24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uzalishaji wa umeme na gesi asilia waongezeka

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

IMEELEZWA kuwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyoungwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia megawati 1,777.05 Desemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.87, ikilinganishwa na megawati 1,694.55 zilizokuwepo hadi kufikia Septemba 2022.

Waziri wa Nishati, MhJanuary Makamba akizungumza wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha mwezi Julai-Desemba, 2022. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato na wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Aidha, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 jumla ya futi za ujazo milioni 38,172 za Gesi Asilia zilizalishwa katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay ambapo uzalishaji wa Gesi asilia umeongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na kipindi Julai hadi Desemba, mwaka 2021 ambapo futi za ujazo 29,996 zilizalishwa.

Hayo yameelezwa Januari, 20, 2023 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ikiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba ilipowasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati Taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha mwezi Julai-Desemba, 2022.

Waziri wa Nishati, amesema kuwa, ongezeko la uwezo wa mitambo hiyo ya kuzalisha umeme iliyoungwa katika mfumo wa gridi limetokana kuingizwa katika Gridi ya Taifa megawati 90 za umeme zinazozalishwa katika Kituo cha Kinyerezi I Extension.

Aidha, amesema kuwa, uwezo wa kuzalisha umeme kwa mitambo ambayo haijaunganishwa katika Gridi ya Taifa umefikia megawati 39.302 na hivyo kufanya jumla ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kufikia megawati 1,816.352 ikilinganishwa na megawati 1,733.38 zilizokuwepo mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.89.

Kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji wa Gesi asilia amesema kuwa “ongezeko hili limetokana na ufungaji wa kompresa tatu katika Kitalu cha Songosongo ambazo zimeongeza mgandamizo na msukumo wa Gesi kutoka kisimani na sasa wastani wa futi za ujazo milioni 240 zinazalishwa kwa siku kutoka katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha mwezi Julai-Desemba, 2022. Wa Pili kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati. Mhe.January Makamba na wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Gesi hiyo inayozalishwa, inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani, kwenye Taasisi, magari na uzalishaji wa wastani wa asilimia 62 ya umeme wa Gridi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati pamoja na kuishukuru Wizara kwa kuwasilisha utekelezaji wa Bajeti yake, alitoa maelekezo mbalimbali yatakayosaidia kutekeleza bajeti hiyo kwa ufanisi zaidi.

Katika kikao hicho na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wizara pia ilieleza utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya Gesi na Umeme mijini na vijijini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Maneno matupu hayasaidii
    Leo katika maeneo ya Gerezani/Kariakoo hatujapata umeme masaa 24. Tanesco imekaa kimya bila ya kuomba msamaha au kueleza katizo hilo la umeme. Wadau na wateja wana haki ya kuelezwa. Wao si watoto

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles