Mambo 10 ya kujifunza yaliyotokea Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki hii

0
2277

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

HII ilikuwa wiki nyingine ya kuona wababe wa soka nini wakikifanya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya pili ya makundi baada ya wiki mbili zilizopita michezo ya kwanza kupigwa.

Michezo 16 ilipigwa wiki hii kati ya Jumanne na Jumatano, kulikuwa na mambo mbalimbali yalitokea na kuacha mjadala, ila tumekuanikia mambo 10 ya kujifunza yaliyotekea kwenye michezo hiyo katikati ya wiki.

Hatari kwa Mauricio Pochettino

Kocha wa timu ya Tottenham, Mauricio Pochettino, msimu uliopita kwenye michuano hii alionekana kuwa mmoja wa makocha bora kutokana na kuifikisha fainali Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool.

Lakini msimu huu unaonekana kuwa mbaya kwake baada ya kuanza na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Olympiacos, lakini wiki hii Tottenham walikutana na kipigo kitakatifu cha mabao 7-2 dhidi ya wababe wa soka nchini Ujerumani, Bayern Munich, huku Tottenham wakiwa nyumbani. Hivyo akishindwa kufanya vizuri michezo inayofuata safari ya kufukuzwa inaweza ikamkuta.

Serge Gnabry aibeba Bayern

Huyu ni nyota wa zamani wa Arsenal ambaye kwa sasa anakipiga katika kikosi hicho cha Bayern Munich. Kiwango ambacho alikionesha kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham kiliwashangaza wengi.

Katika ushindi wa mabao 7-2, yeye alicheka na nyavu mara nne, jambo ambalo viongozi wa timu hiyo na wachezaji waliamua kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kumuomba asimame katikati yao na kisha kumpigia makofi ya heshima kwa kile alichokifanya.

Mabao manne aliyoyafunga mchezaji huyo yaliwafanya mashabiki wa Arsenal wabaki na maswali mengi huku wakivuta picha kama mchezaji huyo ambaye walimuacha mwaka 2016 aondoke, leo hii angewasaidia kwa kiasi gani kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Chelsea itafaidika na Fikayo Tomori

Huyu ni kijana mwenye umri wa miaka 21, akitokea timu ya vijana na kupelekwa kwenye klabu mbalimbali kwa mkopo ikiwa pamoja na Brighton, Hull City na Derby County kabla ya kiangazi mwaka huu kurudishwa kikosini.

Kocha wa timu hiyo Frank Lampard amekuwa akiwatumia wachezaji wengi chipukizi kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya usajili baada ya kufungiwa, hivyo Tomari alionesha kiwango cha hali ya juu katika safu ya ulinzi dhidi ya Lille huku Chelsea ikishinda mabao 2-1. Mchezaji huyo alionesha kiwango cha hali ya juu.

Real Madrid haiogopwi

‘Hat-trick’ ambayo aliipata kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ya kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo liliwaogopesha wapinzani, lakini tangu msimu uliopita hadi sasa timu hiyo inaonekana kuwa ya kawaida.

Mchezo wao wa kwanza hatua ya makundi walikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya PSG, hao walikuwa wakubwa tupu, lakini wiki hii Madrid wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani Santiago Bernabeu na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Club Brugge.

Hata hivyo Club Brugge walianza kuwa mbele kwa mabao mawili kabla ya Sergio Ramos na Casemiro kusawazisha dakika za lala salama. Club Brugge imeziaminisha klabu zingine kuwa Madrid haitishi msimu huu. Inashika nafasi ya mwisho kwenye kundi lao.

Inter Milan imerudi

Baadhi ya watu wataikumbuka timu ya Inter Milan ya miaka 90, ambayo ilichukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa na mastaa kama vile Ronaldo de Lima, Ivan Zamorano na Diego Simeone. Baada ya hapo kocha Jose Mourinho alifanya makubwa mwaka 2010 kwa kuzifunga timu kubwa kama vile Chelsea, Barcelona na Bayern Munich na kutwaa ubingwa huo.

Baada ya hapo Inter Milan ikapotea kwenye ubora wao, lakini sasa inaonekana kurudi japokuwa ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Barcelona kwenye uwanja wa Camp Nou, Jumatano wiki hii, ila inaonesha kuwa kocha wa timu hiyo Antonio Conte anairudisha kwenye ubora.

Bila ya kujali kuongeza kwenye msimamo wa Ligi nchini Italia, lakini kwa jinsi walivyokuwa wanaishambulia Barcelona na kuongoza bao kupitia kwa mchezaji wao Lautaro Martinez, inavutia kuitazama.

Kumbe Liverpool inapitika

Liverpool ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, uimara wao kwenye safu ya ulinzi na ubora wa safu ya ushambuliaji uliifanya timu hiyo kutwaa ubingwa msimu uliopita, lakini timu ya Red Bull imeonesha kuwa Liverpool wanapitika.

Kwenye mchezo wa Jumatano, Liverpool walikuwa wanaongoza mabao matatu hadi dakika ya 36, lakini kuanzia dakika ya 39 Red Bull waliweza kupata bao la kwanza hadi kusawazisha kabla ya Liverpool kupata bao la ushindi dakika ya 69 na kuwa mabao 4-3.

Phil Foden apewe nafasi

Huyu ni kiungo aliyetokea timu ya vijana, amekuwa na msaada mkubwa kila wakati akipata nafasi, hata hivyo amekuwa akipewa nafasi chache sana. Msimu huu amepata nafasi ya kucheza dakika 10 tu kwenye Ligi Kuu England.

Lakini kutokana na kile alichokifanya kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Diamo Zagreb na kufunga bao dakika ya 90, kumewafanya mashabiki watumia kurasa za mitandao ya kijamii kumwambia kocha wake Pep Guardiola ampe nafasi ya kutosha.

Ajax bila De Jong, De Ligt inawezekana

Hawa ni nyota ambao walikuwa na mchango mkubwa msimu uliopita na kuifanya timu hiyo ifike nusu fainali, lakini kiwango chao kilizifanya klabu mbalimbali kuwania saini zao na hatimaye De Jong akajiunga na Barcelona, huku De Ligt akitua Juventus na Kasper Dolberg akijiunga Nice.

Kuondoka kwao kuliwaaminisha wengi kuwa timu hiyo itakuwa na wakati mgumu, lakini bado imeonesha kiwango cha hali ya juu dhidi ya Valencia wakishinda mabao 3-0, huku mchezo wa kwanza kabisa wakishinda mabao 3-0 dhidi ya Lille.

Real Madrid walikosea kwa Achraf Hakimi?

Timu ya Real Madrid inaonekana kufanya makosa kumtoa kwa mkopo mchezaji huyo ambaye alijiunga na Borussia Dortmund. Ndani ya klabu hiyo ameonesha ubora katika nafasi yake safu ya ulinzi, wakati huo Madrid kwenye ulinzi ni tatizo.

Dortmund walitoka bila kufungana na Barcelona kwenye mchezo wa kwanza, huku wakija kushinda mabao 2-0 dhidi ya Slavia Prague.

Ronaldo aishikiria rekodi

Cristiano Ronaldo ni mchezaji ambaye bado anaongoza kwa kuwa na mabao mengi kwenye michuano hiyo ikiwa anafunga kila msimu kwa miaka 15 sasa, hivyo ana jumla ya mabao 127 akifuatiwa na Messi mwenye mabao 112.

Ronaldo ameifungia bao moja klabu yake ya Juventus kwenye mchezo dhidi ya Bayer Leverkusen huku Juventus ikishinda mabao 3-0.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here