MAGUFULI ATAFANIKIWA KUUFUMUA MFUMO

0
673

NA VICTOR MAKINDA


MFUMO ni muundo unaundwa na watu kwa lengo la kuwasaidia watu hao katika maisha yao ya kila siku. Mfumo  hauonekani kwa macho. Ni dhana ya kimuundo ambayo hubeba watu wa jamii  mbalimbali. Mfumo ni muundo unaowaleta pamoja wanamfumo bila kujali kabila, dini wala itikadi.  Mfumo huzingatia  tu maslahi mapana na endelevu ya wanamfumo husika.

Mfumo unapoona hatari ya kufumuliwa hutumia hata vyombo vya kutunga sheria kama vile  Bunge na baadhi ya wabunge ili kujilinda na maadui. Mfumo huenda mbali zaidi hata kutumia vyombo vya usuluhishi na usimazi wa sheria kulinda maslahi ya yake.  Mfumo hutumia viongozi wa kisiasa iwe ni wa upinzani au chama tawala, kutoa utetezi wa kina na kinga madhubuti ili mfumo huo uweze kuishi hai.

Izingatiwe kuwa kuna aina mbili za mifumo, mfumo mbaya na mfumo mzuri. Si mifumo yote ni mibaya, la hasha! Ipo mifumo mizuri yenye tija na faida kubwa kwa mustakabali wa jamii pana. Lakini ikumbukwe na kuzingatiwa kuwa ipo mifumo mibovu na mibaya kabisa inayokinzana na Utawala Bora na haki za raia. Mifumo mibovu ni chanzo cha udumavu wa jamii na ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. Si hayo tu bali mifumo mibovu husheheni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya utu na haki na ni chanzo kikubwa  cha vurugu na vita. Haki inapotoweka amani  hutoweka pia. Amani inapotOweka, vurugu huchukua nafasi ya amani.

Nchi nyingi zimeingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya kuikumbatia mifumo inayokinzana na Utawala Bora na haki sawa kwa wote. Tuna mifano mingi ya nchi hizo. Mojawapo ni kile kinachotokea nchini Rwanda. Nazungumzia mauaji  ya Kimbari ya mwaka 1994  yaliyoua malaki ya Wanyarwanda na kuacha yatima wengi na makovu makubwa kwa wananchi wa nchi hiyo.  Tunaelezwa kuwa sababu kubwa ya mauaji hayo ni mfumo mbovu wa utawala uliokuwa ukiegemea katika ukabila. Wanyarwanda na ulimwengu kwa ujumla, hawatosahau kamwe kilichotokea.

Zipo nchi nyingi duniani zinazopigana vita kila kukicha. Vita hivyo hupiganwa dhidi ya mifumo kandamizi inayowapendelea watu wa jamii au koo fulani iwe ni kisiasa au kijamii. Mifumo mibovu ya rasilimali za nchi na mgawanyo sawa wa mapato yatokanayo na rasilimali hizo, hauiachi  nchi hiyo salama. Ipo mifano pia, Kongo,  Zimbabwe, Angola Sudan ya Kusini Nigeria ni mifano ya nchi chache ambzo zilipigana au bado zinapigana vita inayotokana na mfumo wa mgawanyo wa rasilimali za nchi.

Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi mno. Ninaweza kusema kuwa mwenyezi Mungu ametujalia na kutupendelea kila aina ya rasilimali ambazo kama zikitumiwa vizuri, hakuna mwananchi atakayekufa kwa kukosa iwe ni chakula au dawa. Cha ajabu maisha ya Watanzania walio wengi ni kinyume chake. Tatizo nini? Jibu ni jepesi kabisa. Tatizo ni mfumo mbaya uliojengwa na kuimarishwa na wanamfumo mbaya ambao hautoi fursa sahihi za usimamizi na mgawanyo mzuri wa rasilimali.

Miongozi mwa rasilimali tulizonazo ni ni ardhi kubwa yenye rutba na mabonde oevu. Tumejaaliwa misitu minene yenye miti mingi, hata miti mrefu  Tanzania. Tumejaaliwa wanyama pori wa aina mbali mbali ambao ni kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na nje.

Tanzania  tumejaaliwa kupata mito mingi ambayo inaweza kutumika kumwagilia mazao ya kilimo na hata uvuvi. Tumejaaliwa kuwa na mlima mrefu kuliko yote barani Afrika. Tumejaaliwa kuwa na bahari na maziwa ambayo ikiwa yatatumika vizuri kwa ajili ya shughuli za uvuvi, usafirishaji na utalii basi kulala njaa Tanzania ingelikuwa ni ndoto.

Ni vigumu mno kuorodhesha rasilimali zilizopo nchini. Si kwa sabaau hazipo, hapana, ni kwa sababu tuna lundo la rasilimali ambazo kuziorodhesha inaweza ikachukua kurasa zote za gazeti hili na bado  orodha isiwe imekamilika. Cha ajabu bado tunakabiliwa na umaskini wa kutupwa licha ya lundo la rasilimali linalochangiwa na rasilimali muhimu kabisa, rasilimali watu waliojaa mioyo ya amani na utulivu.

Leo hii, mjadala wangu utajielekeza sehemu moja tu. Nitaangazia juu ya rasilimali madini pekee ambayo imeonesha kuwa kama ikisimamiwa vizuri basi ile ahadi ya kuifanya nchi yetu kuwa na wakazi wanaoshi maisha bora isiwe ni ndoto.

Tunayo kwa wingi madini ya  almasi, dhahabu, ulanga, chuma, magadi, uraniamu, rubi chokaa na makaa ya mawe.  Tuna gesi mamilioni ya tani za ujazo na kuna hati hati ya kupata mafuta hivi karibuni. Tunayo madini ambayo tunayo sisi tu, madini ya kipekee yenye mng’aro wa kusisimua na kushangaza madini yaliyobeba jina la nchi yetu Tanzanite.

Madini haya licha ya kuwa na thamani kubwa, hayapatikani mahali pengine popote duniani. Cha ajabu ni kwamba wauzaji na wasambazi wakubwa madini haya ni Kenya, Afrika Kusini na India. Sisi tunachimba tu na kuambulia pesa kidogo.

Nasema kwa sauti kubwa,  mfumo mbovu wa usimamizi wa sekta hii iliyojaa utajirisho, ndiyo chanzo kikuu cha ufukara wetu.  Wakongwe na waumini waliobobea katika  mifumo ya ubinafsi, ulafi na ufisadi, wamehodhi na kupitisha mikataba kandamizi kabisa ya uchimbaji wa madini yetu tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu huku wawekezaji wakiondoka na madini yenye thamani kubwa, maskini  Watanzania tuliambulia visenti kidogo, tunaviita Mrahaba.

Wanamfumo kandamizi wameigawa migodi yetu kwa wawekezaji uchwara kwa bei ya kutupa na kwa mikataba ambayo kwa kuusema ukweli kabisa haina tija si tu kwa Watanzania bali pia hata wale waishio pembezoni mwa migodi hiyo. Ukitaka kulifahamu hili nenda katembelee kwenye vijiji vya jirani vinavyozunguka migodi mikubwa ya uchimbaji wa madini.  Hapo utayaona maisha halisi ya wananchi waishio juu ya ardhi tajiri wakiogelea umaskini  wa kutupwa huku  wakikabiliwa na adha ya ukosefu wa  maji, hospitali, shule, miundombinu mibovu na kila aina ya madhila ya kibinadamu.

Tazito linabaki pale pale na ni lile lile, nalo ni kwamba tuna mfumo mbovu wa usimamizi wa rasilimali zetu. Mfumo wa usimamizi wa rasilimali zetu umejaa ufisadi na ubinafsi uliopindukia.   Usimamizi wa rasilaimali madini ni kichaka kikubwa cha waumini wa mfumo wa rushwa kubwa kubwa wanapojificha. Ripoti za tume mbili alizoziunda  Dk. John Magufuli, kuchunguza kuhusu mikataba ya madini na mchanga wa dhahabu maarufu kama makinikia, zimeuacha na kuwaacha uchi wanamfumo  waliosimamia mikataba ya madini yetu.

Tumedhulumiwa mattilioni ya shilingi. Tujiulize, Je, waliopewa dhamana ya kuisimamia rasilimali hii muhimu  hawakuwa na weledi wa kisheria kujua namna nzuri ya kuingia mikataba yenye tija na wawekezaji? Je, hawakujua kuwa mikataba wanayoingia haina tija kwa watanzania bali ilikuwa inawanufaisha zaidi wawekezaji.?  Ni kweli kuwa hawakunufaika na chochote wao binafsi kwa kukubali kusaini mikataba ambayo ninaamini kabisa walibaini upungufu wake?

Ukweli  ni kwamba walikuwa wanajua kila kitu. Hawa walifanya kusudi. Walijiundia mfumo wao wa upigaji. Hawakuwa na hawana uchungu na rasilimali zetu zitufaidishe Watanzania.

Waliangalia  zaidi matumbo yao na watu wao wa karibu. Ninaamini kuwa kwa ufisadi huo mkubwa walioufanya, wachimbaji  kwa  maana ya wamiliki wa migodi na waliosaini mikataba isiyo na tija ya kukubali kuchimbwa madini yetu kwa hasara, wameneemeka sana na kwa muda mrefu.

Sina shaka hawa ni mabilionea wakubwa kwa sasa. Wanaweza kuwa wamejijengea mifumo imara yenye uwezo wa kupambana na dhamira njema ya Rais Magufuli, dhamira ya kuufumua mfumo mbovu wa usimamizi wa madini, sheria na mikataba ya uchimbaji wa madini. Pia wanaweza wakawa na uwezo na nguvu imara ya kumfumua yeyote anayetaka kuufumua mfumo wao dharlimu. Ikifika hapo ndipo ninapojiuliza swali hili, Rais John Magufuli, atafanikiwa kuufumua mfumo huu kandamizi na wa kifisadi?

Nikimtazama usoni Rais Dk.. Magufuli, siipati shaka yoyote. Ninaamini kuwa anayo dhamira ya dhati. Anao uwezo wa kuufumua mfumo huu wa ufisadi wa madini pamoja na mifumo yote mibovu.

Mfumo wa utolewaji huduma za jamii uliojaa urasimu, rushwa na ufisadi kwa sasa naweza kusema kuwa kama sio kuzimia basi unaelekea kufa kabisa. Mfumo wa usambazwaji na uuzwaji wa madawa ya kulevya unaelekea kufa pia. Mfumo wa uonevu, upendeleo, kughushi nyaraka na urasimu, unakaribia kufa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here