24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Rais Magufuli: Tumeweza

LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema licha ya baadhi ya watu kubeza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa yenye uwezo wa kupitisha treni inayotumia umeme (SGR), sasa Tanzania imekwenda kuihakikishia dunia inaweza.

Kutokana na hali hiyo, alisema kwa mwaka Serikali ilikuwa ikitumia Sh bilioni 5 hadi 7 kwa ajili ya ukarabati wa reli hiyo ambapo sasa fedha hizo zitaelekezwa maeneo mengine ya miradi, baada ya kukamilika kwake.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Kilosa mkoani Morogoro, alipokuwa akizindua ujenzi wa mahandaki ya reli hiyo ambapo alisema ujenzi wake utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi wilayani humo, ikiwamo utalii.

Mahandaki hayo yenye urefu wa kilometa 2.7 yanajengwa kipande cha Morogoro-Makutupora, yanajengwa kuzuia miundombinu ya reli kusombwa na maji.

Dk. Magufuli alisema huenda mkandarasi aliyekuwa akifanya ukarabati huo, alikuwa na makubaliano ya ‘upigaji’ kati yake na Wizara ya Ujenzi.

Alisema aliposema anajenga reli ya kisasa inayotumia umeme baadhi ya watu walimwona kama anaota mchana, alimwamini Mungu na Watanzania hasa maskini waliokuwa pamoja na yeye na chama chake.

Alisema wananchi ni mashahidi kwa sababu ujenzi wa reli hiyo inayogharimu zaidi ya Sh trilioni 6.03 zinazotokana na Watanzania wenyewe jambo linalowafanya kutembea kifua mbele.

“Watanzania sisi siyo maskini ni cash inatoka hapa, ukishatoa cash hutajidai ndugu zangu? Ukitoa cash hujidai? Ndiyo maana ninawaopa Watanzania tutembee kifua mbele.

“Mradi huu ni wa historia, tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora- Dodoma na mradi kwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, umeshakamilika kwa asilimia 82 mpaka jana.

“Ndugu zangu nimekuja kuweka jiwe la msingi la handaki hili, siyo handaki la kawaida, Kilosa tunatengeneza ramani nyingine ya mahali ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali watakuja.

“Wapo watu watakuja na washikaji wao watakaa humu humu kwenye handaki, nasema uongo ukimleta mshikaji hapa atakukataa?alisema na kuhoji

Rais Dk. Magufuli, alisema ujenzi huo umefungua fursa nyingine ya utalii na kuwaasa wakazi wa wilaya hiyo kuitumia fursa kujiletea maendeleo zaidi kwa sababu watu wanakwenda hapo wanapeleka fedha.

“Muanze kutengeneza mianya ya kutengeneza pesa, mwenye uwezo wa kujenga hoteli ajenge,niwaombe maeneo ya reli yote na hii niiombe wizara ya ujenzi na wizara nyingine zinazohusika kwa kushirikiana na viongozi wa mkoa muanzishe korido za kiuchumi.

“Kama ni mashamba muanzishe mengi ya kutosha, mtalima matunda yatasafirishwa mpaka Ulaya wenye kufunga wafuge nyama zitasafirishwa na ndiyo maana nilimwagiza Waziri wa Ardhi na viongozi wa Mkoa wa Morogoro suala la migogoro ya ardhi lazima liishe.

“Ndiyo maana nikafabnya mabadiliko ya uongozi hapa nikamteua mkuu wa mkoa hapa, mtani wangu masai, yeye ni mfugaji, awatetee wakulima na wafugaji,” alisema Dk. Magufuli.

MIGOGORO YA ARDHI

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi, Rais Magufuli alisema mingi mkoani humo inasababishwa na mashamba kuchukuliwa na matajiri ambapo hadi sasa asa tayari wamefuta mashamba 49, huku akisubiri kufuta mengine 11 kabla ya Jumamosi wiki hii.

Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza viongozi wa serikali wilayani Kilosa na nyingine za mkoa huo kukaa na kuandaa utaratibu ili ardhi hiyo, igawiwe bure kwa wananchi maskini na si kuchukuliwa na wakubwa kwa sababu amepata habari hata baadhi ya viongozi wa serikali wanahusika na migogoro hiyo.

Aliwataka viongozi wa dini kusaidia kutatua migogoro hiyo kwa sababu hata vitabu vitakatifu vinasema heri walio wapatanishi watauona ufalme wa mbingu, suala hilo limekuwa likimkera.

Aliwaonya wasiwaonee watu ambao wanayaendeleza mashamba yao vizuri kwa sababu linaweza kutafusiriwa kama zoezi la kunyang’anya watu mashamba.

DED, DC WANYOSHEWA KIDOLE

Rais alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Asanjile Mwambale, kubadilika kwa sababu ana matatizo ikiwamo kuuza maeneo ya ardhi kwa wawekezaji. 

“Ajirekebishe, siwezi nikamtumbua mbele ya askofu, madhambi yake anayajua. Ameuza maeneo kule, kikao kikakaa siku hiyo hiyo na mkataba akasaini siku hiyo hiyo akauzia kampuni ya Wachina.

“Ninaambiwa yeye alisaini kwa shilingi milioni 225, ndizo akaziingiza kwenye akaunti kwa taarifa za pembeni ziliingizwa milioni 400. Niliagiza hospitali ya Dumila, yaliyokuwa majengo ya Tanroads yaanze ku-operate kama hospitali naambiwa inasuasua,” alisema Rais Magufuli

Licha ya hali hiyo, alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Adam Mgoyi, ajirekebishe kutokana na kasoro mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuwatetea wananchi badala yake anawazuia kuendesha kughuli zao katika mashamba yanayomilikiwa na wageni.

Pia alizungumzia ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambapo alisema kuna watu walipinga ujenzi wake lakini sasa umesaidia kupatikana kwa bilionea Ulininiu Laizer ambaye pengine asingepatikana au hata kuuawa kama ukuta huo usingejengwa.

KIMAMBA

Wakati akiendelea katika uzinduzi huo msafara wake, ulisimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Kimamba Wilaya Kilosa, ambapo walimwelekeza kero mbalimbali ikiwamo migorogo ya ardhi baina ya wananchi na mwekezaji wawekezaji.

Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuhakikisha anampelekea orodha ya mashamba 11 hadi ifikapo Jumamosi wiki hii ili hati zake zifutwe yatolewe bure kwa wananchi.

Alimwagiza Waziri Lukuvi, mkuu wa mkoa wa Morogoo na katibu tawala mkoa wa Morogoro na mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Kilosa kushughulikia matatizo ya ardhi katika wilaya hiyo ndani ya wiki moja kuanzia jana.

Pia Dk. Magufilu aliagiza kukamatwa na kufikisha mahakamani kwa Ofisa Maliasili wa wilaya hiyo, aliyetajwa kwa jina moja la Ndembo ambaye anadaiwa kuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi wilayani humo.

“Mnakodishiwa kwa sababu zile hati zimechukuliwa na wakubwa sasa mimi nataka nilale nao hawa wakubwa. Kwa hiyo nimesema siku saba waziri ataleta, pamoja na mkuu wa mkoa, atakuja na mwenyekiti na nitasaini mbele yako mwenyekiti uje uwaeleze,” alisema

Aidha aliwataka kutotumia ardhi itakayotolewa kama chanzo cha migogoro na kwamba ardhi hiyo itakuwa na maeneo ya wakulima na wafugaji.

Akiwa kijijini hapo, Dk. Magufuli alimnyooshea kidole Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilosa kwa kuwa sehemu ya migogoro ya ardhi wilayani humo, huku ekieleza kuwapo taarifa amemweka mkononi Waziri Lukuvi.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alihoji kuhusu mwekezaji raia wa China kupewa ardhi wakati utaratibu unawataka raia wa kigeni kupewa ardhi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tazania (TIC).

 KAULI YA KADOGOSA 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa alisema ujenzi wa kipande cha kwanza cha Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilometa 300 umefikia asilimia 8, huku kile cha Morogoro hadi Makutupora Dodoma ujenzi wake ukifikia asilimia 34.

Alisema mahandaki manne yaliyowekwa jiwe la msingi jana kwa pamoja yana urefu wa kilometa 2.7.

Alisema kutokana na reli ya zamani kupita kandokando ya mto kwa zaidi ya kilometa 120, jambo ambalo limekuwa likisababisha kutumika kwa fedha nyingi kutokana na reli kusombwa na maji na kwamba kwa ujenzi huo reli ya kisasa haitakumbwa na tatizo hilo.

Alisema ujenzi wa stesheni zote 16 za kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, umefikia asilimia 90, na kwa kipande cha pili wameanza ujenzi kati ya Mkata na Kilosa kwa asilimia 15.8.

Alisema ujezi wa daraja la juu la Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 2.56 umefikia asilimia 86 na madaraja mengine zaidi ya 100 kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora kipande cha kwanza ni zaidi ya asilimia 85 na kipande cha pili ni zaidi ya asilimia 32.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles