BADI MCHOMOLO NA MITANDAO
MICHUANO ya 31 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo inaendelea kutimua vumbi nchini Gabon, inatarajia kufikia tamati mwishoni mwa wiki hii baada ya miamba 16 kuoneshana ubora wa wachezaji wao.
Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi tangu Januari 14 mwaka huu, ambapo wenyeji Gabon walianza kutupa karata yao ya kwanza dhidi ya Guinea Bissau huku mchezo ukimalizika kwa sare ya 1-1, wakati mchezo wa pili ukiwakutanisha Burkina Faso dhidi ya Cameroon.
Katika michezo hiyo ya awali ilionesha kuwa na msisimko wa hali ya juu ambapo uwanja ulikusanya idadi kubwa ya mashabiki hasa mchezo wa kwanza wa ufunguzi, lakini siku zilivyozidi mashabiki walianza kupungua viwanjani.
Kati ya mataifa 16 ambayo yalikuwa yanashiriki katika michuano hiyo kuna vigogo wa barani Afrika bado walipewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kuwa na wachezaji ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya, lakini hali ilikuwa tofauti.
Baadhi ya timu ambazo zilipewa nafasi kubwa ya kufika mbali kwenye michuano hiyo ni pamoja na mabingwa watetezi Ivory Coast, Algeria, Senegal, Misri, Ghana, Cameroon, Zimbabwe pamoja na mataifa mengine, ila baadhi ya vigogo wameshangaza kutolewa mapema.
Ivory Coast
Timu hii ilikuwa ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambao walitwaa msimu uliopita timu hiyo ikinolewa na kocha wa sasa wa timu ya Taifa ya Morocco, Herve Renard, aliyeondoka baada ya kuwapa ubingwa.
Ivory Coast walipewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kuwa na wachezaji wengi ambao wana majina makubwa na kuzitumikia klabu ambazo zinashiriki ligi kuu mbalimbali barani Ulaya, lakini wachezaji hao walishindwa kuonesha ukubwa wa majina yao na klabu wanazotokea.
Baadhi ya wachezaji ambao walipewa nafasi kubwa ya kulibeba Taifa hilo kwenye Afcon ni pamoja na Eric Bailly, ambaye anakipiga katika klabu ya Manchester United ya nchini England, Wilfried Bony mshambuliaji wa klabu ya Stoke City, Wilfried Zaha mshambuliaji wa klabu ya Crystal Palace, Serge Aurier beki wa PSG, Franck Kessie, anayekipiga katika klabu ya Atalanta, Salomon Kalou wa Hertha BSC na wengine wengi.
Lakini pamoja na kikosi hicho kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa hivyo lakini walishindwa kuonesha ubora wao na hatimaye walitolewa mapema kwenye michuano hiyo hatua ya makundi, huku kundi lao likiwa na DR Congo, Morocco na Togo.
Ni jambo ambalo limewashangaza wengi kwa Taifa hilo kushindwa kuonesha ubingwa utetezi na kupambana angalau kufika hatua ya robo fainali. Hii inaonesha kuwa michuano hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu.
Algeria
Miongoni wa timu ambayo ilikuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa ni pamoja na Algeria, lakini walishindwa kuonesha uwezo wao na kujikuta wakitolewa katika hatua ya makundi kama ilivyo kwa mabingwa watetezi Ivory Coast.
Katika kikosi cha timu hii kulikuwa na wachezaji kama vile Riyad Mahrez, ambaye anakipiga katika klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City, pia mchezaji huyo baada ya kuipa ubingwa klabu yake alifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora nchini England, kabla ya kutwaa tuzo nyingine ya mchezaji bora wa Afrika katika tuzo za BBC.
Wachezaji wengine ambao walikuwa wanaunda kikosi hicho ni pamoja na Islam Slimani, ambaye anakipiga katika klabu hiyo ya Leicester City, Yacine Brahimi ambaye anakipiga katika klabu ya FC Porto pamoja na wachezaji wengine wengi.
Algeria wamekuwa wakifanya vizuri katika michuano mbalimbali hivyo walipewa nafasi kwenye michuano hii kuwa wanaweza kufanya makubwa na kufika mbali na kama si robo fainali basi hata nusu, lakini hatimaye wakaja kuungana na Ivory Coast mapema katika hatua ya makundi.
Gabon
Wakiwa kama wenyewe wa michuano hiyo walipewa nafasi ya kutumia vizuri viwanja vyao na kuweza kufika mbali, lakini walishindwa kufanya hivyo mbali ya kuwa na nyota wao ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji katika klabu ya Borussia Dortmund, Pierre Aubameyang, ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi ya Ujerumani kwa sasa.
Baada ya kutolewa katika michuano hiyo, Aubameyang aliweka wazi kuwa wametolewa mapema kutokana na uongozi wa timu hiyo kufanya mabadiliko ya kocha ambaye wachezaji walimzoea kwa kiasi kikubwa, kocha huyo alifukuzwa ikiwa ni bado mwezi mmoja kuanza kwa Afcon.
Gabon ilimfukuza kocha wao, Jorge Costa ambaye alikuwa na uhusiano nzuri na wachezaji wa timu hiyo na nafasi yake ikichukuliwa na Jose Antonio ambaye alikuja na kubadili mfumo ambao uliwafanya wachezaji wachukue muda kuuelewa.
Togo
Timu hii haikupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri japokuwa ina wachezaji wengi ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya, lakini baada ya mchezo wao wa kwanza kutoka suluhu dhidi ya mabingwa watetezi, Ivory Coast, walianza kupewa nafasi ya kufika mbali.
Lakini hali ilikuwa tofauti na kujikuta wakichezea kichapo cha mabao matatu katika mchezo wa pili dhidi ya Morocco, huku wakipokea kipigo kingine cha mabao matatu dhidi ya DR Congo, ambapo safari yao ikaishia hapo katika hatua ya makundi.
Katika makundi yote manne, kundi B ambalo lilikuwa na Senegal, Tunisia, Algeria na Zimbabwe huku kundi C likiwa na DR Congo, Morocco, Ivory Coast na Togo, yalionekana kuwa ni makundi magumu kwenye michuano hiyo, hivyo vigogo walikuwa na uwezekano wa kutolewa mapema.