25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo Halotel waendelea kusota rumande kwa miezi mitatu

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

VIGOGO sita wa Kampuni ya Viettel Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46), wanaokabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya zaidi ya Sh bilioni 78, wanaendelea kusota rumande wakisubiri majibu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

Washtakiwa hao ambao kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani Machi 27 mwaka huu, jana walisomewa kesi yao kwa njia ya Mahakama Mtandao ambapo upande wa Jamhuri ulidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwamba upelelezi haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi haujakamilika na akaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Benedict Ishabakaki akijibu alidai waliandika barua kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kumaliza kesi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hivyo wanaendelea na mazungumzo na ofisi ya DPP.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja hizo, alisema mazungumzo yakikamilika kabla ya tarehe ya kutajwa tena Julai 22 mwaka huu washtakiwa wataletwa kwa hati ya wito.

Awali ilidaiwa kuwa washtakiwa hao  Aprili 21 mwaka huu waliandika barua kwa DPP kukiri makosa.

Barua hiyo inadaiwa ilipokewa, majadiliano yalianza na yalikamilika kwa kiasi kikubwa, kinachosubiriwa ni hati ya kuipa mamlaka Mahakama ya Kisutu kuendelea na shauri hilo kutoka kwa DPP.

Mbali na Nguyen washtakiwa wengine ni Nguyen Minh (40)  na Vu Tiep wote ni Mameneja wa Halotel, Ha Than (39) ambaye ni Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) Halotel, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel.

Awali waliposomewa mashtaka Machi 27 mwaka huu mbele  ya Hakimu Simba, washtakiwa hao walidaiwa  kati ya Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida.

Inadaiwa kati ya Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020  maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, kwa pamoja walitumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.

Pia inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.

Katika shtaka la nne, inadaiwa washtakiwa hao walikwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganishwa Viettel Tanzania na Vietnam  kinyume na sheria.

Inadaiwa Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo hayo kwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA walisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 75.

Pia wanadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh bilioni 3.03.

Katika shtaka la saba, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.

Kampuni ya Viettel Tanzania inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu ilitakatisha Sh bilioni 3.03 na shtaka la tisa na 10, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 75 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles