LIVERPOOL, ENGLAND
BEKI wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk, amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo baada ya safu yake ya ulinzi kuruhusu mabao matatu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi dhidi ya Red Bull, Jumatano wiki hii.
Katika mchezo huo ambao Liverpool walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani walifanikiwa kushinda kwa mabao 4-3, lakini mashabiki walishangaa kuona safu yao ya ulinzi inaruhusu mabao matatu ambapo ni idadi kubwa ya mabao.
Kitendo hicho kimempa wakati mgumu beki hiyo wa kati, lakini amewatoa wasiwasi mashabiki na kuwaambia makosa waliyoyafanya hayawezi kurudiwa tena.
“Bila shaka kila shabiki lazima achukizwe, lakini wanatakiwa kujua tulishinda mchezo huo, hivyo hakuna sababu ya kutoa lawama, kwa sasa siangalii mabaya tuliyoyafanya, ila ninachokiangalia ni jinsi gani tutaisaidia timu kufanya vizuri.
“Kikubwa mashabiki wanatakiwa kujua kwamba sisi ni binadamu, hatuwezi kufanya vizuri muda wote, kuna wakati tutakuwa tunakosea, hivyo kuna wakati kuzidiwa inatokea lakini sio kusudio la wachezaji kufanya vibaya.
“Lakini jambo zuri ni kwamba bado tunaendelea kufanya vizuri msimu huu, ila mashabiki wajue hata sisi wachezaji hatukuwa sawa baada ya kuruhusu mabao matatu japokuwa tulishinda mchezo huo.
“Hakuna sababu ya mashabiki kuchukia, wanatakiwa kutulia na kuangalia jinsi gani tutakuja kivingine kwenye michezo inayofuata, tunatarajia kucheza dhidi ya Leicester City, tunaamini tutafanya vizuri kwenye mchezo huo,” alisema beki huyo.
Leicester City ambayo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi nchini England, ipo chini ya kocha wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers, hivyo mchezo huo wa leo utakuwa na ushindani wa hali ya juu japokuwa Liver watakuwa nyumbani.
Rodgers alikuwa Liverpool tangu mwaka 2012 hadi 2015 alipokwenda kujiunga na timu ya Celtic kabla ya mwaka huu kupewa jukumu hilo Leicester City.