NA MWANDISHI WETU, RUFIJI
ZAIDI ya wakazi 5,000 wa vijiji sita vya Kata ya Mohoro wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, wameweza kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kupitia Mradi wa Elimu kuhusu Afya ya Uzazi na Mtoto.
Mafanikio hayo yamepatikana katika mwaka mmoja kupitia Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Taasisi ya Uzazi na Malezi Bora (Umati).
Takwimu hizo zilitolewa jana na Ofisa wa Programu wa mradi huo wilayani hapa, Radhia Mamboleo.
Alisema mradi huo umehusisha vijiji vya Shela, Mohoro Mashariki, Mohoro Magharibi, Ndundutawa, King’ong’o na Kwaijia.
Radhia alisema mradi huo umeleta mafanikio makubwa ikiwamo kupunguza vifo vya mama na mtoto, wanawake kupata mwamko wa kuhudhuria kliniki kwa wakati muafaka kipindi cha ujauzito na kuboreshwa kwa huduma za uzazi katika vijiji hivyo.
“Mradi umefanikiwa kupunguza maambukizi ya a Ukimwi na kuwapatia wanawake chanjo kwa wakati tofauti na awali.
“Lakini pia mradi huu umefanikiwa kutoa elimu kwa watoa huduma jumuishi (Waja) ambao walipatiwa mafunzo kwa ajili ya kuelimisha jamii jambo ambalo limeongeza uelewa wa masuala ya afya ya mama na mtoto katika jamii ya watu wa Rufiji,” alisema.
Kuhusu changamoto za mradi huo ambao unafikia tamati Oktoba mwaka huu, Radhia alisema kikwazo kikubwa ni maeneo ambayo ufikaji wake ni wa kusuasua.