Mayrose Kavura, Mnyama Leonard Toja, Freeman mbowe, Mchungaji Peter Msigwa, Mwanalyela Gasper Nicodemus, Nalo Opiyo, Neo Simba Richmund, Shaban Msafiri na Lazaro Nyalandu. 

Akizungumzia kuhusu wagombea ubunge, Munisi alisema zoezi hilo litaanza rasmi Julai 4 hadi 10 mwaka huu kwa wanaotaka kugombea kuchukua fomu ofisi za majimbo, kanda au mitandoni kisha kuzijaza na kuzirejesha ofisi ya jimbo analogombea. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here