26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UVUVI HARAMU WAPUNGUA DAR ES SALAAM

UVUVI HARAMU WAPUNGUA DAR


UVUVI haramu ukihusisha wale wasio na leseni na wale wanaotumia njia haramu za uvuvi, unapigwa vita kwa marefu na mapana ili kulinda mazalio ya samaki na kuwa na mazingira endelevu.

Vita hiyo inaendeshwa na wadau wote wa biashara ya uvuvi kwa masilahi ya vizazi vya sasa na vya baadaye.

Juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kama inavyoshuhudiwa na wadau mbalimbali.

Uongozi wa Soko la Samaki Feri jijini Dar es Salaam, umesema uvuvi haramu umepungua kwa kiasi kikubwa tangu walipokamata tani 1.7 za samaki waliovuliwa kwa njia ya magendo na kuwateketeza bayana mbele ya mashahidi.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Asha Zewe, alisema Desemba 16, mwaka jana walikamata samaki hao ambao walikuwa na thamani ya Sh milioni 11 na kuwateketeza, kitu ambacho kimewaogopesha waliokuwa na tabia hiyo mbaya na ya uharibifu kwa ustawi wa sekta hiyo.

Zewe alisema kwa sasa wameboresha ukaguzi kuanzia kwenye maboti na hata samaki wanaotoka nje ya Dar es Salaam kama Bagamoyo, Mafia, Temeke na Kisiju kuingizwa sokoni hapo.

“Maofisa uvuvi wameongezeka watatu ili kuwa na nguvu zaidi na wale samaki wanaoingizwa usiku hawaruhusiwi kuuzwa hadi asubuhi atakapokuja Ofisa Uvuvi na kufanya ukaguzi,” alisema.

Alisema operesheni wanayoifanya kwa sasa inaendana na kukamata maboti yasiyo na namba ambayo yanaaminika ndiyo yanaongoza kwa uvuvi haramu na uharamia baharini.

“Hata askari pia tumewaongeza kutoka saba hadi 14 ili kuwadhibiti wale wote wanaotaka kujinufaisha kupitia uvuvi,” alisema.

Uvuvi wa kokoro umedhibitiwa eneo lote la bahari ili kulinda mazalio na samaki wadogo na wachanga.

 “Sokoni Feri tumepiga marufuku uingizaji wa samaki wachanga sokoni ambao mara nyingi wanavuliwa kwa kokoro,” aliongeza Asha.

Alisema kufanikiwa kudhibiti uvuvi haramu kunatokana na kuwepo kwa ushirikiano baina yao na kikosi cha doria kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

“Sisi kama Halmashauri ya Ilala, hatuwezi kufanya doria sehemu yote kwa sababu bahari imekatiza eneo kubwa la Dar es Salaam si manispaa yetu pekee,” alisema Asha.

Alisema kutokana na kushirikiana na Wizara, wenye vifaa na rasilimali  nyingi wameweza kujiongeza na wanaweza kufanya doria eneo kubwa zaidi na ndiyo sababu uvuvi haramu unaendelea kupungua kadiri muda unavyokwenda.

Asha amewataka wanunuzi na walaji wa samaki kuangalia vigezo vyote vya samaki wabovu wanaouzwa mitaani kwani ni hatari kwa afya zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles