23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UZINDUZI RIPOTI YA UTAFITI WAZUIWA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SERIKALI imelizuia Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (Human Rights Watch) kuzindua ripoti inayoelezea namna wafanyakazi wa ndani wa kitanzania wanavyonyanyaswa katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Utafiti huo ulifanywa na shirika hilo hapa nchini kwa kuwahoji wasichana kadhaa waliowahi kufanya kazi nchi za UAE na jana ripoti hiyo ilitarajiwa kuzinduliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. William Kindeketa, alisema watafiti hao hawakufuata taratibu zinazotakiwa na wala hawakuwa na kibali cha kufanya utafiti huo.

“Tulivyomuhoji huyu mtafiti tumebaini alikuwa hajapitia taratibu zinazotakiwa, hana viza ya utafiti wala kitu chochote, ndio maana tulimwambia hili ni kosa,” alisema Dk. Kindeketa.

Alisema kabla ya kufanya utafiti, mtu au shirika anatakiwa aandike dokezo na kuliwasilisha Costech kwa ajili ya kupitiwa na kamati maalumu inayohusika na masuala ya utafiti na kama likikidhi vigezo muhusika hupewa kibali cha kuendelea na utafiti wake.

“Katika nchi yoyote ukitaka kufanya utafiti lazima ufuate utaratibu, hata hapa kwetu tuna utaratibu huo. Uwe utafiti wa kijamii, sayansi au wowote ule Costech ndio wenye mamlaka.

“Unatakiwa uandike dokezo lako kisha unaliwasilisha Costech, wataalamu wataliangalia halafu litapelekwa kwenye kamati ya taifa ya kusajili tafiti, wao wanaweza kulikataa ama kulikubali.

“Na kama si Mtanzania ukishapata kibali lazima uende uhamiaji kupata kibali cha ukaazi. Utafiti huu umefanyika hapa kwa kuhoji wafanyakazi ambao walisharudi kutoka Oman lakini wahusika hawakufuata utaratibu na hili ni somo katika taasisi zingine,” alisema.

Naye Mtafiti wa Human Rights Watch katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, Rothna Begum, alisema walifuata taratibu lakini wameshangaa kuzuiliwa kuzindua ripoti hiyo.

“Leo (jana) asubuhi kuna maafisa kutoka Costech wamekuja na kutuambia kwamba hatukufuata taratibu za kufanya utafiti huu hivyo, haturuhusiwi kuizindua ripoti yetu.

“Tumefuata taratibu zote ambazo huwa zinatakiwa kabla ya kufanya utafiti na tulikuwa na mikutano na wizara tofauti kabla ya kuja hapa kutaka kuizindua ripoti hii.

“Tumekuja mara nyingi Tanzania kuzindua ripoti lakini kwa hii ya leo (jana) wamesema kwamba kuna taratibu ambazo hatujazifuata.

“Huwa tunaandika barua kwa serikali na kuwaambia kuhusu utafiti tunaotaka kuufanya na tulizungumza nao na mazungumzo yalikuwa mazuri hadi sasa,” alisema Begum.

ILIVYOKUWA

Uzinduzi wa ripoti hiyo ulipangwa kufanyika katika Hoteli ya Holday Inn, Dar es Salaam na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari walialikwa kuhudhuria.

Waandishi walipofika waligawiwa nakala za ripoti hiyo lakini kabla ya kuanza kwa mkutano huo, ghafla walifika maofisa wawili wa serikali Dk. Kindeketa na mwingine aliyetambulika kama Ally Kapola na kulizuia shirika hilo lisiendelee na uzinduzi huo.

Hali hiyo ilisababisha maafisa wa shirika hilo kutoka nje ya ukumbi kwenda kujadiliana na maofisa hao wa serikali huku waandishi wakiendelea kusubiri.

Majadiliano hayo yaliyodumu kwa dakika kadhaa hayakufua dafu kwani maofisa wa shirika hilo na waandishi wa habari waliamriwa waondoke eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles