26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

VIATU VYA DK. SLAA, KUNA MTU VINAMPWAYA

SIKU za nyuma baada ya Rais Magufuli kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) niliandika makala katika gazeti hili hili nikiwausia na kuwatahadharisha Chadema  kuwa wajiandae kisaikolojia maana wanakwenda kupata ushindani mkubwa sasa kile nilichokiandika leo kimetokea, yawezekana isiwe kwa asilimia mia moja lakini kwa sehemu fulani yametimia.

Moja ya vitu vilivyonifanya niandike makala hii ni ripoti ya TWAWEZA iliyotolewa wiki iliyopita ikionesha kushuka kwa asilimia za kuungwa mkono na wananachi kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kutoka asilimia 32 mpaka asilimia 17 mwaka huu. Hili ni anguko kubwa, wapo watakaobeza ripoti hii ya utafiti wa TWAWEZA lakini ili kupingana na ripoti hii wanatakiwa kufanya utafiti wao na kuja na ripoti ndio tutakubaliana nao.

Moja ya vitu vigumu kwa mwanadamu kujifanyia mwenyewe basi huwa ni kujisahihisha, hii si kwa Chadema  tu bali hata kwa mtu mmoja mmoja, mtu anaweza kuwa yupo kwenye nafasi fulani mfano kwenye nafasi ya mfanyabiashara mkubwa anaweza akapewa ushauri kuhusu masuala fulani akakaidi na mbaya zaidi hata yeye mwenyewe asipate muda wa kujifanyia tathimini mpaka atakapoanguka ndio hugundua kuwa kuna mahala alikosea, sasa leo nitasema na Chadema  kuhusu kujisahihisha halafu wiki ijayo nitazungumza na Chama Cha Mapinduzi.

Chadema mnapaswa kujifanyia tathimini upya, moja ya vitu vilivyokipandisha chama hiki miaka ya mwanzoni mwa 2000 basi ni siasa za masuala, siasa ambazo ziliibua vitu ambavyo mwanzoni vingeweza kupingwa lakini kwa kuwa muda haukuwahi kusema uongo yote yalioibuliwa hutokea kuwa kweli mfano turejee sababu zilizomfanya Zitto akafukuzwa bungeni kipindi kile, yale aliyoyasema bungeni yalitokea na hata leo usishangae kusikia baadhi ya majina ya wanasiasa wakitajwa kwenye ripoti ya makinikia ni wale wale waliowahi kutajwa na Mh. Zitto Kabwe, kwa bahati mbaya siku hizi nawaona mmeanguka kutoka kwenye siasa za masuala na hoja mpaka kwenye siasa za kudandia na hii inawafanya chama tawala kuendelea kupeta kwa kuwa wanawafanya ninyi na wananchi wengine kucheza ngoma wanayoipiga mfano ni ripoti ya mchanga.

Changamoto kubwa ambazo mnakutana nazo ni mbili, moja mnashindana na chama dola, pili kutofahamu kwa Watanzania wengi na haya msipoyashughulikia mnaweza kushtuka mmeshaanguka kisiasa. Miaka ya nyuma mlikuwa mnapata uhuru wa kufanya mikutano mkaweza kusambaza elimu ya uraia sehemu mbalimbali lakini hivi sasa mikutano hiyo imepigwa marufuku na hata kujumuika mfano mahafali ya wanafunzi wa vyuo ambao ni wanachama wa chama chenu mahafali hizo huzuiwa lakini haiwi hivyo kwa wafuasi wa chama tawala sasa hili mnatakiwa kuliundia mikakati kulishinda maana huu ni kama mchezo, sheria za mchezo zikiwa ngumu hazikubani wewe kutafuta njia nyingine ya kukabiliana nazo ili upate ushindi.

Pili kutofahamu  kwa Watanzania wengi, nimeona ripoti ya TWAWEZA ikisema kuwa Chama cha Mapinduzi kinaungwa mkono na watu wengi wasiokuwa na elimu, hili nalikubali kwa asilimia mia na kwa bahati nzuri wenzenu CCM wanalijua hili vyema na ndio maana wanapatwa kuungwa mkono maana wananchi wengi wa Tanzania ni watu wasio na elimu, kama hili la Makinikia ni moja ya njia watakazotumia kuwasumbulia kwa sababu wananchi hao wasio na elimu hawatakumbuka tena kuwa ni nani aliyepitisha hiyo mikataba mpaka kulifikisha Taifa hapa lilipo, watasahau kabisa kuwa ni CCM hao hao na watajwa katika ripoti ile ni wanaCCM mashuhuri na wengine wapo bungeni mpaka leo.

Zamani mlifahamu kuwa moja ya sababu zinazofanya maisha kuwa magumu ni ufisadi, yaani si  kwamba pesa haipo hapana bali pesa ipo lakini ipo mikononi kwa watu wachache na mlisema hivyo, mkaibua kashfa nyingi mkaungwa mkono lakini leo hii mambo yamebadilika mtaani pesa hakuna na maisha magumu lakini hamuwaambii watu wakawaelewa na wala hamuibui masuala, tazama juzi Bajeti ya kambi ya rasmi ilivyozimwa na ripoti ya Makinikia utafikiri hamna kilichotokea bungeni.

Rudini chini, mjitafakari wapi mlikosea mjisahihishe, viatu vya Dk. Slaa nahisi kuna mtu vinampwaya. Ripoti ya TWAWEZA  inaonesha wananchi wamepunguza asilimia za kumuunga mkono Rais kwa Zzaidi ya asilimia 20 unafikiri ni kwa nini? Ni kwa sababu maisha yamekuwa magumu lakini nawaona mpo tu, zamani mlitolewa bungeni kwa kuibua kashfa leo mnafukuzwa bungeni kwa kutaka kupigana, waliwafukuza kashfa zikawaumbua zikawapa nafasi Je, leo kufukuzwa bungeni kutakuja kuwaumbua?

Tafakari chukua hatua.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles