24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

UVCCM YAJIBU MAPIGO YA LOWASSA

Na Mwandishi  Wetu,

-DAR ES SALAAM

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umemtaka Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, kufuta fikra ya kuwa Chadema ya kukibwaga chama tawala hata kama kutakuwa na Ukawa.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Lowassa kulaani hatua ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, kuzuia kongamano la demokrasia ambapo alisema CCM mwaka 2020 inaweza kupulizwa kwa upepo kama inzi anavyotolewa kwenye bilauli la maziwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM,  Shaka Hamdu Shaka, alisema kwa bahati mbaya Lowassa amesukumwa na hasira  na kujikuta  akajitoa CCM  mwaka 2015 kama mtu aliyekuwa anacheza ngoma kwa kwenda upinzani, huku akiwa na matumaini ya kuukwaa urais.

Alisema kama kuna kosa ambalo Lowassa amelifanya ni kuihama CCM na kujiunga upinzani hasa Chadema kwa sababu yeye mwenyewe ameshawahi kutamka hadharani akihutubia mkutano wa hadhara mwaka 2006 akilinganisha upinzani na watoto wanaokimbilia  mdundiko.

“Lowassa asikubali kucheze tombola katika siasa, siasa ni hesabu na fomula zake, nafikiri  amekurupuka kujiondoa CCM, ameupanda mkenge kwenda Chadema, ajue si Ukawa wala udeta wenye ubavu wa kuiondosha CCM madarakani,” alisema Shaka.

Alimtaka Lowassa kujua kuwa  hata viongozi na wanachama wa upinzani hawamwafiki mwanasiasa huyo kwa asilimia kubwa, kwani wapo viongozi aliowakuta ambao  wametoa jasho jingi kuvijenga vyama vyao hivyo hawako tayari kumpisha agombee tena urais.

Akijibu hoja na madai yaliyotolewa na Lowasa aliyesema kuna ukandamizaji wa demokrasia, Shaka alisema  haiba ya demokrasia iliopo Tanzania  huwezi kukutana nayo mahali popote Afrika, Afrika Mashariki na duniani ila uamuzi wa Serikali  ya Awamu ya Tano ni kuwahimiza wananchi kufanya kazi na kuzalisha mali viwandani na mashambani .

“Uhuru, demokrasia au watu kujitawala bila shibe na maendeleo ya kisekta ni upuuzi, tumemaliza kampeni na uchaguzi mkuu kila mmoja sasa afanye kazi, kukusanya watu kwenye makongamano na kuwapa bahashish ni kuwapumbaza kiakili  ikiwa bado ni masikini,” alisema.

Alisema Serikali yoyote ni taasisi pana yenye mikono mingi ya kiutendaji ambayo kwa kadiri itakavyofanya  na kutenda kutimiza yote kwa niaba ya hadhi  ya nafasi ya rais, hivyo hakuna mantiki yoyote viongozi wa nchi kukusanyana mahali pamoja kama utitiri au kundi la nzige.

“Akifika mahali popote mteule wa rais na wateule wengine kwa mintaraf ya  uwakilishi, huwakilishwa rais na madaraka yake, rais hawezi kuwa kama Mungu wa madhehebu fulani mwenye mikono saba, vinginevyo Lowassa aseme alihitaji nini rais afike mahali hapo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles