25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO MSD KORTINI KWA KUTUMIA MADARAKA VIBAYA

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


ALIYEKUWA Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani na Meneja Ununuzi, Fredrick Nicolaus wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Aneth Mavika akisaidiana na Leonard Swai alidai  kwamba washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Machi mosi mwaka 2013 na Machi 19 mwaka huo, Makao Makuu ya MSD wilayani Temeke.

Alidai washtakiwa wakiwa katika nafasi zao za kazi, kwa makusudi, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuandaa na kusaini mabadiliko ya mkataba namba moja wenye kumbukumbu namba MSD/003/Q/G/2010/2011/60 wa Machi 19 mwaka 2013.

Inadaiwa, kusaini mabadiliko hayo kulisababisha Kampuni ya H.H.Hillal kujipatia faida ya Sh 482,266,000.

Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upelelezi umekamilika na Jamhuri haikuwa na pingamizi kwa washtakiwa kupata dhamana.

Hakimu Mwijage alitoa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika  atakayesaini dhamana ya Sh milioni 20 na kuweka mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 200. Kesi iliahirishwa hadi Machi 21 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles